Mzalendo aliyesalitiwa na jumuiya ya kimataifa
Tanzia kuhusu kifo cha mwanamapinduzi nguli wa Afrika, mpigania uhuru wa Zimbabwe na mwana wa Afrika, Robert Gabriel Mugabe, zilianza kusambaa Ijumaa ya Septemba 6, 2019. Salamu za rambirambi zilianza kumiminika kutoka kila kona ya dunia muda mfupi baadaye.
Kwa upande wa Tanzania, ambako Mugabe alipachukulia kama nyumbani kwake, Rais Dk. John Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) alikuwa miongoni mwa viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali kutuma salamu za pole kwa wananchi wa Zimbabwe na kwa Wana SADC kwa ujumla.
Aidha, kwa kutumia mamlaka aliyonayo kisheria, Rais Magufuli alitangaza siku tatu za maombolezo kumuenzi jemedari Robert Mugabe.
Baada ya mzee Mugabe kufariki dunia, vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya Afrika vilianza kuchapisha makala kuhusu mapito ya jabali hilo la Afrika. Nilishawishika kusoma na kutazama makala hizo, lakini kama nilivyotarajia, waandishi wa makala hizo ama walikuwa na uelewa mdogo kuhusu mapito ya Mugabe, ama walikuwa wanajaribu kupotosha kwa makusudi, ama vyote viwili.
Sitaki kusema kwamba ninamfahamu sama mzee Mugabe kuliko watu wote duniani, wala sipendi ieleweke kwamba ninamchukulia Mugabe kama malaika, la hasha! Bali ninadhani pale ambapo historia inakaribia kupindishwa au inapopindishwa kwa kukusudia au kutokusudia, ni vema kuweka kumbukumbu vizuri, na ninaamini hili ni jukumu la kila kijana wa Kiafrika.
Wajuzi wa mambo wanao msemo wao kwamba, usipoandika historia yako, wengine watakuandikia, hivi ndivyo baadhi ya makala kumhusu Mugabe zilivyoandikwa (kujaribu kufuta au kupindisha historia) na mimi ninawiwa kuandika japo kidogo ninachokifahamu kuhusu chimbuko la vita kubwa dhidi ya utu na haiba ya Mugabe.
Ukisoma makala mbalimbali kuhusu mapito ya Mugabe, jambo moja kubwa ambalo kwa maoni yangu ninadhani kuna jitihada za kupotosha ukweli wake ni kuhusu sakata la ardhi. Wengi miongoni mwa wachambuzi na waandishi wa vyombo vya habari vya kimataifa, wanajitahidi sana kuonyesha kwamba Mugabe anafaa kulaumiwa kwa madhila yaliyoifika Zimbabwe kutokana na namna alivyoshughulikia suala la mgawanyo wa ardhi.
Nionavyo mimi, wachambuzi na waandishi hao hawajielekezi kwenye chimbuko la suala zima la mgawanyo wa ardhi. Chimbuko la suala la ardhi ni usaliti uliofanywa na mshiriki muhimu sana kwenye mazungumzo ya uhuru wa Zimbabwe yaliyofanyika kwenye jengo la Lancaster mjini London, Uingereza kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba mwaka 1979.
Mazungumzo hayo yalijumuisha pande kuu tatu; upande wa Serikali ya Uingereza, upande wa wapigania uhuru (ukiongozwa na Joshua Nkomo pamoja na Robert Mugabe) na upande mwingine ukiwa ni upande wa serikali iliyojitangazia uhuru kupitia kwa kibaraka wao, Askofu Muzorewa.
Kwenye mazungumzo hayo ya Lancaster ambayo mwenyekiti wake alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza wa wakati huo, Lord Carrington, yalijadiliwa masuala mengi ambayo baada ya kukubalika yalijumuishwa kwenye Katiba ya Zimbabwe huru. Itakumbukwa kwamba moja kati ya masuala tisa ambayo ujumbe wa upande wa wapigania uhuru (Nkomo na Mugabe) walilisimamia kidete ni suala la ardhi kwa wazawa.
Simulizi zinasema kwamba, suala la ardhi wakati wa majadiliano ya Lancaster nusura livunje mazungumzo ya kuipatia Uhuru Zimbabwe kama isingekuwa jitihada za makusudi za baadhi ya viongozi wa nchi zilizo msitari wa mbele kushauri ujumbe wa kina Nkomo na Mugabe kuridhia upatikane uhuru kwanza, kisha suala la ardhi lizungumzwe baada ya uhuru kupatikana.
Mkwamo wa upatikanaji wa uhuru ulitokana na msimamo thabiti wa wapigania uhuru kwamba, uhuru usingekuwa uhuru bila wananchi wazawa kumiliki ardhi yao ya asili.
Suala la ardhi pia lilipata sura mpya na yenye matumaini baada ya Serikali za Uingereza na Marekani kuahidi kufadhili fidia kwa walowezi katika utaratibu makubaliano huru baina ya muuzaji na mnunuzi (willing buyer, willing seller) baada ya miaka 10 ya uhuru wa Zimbabwe.
Hata hivyo, miaka 10 baada ya uhuru wa Zimbabwe (1995) ambapo muda wa utekelezaji wa ahadi ya Uingereza na Marekani ulikuwa umewadia, serikali za nchi hizo zilianza kuonyesha dhahiri kutokuwa tayari kutimiza ahadi yao hiyo ya kihistoria.
Mwaka 1997 Serikali ya Uingereza kupitia kwa Waziri wake aliyekuwa anashughulikia Maendeleo ya Kimataifa, Bibi Clair Short, ilinukuliwa ikijitenga na ahadi hiyo iliyotolewa na Serikali halali ya Uingereza chini ya Chama cha Conservative.
Alifanya hivyo kwa maelezo mepesi kwamba Serikali mpya ya Chama cha Labour chini ya Waziri Mkuu Tony Blair haikuwa na wajibu wowote wa kugharamia fidia kwa walowezi kwa kuwa haikuwa na nasaba yoyote na masuala ya ukoloni (We do not accept that Britain has a special responsibility to meet the cost of land purchase in Zimbabwe; we are the new government from diverse backgrounds without links to former colonial interests).
Kauli hiyo kutoka kwenye Serikali ya Taifa kubwa kama Uingereza si tu ilidhihirisha uchanga wa Serikali ya Tony Blair wakati ule, bali pia iliongeza chumvi kwenye kidonda cha uvumilivu mkubwa wa wananchi wengi wa Zimbabwe, ambao kupitia serikali yao walikuwa na ahadi ya kupatiwa mashamba katika utaratibu ambao ungewekwa baada ya Uingereza kutoa fedha kwa ajili ya fidia.
Ni wazi kwamba kauli ya Serikali ya Blair ilikuwa ni tangazo la vita na ilikuwa ni kauli iliyohitimisha uvumilivu wa Mugabe na Wazimbabwe kuhusu suala la ardhi. Itakumbukwa kwamba wakati Uingereza inakabidhi uhuru wa Zimbabwe, asilimia 73.8 ya ardhi yote yenye rutuba ilikuwa inamilikiwa na walowezi wachache.
Kufuatia msimamo huo rasmi wa Serikali ya Uingereza, na kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wananchi wenye uhitaji mkubwa wa ardhi, na kwa kuzingatia kwamba Serikali ya Mugabe haikuwa na fedha za kutosha kuweza kuwalipa walowezi wote baada ya ahadi ya Uingereza na Marekani kuyeyuka, Serikali ya Mugabe alibaki na njia moja tu, nayo ni kutwaa ardhi kutoka kwa walowezi bila kulipa fidia, huu ndio ulikuwa msimamo wa wapigania uhuru tangu wakati wa mazungumzo ya uhuru.
Uamuzi huo wa Serikali ya Zimbabwe kupitia kwa mzee Mugabe kwa vyovyote vile ulitokana na hasira ya kusalitiwa, kudharauliwa na kubagazwa na serikali ambayo ilitakiwa kushirikiana naye kumaliza tatizo hilo kubwa lenye sura ya kimataifa.
Itakumbukwa kwamba idadi kubwa ya walowezi wa Zimbabwe walikuwa na asili ya Uingereza, hivyo Uingereza ilikuwa na nafasi kubwa ya kuonyesha uongozi katika jambo linalogusa masilahi ya wananchi wenye asili ya Uingereza.
Ni dhahiri kwamba uamuzi wa kugawa ardhi kwa wazawa haukuratibiwa vizuri, hivyo kukawa na madhara makubwa kwa walowezi, mali zao na kwa uchumi wa taifa.
Inasikitisha kwamba Serikali ya Uingereza na jumuiya ya kimataifa vilizinduka usingizini baada ya uamuzi wa hasira wa Serikali ya Mugabe baada ya kukerwa na kutowajibika kwa Uingereza kwenye suala ambalo ilitakiwa kudhihirisha uongozi na ukomavu.
Badala yake, Uingereza na jumuiya ya kimataifa wakaelekeza lawama zote kwa Mugabe, na kampeni kubwa ikafanyika kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kumchafua mzee Mugabe na kuuaminisha umma wa Wazimbabwe, Waafrika na dunia kwa ujumla kwamba Mugabe alikuwa ni mkosaji na alikuwa ni dikteta aliyestahili kuondolewa madarakani kwa namna yoyote ile kupitia kampeni za regime change kama ilivyofanyika Iraq, Afghanistan na kwingineko.
Ukisoma kwa makini makala kuhusu maisha ya Mugabe kutoka kwenye vyombo vya kimataifa, utabaini kwamba uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kuichafua taswira ya Mugabe ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa, ni watu wachache wanapata ujasiri wa kudadisi, kusaili na kuonyesha kisiki ambacho Mugabe alijikwaa kwacho, badala yake wanatumia nguvu kubwa kuonyesha alipoangukia.
Binafsi nadhani huu ni upotoshaji wa historia na hatuisaidii hii dunia. Tunao wajibu wa kubainisha ukweli wote ili badala ya kurithishana maadui, kila mtu achague adui wake kwa vigezo vyake, endapo itakuwa ni lazima sana kutengeneza maadui.
Mugabe tayari ametunukiwa hadhi ya shujaa wa Taifa na atapumzishwa kwenye makaburi ya mashujaa wengine wa Zimbabwe (Heroes acre) nje kidogo ya Jiji la Harare ambapo pia mkewe wa kwanza, raia wa nchi ya Ghana, Sally Hayfron, pia alipumzishwa.
Ni imani yangu kwamba akiwa mapumzikoni atapata muda wa kuonana na mwanaye wa kwanza, Nhamo Mugabe aliyefariki dunia nchini Ghana mwaka 1966 akiwa na umri wa miaka mitatu tu, na Mugabe akiwa gerezani akanyimwa ruhusa ya kumzika mwanaye kipenzi.
Robert Gabriel Mugabe alizaliwa mwaka 1924 katika eneo la Kutama, kilometa 100 nje ya Jiji la Harare. Kitaaluma ni mwalimu na aliwahi kufundisha nchini Ghana, ambako alikutana na mkewe wa kwanza, Mayi Sally, kama alivyokuwa akifahamika.
Mwaka 1960 Mugabe alijiunga na Chama cha National Democratic Party (NDP) kilichokuwa chini ya Joshua Nkomo, na akateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho. Mwaka 1961, Mugabe alifunga ndoa takatifu na Sally Hayfron. Mwaka 1964 Mugabe alikamatwa na kuwekwa kizuizini. Mwaka 1966 kijana wa kwanza wa Mugabe alifariki dunia.
Mwaka 1974, Mugabe aliachiwa huru kutoka kizuizini na mwaka mmoja baadaye akakimbilia nchini Msumbiji kujiunga na wapigania uhuru wa msituni. Mwaka 1979 Mugabe alishiriki kwenye mazungumzo ya kuipatia uhuru Zimbabwe. Mwaka 1980, Mugabe akachaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Zimbabwe.
Buriani mwana mwema wa Afrika. Buriani Komredi Robert Gabriel Mugabe. Pamberi ne Afrika!