Mwaka ni kipindi cha miezi kumi na miwili, kuanzia Januari hadi Desemba, kulingana na kalenda ya Kirumi, na mfunguo nne (muharami) hadi mfunguo tatu kulingana na kalenda ya Kiarabu. Watanzania wanazitumia kalenda hizi zote mbili.

Ni kipindi cha siku 364 kwa mwaka mfupi na 365 kwa mwaka mrefu. Katika kipindi chote hicho Watanzania tunafanya mambo mengi mbalimbali yakiwemo ya kufanya kazi, kutunza amani yetu, kupendana na kumcha Mungu.

Leo ni Desemba 31, tunakamilisha kalenda ya Kirumi na kesho penye majaliwa yake Mwenyezi Mungu tutaanza mwaka mpya. Buriani mwaka 2019 na karibu mwaka 2020. Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kutuwezesha kuona yote haya. Amin.

Katika miezi kumi na miwili iliyopita, yako mambo mengi yametokea kuanzia katika familia zetu hadi taifa. Mabaya na machungu, mazuri na matamu. Hatuna budi kupeana pole na pongezi kwa yaliyotufika.

Leo tumiminike katika nyumba za ibada kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kumaliza mwaka salama salimini. Na tumuombe Mungu aturuzuku heri, baraka na fanaka kuishi katika miezi kumi na miwili ijayo kwa amani.

Wakati tunaupa buriani mwaka 2019, kuna mambo ya kuyaangalia na kuyapima kwa kiasi gani tumefanikiwa au la. Vilevile tunapoingia katika mwaka 2020, tujiulize tunadhamiria kufanya nini kwa masilahi ya familia zetu na taifa letu.

Ni kweli mambo yako mengi kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini hatuna budi. Lililo kubwa katika haya ni amani. Amani ndiyo ngome na ngao. Hatuwezi kufanikisha shughuli yoyote iwapo hatuna amani katika taifa letu. Kwa hiyo tuupambe mwaka 2020 kwa upendo na amani.

Wataalamu wetu wa siasa, uchumi na ustawi wa jamii tupatieni takwimu zenye tathmini za mafanikio au hasara tuliyopata mwaka 2019, na ushauri tufanye nini mapya ambayo kwayo yatatuwezesha kupata mafanikio bora zaidi katika mwaka 2020.

Maendeleo yetu katika huduma za jamii, yaani maji, afya na elimu na katika uchumi kwa maana ya miundombinu ya usafiri, viwanda, kilimo na biashara yakoje?

Na utumishi wetu kwa umma katika haki, uaminifu na uadilifu tumeshiriki kwa kiwango gani?

Mizania inasomaje katika maendeleo ya watu na vitu, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na dhuluma? Utetezi wa haki na utoaji wa masilahi kwa wananchi nao ukoje? Vipi kuhusu uhuru wa kutoa na kupokea habari kwa mujibu wa sheria,  na wajibu wa kulinda na kuhifadhi mali na rasilimali zetu?

Mambo haya na mengineyo yanahitaji tafakuri ya kina na makini, ili mwakani tujue tunaanzia wapi. Si viongozi wa siasa na serikali tu wanaopaswa kuwa na majadiliano ya pamoja katika kudumisha haki na amani, bali hata wanachama na mashabiki wa siasa na wananchi tunahusika.

Mwaka 2019 tumeshuhudia malumbano na vijembe vya kisissa, vilio vya kutaka kupata kazi na masilahi mazuri na mienendo ya baadhi ya viongozi wetu kutowaridhisha wananchi. Lakini kubwa ni kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini kwa utulivu na amani.

Mwakani 2020, tudhamirie kufanya mambo mazuri kwa faida yetu. Tusiruhusu joto la kisiasa kupanda na kututia jakamoyo na tusielewane. Taratibu za kisiasa, kikatiba na kidemokrasia tulizojiwekea ziheshimiwe na zitekelezwe.

Jambo kubwa linalotia anga ya Tanzania joto la matumaini ni Uchaguzi Mkuu wa Taifa. Uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya, rais, wabunge na madiwani kwa miaka mitano ijayo. Tunahitaji amani. Karibu mwaka mpya, 2020.