Namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia na kuniwezesha kuuona na kuukaribisha mwaka mpya 2019 na kunipa uwezo kutamka buriani mwaka 2018. Mwaka ambao kwangu na kwa nchi yetu Tanzania ulikuwa ni mwaka wa mafanikio.

Nina wajibu tena na tena kutoa shukrani kwa Mola wangu kunijalia pumzi, afya njema na nguvu tele hata kushika kalamu na kutuma salamu za upendo na amani kwako na kukuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kukubariki katika shughuli zako za kijamii na kiuchumi katika mwaka huu.

Aidha, nina dhima kubwa ya kutoa buriani kwa ndugu zangu na Watanzania wenzangu ambao hawakujaliwa kuuvuka mwaka 2018 na kuuona mwaka 2019. Yote haya ni takdiri yake Mola.  Yaa Rabii wapokee viumbe wako hao na waweke mahala pema peponi. Amin!

Wakati namshukuru Mwenyezi Mungu, hekima inanichunga kuangalia baadhi ya matukio yaliyopata kutia moyo hofu au yaliyopata kutia moyo utulivu wa Mtanzania katika mwaka 2018. Ni hekima pia moyo huu kujaa matumaini yatakayojenga Tanzania huru na mpya.

Jambo moja kubwa ambalo Watanzania tumelifanya ndani ya uongozi na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwa na amani. Amani ambayo tumeijenga chini ya umoja na upendo bila kusita kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Mambo mengi tumefanikiwa, yakiwemo maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kama vile miradi ya miundombinu ya elimu na barabara. Tumejali tabia ya kujenga umoja na mshikamano. Tabia hii hatuna budi kuiendeleza.

Mambo mazuri tuliyohitaji kupata tumeanza kuyapata. Mathalani, kuondoa ufisadi na mafisadi, kuwabaini na kuwakataa viongozi uchwara, kujenga na kuboresha miundombinu ya sekta mbalimbali ikiwemo anga, bandari, nishati na kadhalika. Kurufisha moyo wa kufanya kazi na kuendelea kuwa na amani yetu.

Jambo jingine ambalo baadhi ya Watanzania wamepata kulifanya ndani ya uongozi na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwa na hofu. Iwe kwa kukusudia au kutokukusudia, wameshiriki kutia moyo hofu na watu kuishi kimashaka mashaka na kiwasiwasi.

Mwaka 2018 tulishuhudia watu wakitoa lawama na vilio vilivyotokana na watu kutekwa, kupotea hata kuuawa na watu wasiojulikana. Maelezo kuhusu demokrasia kuminywa yamerindima na kutia masikio moto hata kusukuma vyama sita vya siasa kuweka nia kwamba mwaka 2019 havitakubali kuona hali hiyo ikiendelea. Vitapambana na serikali kuona demokrasia haiminywi.

Matukio chanya yaliyotokea katika kipindi hicho hayana budi kuendelezwa kujenga taifa ndani ya mwaka huu. Yale hasi hayana budi nayo kuachwa, kwani yanavunja umoja na mshikamano na yanaminya maendeleo ya taifa. Yanajenga ugomvi na uadui. Hii si Tanzania ya uadui, ni Tanzania ya amani.

Ombi langu kwa Watanzania, tuuweke mwaka huu kuwa wa amani. Tunapokaa na kuunda makundi yetu ya mazungumzo, michezo, kazi au siasa tukumbuke tunafanya tendo la kuungana. Hatufanyi tendo la kutengana.

Nasema haya baada ya kuona watu wanaoungana kufanya mazungumzo au siasa katika jambo la ukombozi au maendeleo si wamoja katika kauli zao, misimamo yao, na hata katika makusudio yao. Ukweli wanajivisha vilemba vya ukoka na kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa.

Madhali tumekiri kwa kauli yetu kutoa mkono wa buriani kwa mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019 kwa furaha na amani, tuupe mwaka huu kauli za ukweli, amani na uthubutu kwa kuungana, si kwa kutengana.

“Tuendelee kuwa na mshikamano, tuendelee kuwa na amani, tuendelee kuwa na umoja, tuendelee kama kawaida baina yetu sisi Watanzania, na tuendelee kufanya kazi.” Ni kauli ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli katika kuuaga mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019.