*Wabunge wacharuka chama kufanya mabadiliko, uamuzi mzito bila kuwashirikisha
*Wawaambia ‘wakubwa’ Makao Makuu: Kama hamtutaki au mmetuchoka mtueleze tujue moja
*Spika, ‘Chief Whip’ wakumbwa na hofu kuwapo uwezekano wa bajeti kadhaa kukwama
*Rais Samia aingilia kati, azungumza na Dk. Nchimbi kwa simu kupoza munkari, mambo yawekwa sawa
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Mkutano wa 19 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepita katika kipindi kigumu wiki moja tu tangu ulipoanza; JAMHURI linaripoti.
Kikao cha Kwanza cha mkutano wa huo Bunge la Bajeti linalotazamiwa kuendelea hadi mwishoni mwa Juni mwaka huu, kilifanyika Jumanne ya Aprili 8, 2025.
Bunge la 12 chini ya Spika Dk. Tulia Ackson linaundwa na idadi kubwa ya wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hao ndio waliokaribia kuzua tafrani wakati wa kikao chao, kinachofahamika kwa jina la ‘party caucus’.
Kikao hicho kilifanyika Jumanne wiki iliyopita Makao Makuu ya CCM (White House), ikiwa ni wiki moja tu tangu kuanza kwa Mkutano wa 13 wa Bunge, kikiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Yaliyojiri ndani ya ‘caucus’
“Hasira za wabunge zilijionyesha waziwazi! Wabunge walikuwa wakali wakihoji ni kwa sababu gani makao makuu wanafanya uamuzi unaowahusu (unaohusu nafasi zao za ubunge) bila kuwashirikisha,” anasema mtoa taarifa wetu (jina linahifadhiwa).
Taarifa zinasema wabunge wengi walikuwa wakipinga utaratibu wa chama (CCM) kutangaza tarehe na ratiba ya kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwa ajili ya Uchaguzii Mkuu kuwa ni Mei 2, 2025.
Tarehe hiyo ambayo maana yake ndio ingekuwa mwanzo wa kampeni, hata kama si rasmi, za wenye nia ya kuwania ubunge, udiwani na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, ingewakuta wao (wabunge) wakiwa katikati ya Bunge la Bajeti.
“Kutangazwa kwa tarehe hiyo kuliondoa utulivu bungeni. Unadhani Mbunge angewezaje kushiriki na kuchangia hoja mbalimbali wakati jimboni kwake watu wanapita wakizengea nafasi yake?
“Hilo halikuonekana kuwa sawa na ndio maana wabunge walilalamika mbele ya Balozi Nchimbi wakiamini kuwa hawajatendewa haki,” anasema mtoa taarifa wetu.

Habari za uhakika zilizolifikia JAMHURI zinadai kuwa siku hiyo Balozi Dk. Nchimbi alibanwa kwa maswali nahoja nzito kutoka kwa wabunge kadhaa (majina tunayo); mmoja amekaririwa akisema na kuhoji:
“Lakini ni kwa nini (maofisa wa makao makuu/sekritarieti ya chama) mmetufanyia mambo haya? Mmebadilisha ghafla tarehe ya kuchukua fomu, mmeamua kutangaza ratiba wakati Bunge linaendelea na vikao vyake jambo ambalo miaka yote halikuwepo.
“Hamuona kuwa mmeleta mtafauku mkubwa? Hivi sisi wabunge wenu tumekosa nini? Inaonekana kuwa hamtutakii mema kabisa, sasa ni bora mtuambie tujue, labda wabunge tuliopo sasa hamtutaki, maana majimboni kwetu watu wanajipitsha wakati sisi tupo Dodoma.”
Vigogo wa Bunge nao wahoji
Mbali na hoja hizo za wabunge wenye nia ya kutetea nafasi zao kwa mara nyingine, hoja nyingine nzito iliyotolewa ni kwamba wabunge wengi wanakosa muda wa kushiriki vikao bungeni wakati bajeti za Serikali zikipitishwa.
“Wa kwanza kucharuka na hoja hii nzito alikuwa Lukuvi (Mbunge wa Ismani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvu) ambaye ndiye Chief Whip (Mnadhimu) wa Bunge.
“Akamwambia Katibu Mkuu kuwa kila siku wabunge karibu wote wanaaga, wanakwenda majimboni kwao. Akahoji; ‘sasa ni nani atakayepitisha bajeti za wizara za serikali zinazofuata? Kuna siku ‘quorum’ itashindwa kutimia.’ Hoja yake iliungwa mkono na wabunge wote waliohudhuria,” anasema mtoa taarifa wetu mwingine.
Kana kwamba ni kupigilia msumari na kuongeza msisitizo katika hoja ya Lukuvi, taarifa zinasema kwamba Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk. Tulia Akson, naye akainuka kuzungumza.
Dk. Tulia alilalamikia wakati mgumu unaokikumba ‘Kiti’ kipindi cha vikao kutokana na mahudhurio hafifu ya Bunge katika Mkutono wa 19 wa Bunge la Bajeti.
Anamkukuu Spika Dk. Tulia akisema: “Tunapata wakati mgumu kwa sababu hakuna wabunge wa kutosha ndani ya Bunge. Ninaona ‘maamuzi’ yanakuja bila kutushirikisha (wabunge). Sasa mimi nitawazuiaje? Hawakai bungeni!”
Mtoa taarifa wetu anaamini kuwa hoja ya Dk. Tulia ilikuwa na mashiko na kwamba alikuwa sahihi kwani kutajwa kwa tarehe ya hivi karibuni kulisababisha utulivu kukosekana.
“Wewe unaweza kutulia kweli wakati kitumbua chako kinawaka moto?” anahoji mtoa taarifa wetu.
Anamnukuu Dk. Tulia akisema: “Mnataka watia nia watangaze kugombea wakati sisi bado tuko kwenye madaraka! Hivi mnataka tufanyeje sasa?
“Mheshimiwa Katibu Mkuu, huu ni mtihani mkubwa. Jambo hili linaniweka katika wakati mgumu. Tuna kazi ya kujadili bajeti za wizara, lakini waheshimiwa wengi tunalazimika kukimbia majimboni mwetu.”
Moto wa wake, Dk. Samia aingilia kati
Taarifa zinasisitiza kwamba kikao hiho kilikuwa kigumu na cha moto kuliko ilivyotarajiwa na kwamba huenda Balozi Nchimbi naye pia hakutarajia kukumbana na hoja nzito kiasi kile.
Mbunge mwingine kutoka magharibi mwa Tanzania (jina tunalo) anadaiwa kuzungumza kwa hisia kali zaidi ya wengine wengi, akidai kuwa hata hatua ya kuongeza wigo wa washiriki wa kura za maoni ndani ya CCM haukuwahirikisha wabunge wanaoamini kuwa ndio wadau wakubwa.
Dk. Nchimbi, anayesifika kwa ustahimilivu na usikivu makini, baada ya kuwasikiliza wabunge na viongozi wao pamoja na hoja zao, taarifa zinasema alilazimika kuwaomba wabunge watulie apate nafasi ya kuteta (kwa simu) na Mwenyeniti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Balozi Nchimbi ni mgombea mwenza mteule wa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
JAMHURI limeelezwa kwamba ni mazungumzo kati ya Mwenyekiti wa CCM Rais wa Tanzania, Dk. Samia na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Nchimbi, yaliyodumu kwa dakika kadhaa ndio yaliyozaa uamuzi wa kusogeza mbele muda wa kuchukua fomu za ubunge na udiwani kutoka Mei 2 hadi Juni 28, 2025.

Hofu kutorudi bungeni
Mmoja wa wabunge wa zamani aliyezungumza na JAMHURI kuhusu yaliyojiri ndani ya ‘caucus’, anasema:
“Wabunge wengi wanaonyesha wasiwasi mkubwa wa kutorudi bungeni. Wanaona ni kama kuna mkakati wa makusudi wa kuwaengua.
“Lakini ukweli ile terehe ya awali ilikuwa kama mtego kwao. Uamuzi wa kusogeza mbele umefanyika kwa maslahi mapana ya chama na kila upande umezingatiwa.”
Anasema ndani ya Bunge wamo baadhi yao wanaohitajika kuendelea kuwapo lakini asilimia kubwa wanapaswa kuondoka na kupisha wengine.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba kwa wastani asilimia 60 ya wabunge hushindwa kurejea bungeni baada ya uchaguzi.