*Ni baada ya kugundua kuwa mkewe hajakeketwa

*Amkeketa kwa nguvu ili akubalike kwenye familia

*Dawati la Jinsia Mugumu lashindwa kutoa msaada

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Serengeti

WAKATI jamii ikipambana kukomesha vitendo vya ukeketaji, hali ni tofauti ndani ya familia moja katika Kijiji cha Mbalibali, Serengeti mkoani Mara; JAMHURI linaripoti.

Taarifa kutoka kijijini hapo zinadai kuwa Agosti mwaka huu, binti mmoja mwenye umri wa miaka 20 amekeketwa kwa nguvu mara tu baada ya kuolewa.

Akizungumza na JAMHURI, binti huyo (jina linahifadhiwa) amesema hakutarajia kufanyiwa ukatili huo maishani mwake.

Huku akitokwa machozi, anasema: “Kwetu tumezaliwa wasichana tisa na kulelewa katika misingi ya dini. Hakuna aliyekeketwa. Kwa nini leo nifanyiwe hivi baada ya kuolewa?”

Anasema amekeketwa kwa nguvu na kusababishiwa kupata maambukizi ya fangasi sehemu za siri, kisha mumewe, kwa dharau, akamrudisha kwao akatibiwe na baba yake.

Anasema sasa anahisi kuwa thamani ya utu wake mbele ya jamii imedorora na kwisha kabisa.

Ilivyotokea

Agosti 2, 2024 binti huyo aliamini kuwa ndiyo siku ya kukumbukwa zaidi kwani ilibadili historia ya maisha yake baada ya kufunga ndoa.

“Niliona fahari sana kwa kuwaheshimisha wazazi wangu, na wao wakaniaga kwa furaha kubwa na kunipa zawadi mbalimbali.

“Lakini siku nne tu baadaye, dunia ikageuka na kuwa yenye mateso makubwa kwangu,” anasema.

Siku hiyo, baada ya chakula cha jioni wakati wanakwenda kulala, mume wake, Maina Marwa Chokera (34), akabaki sebuleni akizungumza na mama yake, yaani mama mkwe wa binti huyo.

Anasema baadaye wakamwita na kumuuliza iwapo amekeketwa.

“Nikawajibu kwamba kwetu hatukeketwi. Wakanyamaza, mimi nikaondoka lakini mwenzangu akabaki na kuendelea kuzungumza na mama. Sikujua wameongea nini, baadaye akaja, tukalala,” amesema.

Anasema Agosti 6, mwaka huu saa sita usiku, wakiwa wamelala, alisikia mlango unagongwa, mumewe akaamka.

“Nikamuuliza hawa wageni wa usiku ni kina nani? Hakunijibu, badala yake akaenda kuwafungulia. Mimi nikaamka, nikajifunga nguo, nikakaa chumbani kwenye kiti.

“Mara, mume wangu akiongozana na mama yake, vijana wawili na mwanamke mmoja, wote wakiwa wameficha nyuso zao, wakaja chumbani na kuniambia ni lazima wanikekete ili kutimiza sharti la marehemu baba mkwe.

“Kwamba baba yake mume wangu aliacha wosia kwamba ndani ya mji wake asiingie mwanamke ambaye hajakeketwa,” amesema.

Anasema watu hao walimdhibiti na kumziba mdomo asipige kelele, wakamwangusha chini.

“Wale vijana wawili, mama mkwe na mume wangu walisaidiana kunibana, kisha yule mwanamke waliyekuja naye, kumbe ni ngariba, akanikeketa. Wakaondoka,” anasema akitokwa machozi.

Usiku huo ukayabadili maisha yake na hukupata usingizi tena, akabaki akilia kutokana na ukatili aliotendewa huku akivuja damu kwa wingi.

Asubuhi akafungiwa ndani kwa hofu kwamba huenda angetoroka.

“Sikumtaarifu mtu yeyote kwa kuwa simu haikuwa na chaji na mume wangi aligoma kwenda kunichajia. Alijua kwamba ningewataarifu wazazi wangu,” anasema.

Mchana wa siku hiyo mama mkwe wake alimpelekea chakula na siku mbili baadaye, Agosti 8, 2024, akapata nafasi ya kumpigia simu baba yake na kumweleza ukatili aliotendewa.

“Baba hakuwapo. Alikuwa safarini, akaniambia nitoe ripoti Kituo cha Polisi na kutafuta matibabu haraka.

“Pamoja na maumivu niliyokuwa nayo, nilitoka kijijini kwa mguu hadi kwa dada yangu anayeishi Mugumu. Nikamweleza ushauri alionipa baba.

“Akanisindikiza hadi kwenye Dawati la Polisi la Jinsia. Kati ya Agosti 12 hadi 14 nilipata vipimo na matibabu. Hospitali ya Nyerere wakabaini kuwa nina maambukizi ya fangasi yaliyotokana na kukeketwa,” anasema.

Ndoa ya binti huyo iliyofungwa Agosti 2, 2024 ikitanguliwa na tukio la mahari lililofanyika Juni mwaka huu, ikawa imefika mwisho na kuvunjika ndani ya wiki moja tu, kila upande ukitoa sababu zake.

Ukeketaji unavyofanyika

Tukio hilo limezua gumzo kubwa kijijini Mbalibali kwa kuwa limetendeka kinyume cha utaratibu uliozoeleka.

JAMHURI limeelezwa kwamba kwa mujibu wa taratibu, mila na desturi za maeneo hayo, wanawake ambao hawajakeketwa huandaliwa ngariba kwa siri na hukeketwa wakati wa kujifungua ili kuhararishwa kuingia kwenye familia ya mume.

Wilayani Longido mkoani Arusha, mbinu inayotumiwa siku hizi, watoto wadogo hukeketwa wakati wa sherehe za ubatizo au kipaimara.

Watuhumiwa wataka yaishe

Binti aliyefanyiwa ukatili anasema baada ya kutoa ripoti polisi, mume wake na mama mkwe walikamatwa na kuwekwa mahabusu.

“Wakaniomba wakitaka mambo haya yaishe kwa kunilipa fidia ya fedha kwa ukatili walionifanyia.

“Kituo cha Polisi Mugumu kikageuka mnadani. Pakawa sehemu ya kupangiana bei kwa madhara niliyopata.

“Mimi nikakataa. Nikataka watuhumiwa hao wakatili wapelekwe mahakamani. Ndugu wakaingilia kati na kutaka tuyamalize kifamilia,” anasema.

Anasema alitaka shauri liende mahakamani kwa kuwa kati ya waliomfanyia ukatili, aliwatambua wawili tu na hao, mumewe na mkwewe, walikri mbele ya polisi.

Anawalaumu polisi kwa kutosimamia utaratibu wa kutoa haki, badala yake kugeuka sehemu ya kutaka kumaliza matatizo kinyemela.

Anasema baada ya majadiliano, akadai alipwe Sh milioni 5 na kurudishiwa nguo na vifaa vyake alivyoviacha kwa mume wake.

Hata hivyo, katika mjadala huo mumewe akasema kuwa wao wapo tayari kutoa Sh milioni 2.5, lakini familia yake nayo irudishe mahari waliyotoa; na kwamba mwanamume huyo hataki kuendelea na ndoa yao.

Benjamin Mong’awi (50), baba mzazi wa binti huyo, anadai kuwa baada ya kurudi kutoka safarini, alikwenda polisi kufuatilia shauri hilo.

“Nilipofika, askari wakaniambia nitoe pesa kwa ajili ya mafuta na posho yao ili wakawakamate watuhumiwa. Wakamatwe hao wawili.

“Wote wakasema kuwa wanamfahamu ngariba. Wakati hayo yanaendelea, ghafla na mimi nikakamatwa na polisi, wakidai kuwa watuhumiwa wamenitaja kuwa walinishirikisha mchakato mzima wa kumkeketa binti yangu, na kwamba nilikubali. Nikawekwa ndani siku nzima,” anasema Mong’awi.

Anashangaa polisi kumkamata akihoji kama angekuwa ameshirikishwa, ni kwa nini alitoa fedha ili kuwawezesha polisi kuwakamata watuhumiwa?

“Nina watoto tisa wa kike, hakuna niliyemkeketa. Kama ingekuwa kumkeketa inakuwaje nisubiri hadi aolewe kisha nishiriki ukatili huo? Hapa kuna mchezo mchafu unaofanywa na chombo chenye dhamana ya kutenda haki,” anasema.

Mzee huyo anashangaa jalada la shauri hili kukaa polisi kwa zaidi ya miezi miwili bila kulipeleka mahakamani.

Anasema pamoja na vitisho kuwa angeunganishwa kwenye mashitaka, alikubali na kusisitiza kesi iende mahakamani na huko ukweli utajulikana.

“Baada ya kuona hatubadili msimamo, wakanitaka kuripoti polisi kila siku. Hiyo ni gharama kwa kuwa kwenda na kurudi Mugumu ninatumia zaidi ya Sh 10,000 bila kula.

“Lengo lao ni kunikomoa hadi nikubali mipango yao. Polisi ninakwenda mimi, watuhumiwa siwaoni hata siku moja,” anasema akilitupia lawama Dawati la Jinsia Kituo cha Polisi Mugumu.

Mtuhumiwa anena

Akizungumza na JAMHURI, Maina anasema hakubaliani na taarifa ya hospitali kwamba mkewe alipata maambukizi ya fangasi kutokana na kukeketwa.

“Nadhani taarifa yao haikuwa sahihi, maana huyo mimi ninamfahamu. Alikeketwa zamani huko huko kwao, ila baada ya kuoana nikabaini kuwa anasumbuliwa na fangasi,” amesema.

Amesema alibaini hilo siku ya pili baada ya ndoa na kwamba mkewe huyo alimwambia kuwa alianza kuugua fangasi tangu akiwa darasa la saba.

“Kwa taaluma mimi ni mfamasia. Nilianza kumtibu bila mafanikio. Agosti 16, 2024 nikaamua kuimrudisha kwao akatibiwe, akipona arudi.

“Kufika huko, baba yake akamkataa na kudai kuwa mimi nimemkeketa na kumsababishia ugonjwa,” amesema.

Alipoulizwa kama mtaalamu wa afya alikuwa akimtibu tatizo gani hasa na ni wapi alikompeleka na kupata vipimo, amekiri kuwa hakupata vipimo.

“Mimi nina duka la dawa, kwa hiyo nikawa ninampatia ‘antibiotics’ basi,” amesema.

Maswali mengine aliyoulizwa na JAMHURI ni iwapo mkewe alikeketwa zamani, kwa nini yeye na mama yake waliwaeleza polisi kuwa baba wa binti huyo ameshiriki katika kitendo cha ukeketaji wa Agosti mwaka huu?

Kwa nini alikubali kulipa fidia ya Sh milioni 2.5 wakati hakuhusika? Je, yeye kama mtaalamu wa afya, anakataaje taarifa ya daktari aliyempima wakati yeye alimpa dawa bila kumpima? Na je, anafahamu madhara ya kutumia dawa bila kujua tatizo?

Maina, akionekana kubabaika, anasema: “Ni kweli nilimtaja mzee kuhusika kumkeketa mke wangu. Hilo la fidia, kwa kuwa wanajua nilipata fedha nyingi wakati wa zawadi (za harusi), nilikubali ili yaishe, kisha nirudishiwe mahari yangu nitafute mke mwingine. Suala la vipimo mimi sikumpima, lakini sina hakika kama daktari amesema ukweli.”

Mmoja wa wadau wa haki za binadamu (jina tunalihifadhi), amesema:

“Dhana ya kuwapo kwa dawati la jinsia ilikuwa ni kusaidia kudhibiti vitendo vya ukatili, lakini hali ilivyo sasa mwenye fedha akitenda kosa, anapewa haki.

“Hivi kweli polisi ni sehemu ya kujadiliana watu kulipana kwa kesi ya jinai? Hili linapaswa kuangaliwa kwa jicho makini.”

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Menrand Sindano, alipoulizwa kuhusu suala hili, kwanza alidai kuwa hana taarifa.

Siku mbili baadaye akasema suala hilo linashughulikiwa na dawati la jinsia.

Wataalamu wanasemaje?

Mmoja wa wataalamu wa masuala ya afya wilayani Bunda anasema ukeketaji unaweza kusababisha ugonjwa wa fangasi kutokana na mikato isiyo mizuri na matumizi ya vifaa vichafu.

Mmoja wa wauguzi wakongwe wilayani Serengeti amesema miongoni mwa athari za fangasi ni maumivu na kuwashwa eneo ambalo mtu amefanyiwa ukeketaji.

“Fangasi huathiri mfumo wa uzazi, kwa wajawazito inaweza kuathiri afya ya mtoto,” amesema.

Anasema waathirika wa ukeketaji huathirika pia kisaikolojia, hasa wanapofika kwenye vituo vya polisi na kukosa msaada.