Mbunge aliyemshinda Mwalimu Nyerere

Paul James Casmir Ndobho alifariki dunia Jumapili, Septemba 8, 2019, saa mbili usiku katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza alikokuwa akitibiwa.

Kwa bahati mbaya sana, kifo chake hakikutangazwa na kupewa uzito unaostahili ambao ungeakisi mchango wake kwa taifa lake alilolipenda kwa moyo wake wote.

Ni kutokana na ukweli huu ndipo nilipoona umuhimu wa kushika kalamu na karatasi na kuandika ATIKALI inayomhusu.

Ndobho alikuwa mwanadiplomasia na mzalendo mwenye ujasiri usio na mfano. Alijitofautisha na viongozi wanaojikomba kwa wakubwa, viongozi wasiojiamini, viongozi waoga na viongozi wasiojua nini maana ya uongozi.

Daima alikuwa mkweli na kamwe hakumuogopa mtu yeyote wala hakuogopa kuongea kitu chochote na alisimamia na kutetea kwa nguvu zake zote jambo aliloliamini.

 

Kuzaliwa, elimu

Ndobho alizaliwa mwaka 1938, Efulifu, Musoma mkoani Mara, hivyo hadi mauti yanamkuta alikuwa na miaka 81. Alipata elimu yake seminari iliyoko Nyegezi, Mwanza na kisha kujikita kwenye vyama vya ushirika kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa.

 

Ubunge

Oktoba mwaka 1965, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa inafanya Uchaguzi Mkuu katika mfumo wa chama kimoja cha Tanganyika African National Union (TANU), Ndobho akiwa mwanachama wa TANU, alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge Jimbo la Musoma Kaskazini. Akiwa kijana mdogo tu wa miaka 27 mwaka huo, alikonga nyoyo za wapiga kura na kuibuka mshindi, hivyo kutangazwa kuwa Mbunge wa Musoma Kaskazini.

Mwalimu Nyerere asalimu amri kwa Ndobho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza mafao (gratuities) kwa mawaziri, mawaziri wadogo, wakuu wa mikoa na wilaya nchi nzima. Mzee Rashid Mfaume Kawawa, aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwasilisha muswada husika kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale Karimjee Hall, jijini Dar es Salaam.

Ndobho hakukubaliana na Mwalimu, kwani hakuona mantiki ya viongozi hao kupewa kitita hicho ilhali taifa letu ni maskini, ambapo umaskini ulikuwa umetamalaki mijini hadi vijijini.

Hivyo, Julai 1968, Ndobho aliwasilisha hoja binafsi (Private motion) bungeni kupinga muswada huo wa mafao.

Wabunge wenzake walipigwa butwaa kwa ujasiri wake na kukawa na minong’ono mingi na sintofahamu bungeni humo, kwani halikuwa jambo la kawaida kwa kiongozi au raia wa kawaida  kumpinga Mwalimu.

Ndobho alijenga hoja kwa weledi wa hali ya juu sana na kusababisha aungwe mkono na wabunge wote kasoro mbunge mmoja tu.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Chifu Adam Sapi Mkwawa, alipotangaza matokeo hayo, Bunge lote lilirindima kwa shangwe, bashasha, nderemo na hoihoi kubwa!

Baadaye, Mwalimu alizipokea na kuzikubali criticisms za wabunge hao kuhusu muswada huo. Julai 29, 1968, Gazeti la Serikali la wakati huo – The Nationalist – liliipa habari hiyo kichwa kisemacho  ‘A People’s Victory!’ Hii ilimaanisha – Ushindi wa Wananchi – ingawa kiuhalisia ulikuwa ni ushindi wa Ndobho.  Kwa hakika, hili lilimjengea heshima kubwa sana Ndobho.

Ateuliwa Katibu wa TANU Kigoma

Februari, 1970, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Nyerere, alimteua Ndobho, aliyekuwa na michango iliyosheheni ‘madini’ bungeni,  kuwa Katibu wa TANU Mkoa wa Kigoma. Wadhifa huo, kwa utaratibu wa enzi hizo, ulimfanya pia kuwa mkuu wa mkoa na mbunge.

Ndobho aliwatumikia wananchi wa Mkoa wa Kigoma hadi Novemba, 1975.

Ateuliwa Balozi Urusi

Machi 2, 1976, Rais Nyerere alimteua Ndobho kuwa Balozi wa Tanzania nchini Urusi kwenda kuchukua nafasi ya Balozi Cecil Kalaghe aliyerudishwa nyumbani. Hivyo, mara moja Balozi Ndobho akaondoka nchini na kwenda kuanza kuhudumu kama mwanadiplomasia huko Urusi.

Ndobho ajiunga NCCR-Mageuzi

Baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini  ya Rais Ali Hassan Mwinyi kurejesha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992 kupitia Sheria ya Vyama Vingi, 1992, Balozi Ndobho, aliyekuwa haridhishwi na jinsi mambo yalivyokuwa yakienda ndani ya Chama chake cha CCM, aliamua kujiunga na chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi.

Itakumbukwa kuwa katika miaka hii ya mwanzoni na katikati ya 1990 ndipo aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba, aliposema “CCM Imekosa Dira.”

Aidha, siku tulivu ya Jumatatu ya Mei Mosi, 1995, Mwalimu Nyerere aliyekuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Mei Mosi zilizokuwa zikirindima kitaifa katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, naye alitoa kauli kali kuhusu chama hicho kuwa: “CCM sasa imekuwa ni sawa na dodoki ambalo hubeba vitu visafi na vichafu.”

 

Mwalimu Nyerere amtosa Mwana CCM, amkampenia Balozi Ndobho

Mwaka 1995, katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi vya siasa nchini, Balozi Ndobho alijitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Musoma Vijijini kupitia tiketi ya NCCR-Mageuzi.

Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye kijiji atokacho cha Butiama kilikuwa ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini, katika tukio ambalo lilikuwa la kushangaza na ambalo halijawahi kutokea tena nchini hadi leo, aliamua kumfanyia kampeni Balozi Ndobho badala ya mgombea wa CCM,  Timothy Munena.

Mwalimu Nyerere aliinyanyua juu picha kubwa ya Benjamin William Mkapa na kuwaomba mamia ya wananchi waliofurika katika mkutano kumchagua awe rais wa nchi yetu. Huku wananchi  wakitarajia Mwalimu amfanyie kampeni mgombea wa CCM, Mwalimu Nyerere, bila kutikisa pua wala kupepesa macho, akawaambia wananchi hao wamchague Balozi Ndobho kwani ni kiongozi mzuri na mwadilifu.

Uchaguzi ulipofanyika Oktoba 25, 1995, Balozi Ndobho akaibuka na ushindi wa kishindo na kutangazwa kuwa mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini akimtimulia vumbi mgombea wa CCM.

 

Balozi Ndobho arejea CCM

Balozi Ndobho alihudumu bungeni kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi kwa muhula mmoja tu kwani mwaka 2000 hakugombea baada ya kutoona mwelekeo alioutarajia kutoka upinzani.

Kutogombea kwake kulimfanya mgombea wa CCM, Mwanasheria nguli Nimrod Elirehema Mkono, kuwa mgombea pekee, kwani hakuna mgombea kutoka chama kingine aliyejitokeza kumpinga, hivyo akapita bila kupingwa.

Nukuu kuntu 3 za Balozi Ndobho

Katika maisha yake kama mwana TANU, mwana CCM, mwana NCCR na mwanadiplomasia, Ndobho amefanya mambo mengi sana. Kwa ambao walikuwa hawamfahamu, nimeamua kuchagua nukuu zake tatu tu ili wapate picha ya kujua Ndobho alikuwa ni mtu wa aina gani:

“Mimi ni mwana CCM halisi na siogopi kusema ukweli. Namtaka Rais wetu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kuwaondoa viongozi wote mizigo akianzia na Katibu Mkuu wetu, Yusuph Makamba. Hivi Makamba anafanya kazi gani ndani ya chama? Hata baadhi ya wajumbe wa NEC hawastahili hata kidogo kuendelea kuwa ndani ya chama kwani wamepata vyeo hivyo kwa njia ya rushwa.”

Machi 7, 2011.

“Namuonya Msajili wa Vyama, Bwana John Tendwa, kwa kauli yake ya kutishia kuifuta CHADEMA. Aifute CHADEMA kwa kipi? Akichukua hatua hiyo anaweza kuifanya nchi isitawalike.”

Machi 7, 2011.

“Viongozi wa vyama cha upinzani acheni utamaduni wenu wa kupenda kuilaumu tu serikali ya CCM. Mpinzani wa kweli ni yule anayeikosoa serikali iliyoko madarakani kwa kujenga hoja na kisha kueleza njia mbadala ya nini kifanyike ili taifa letu lisonge mbele. Kama mpinzani huna njia mbadala, basi funga mdomo wako.”

Septemba 12, 2014.

Buriani Mwanadiplomasia na Mzalendo wa ukweli, Balozi Paul James Casmir Ndobho.

 

Tafakuri tunduizi

Je, kitendo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyepewa Kadi Na. 1 ya TANU mchana wa siku ya Jumatano, Julai 7, 1954 na Kadi Na. 1 ya CCM asubuhi tulivu ya Jumamosi, Februari 5, 1977, kumfanyia kampeni hadi kumfanya mgombea wa upinzani (Balozi Ndobho) kuibuka na ushindi wa kishindo, kinatupa funzo gani Watanzania?

Je, kitendo hicho alichokifanya Baba wa Taifa mwaka 1995 hakiakisi anachokisema mara kwa mara Rais Dk. John Joseph Pombe Magufuli kuwa “Maendeleo hayana chama?” Tafakari.