Matukio ya ufisadi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yameendelea kuibuliwa, na safari hii yanahusu malipo ya Sh bilioni 6 kwa kampuni ya bima ya Jubilee.
Malipo hayo kwa bima ya wabunge na familia zao yalianza kulipwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015. Kiwango hicho kiliafikiwa kutoka kile cha awali ambacho kilikuwa ni Sh bilioni 9 kwa mwaka.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwapo kwa maslahi binafsi yawanayopata baadhi ya viongozi waandamizi wa Bunge pamoja na ‘washenga’ waliofanikisha kutolewa kwa zabuni hiyo.
Imebainika kuwa kabla ya kuanza utaratibu wa bima kwa wabunge na familia zao, Bunge lilikuwa likitumia kiasi kisichozidi Sh bilioni 3 pekee kwa mwaka kugharimia matibabu kwa walengwa hao.
“Tulishangaa kuona tunaachana na malipo yasiyozidi Sh bilioni 3 kwa mwaka kwa matibabu ya waheshimiwa wabunge na familia zao na kwenda hadi Sh bilioni 9. Hizi Sh bilioni 6 zinazolipwa sasa ni baada ya wakubwa kuona kiwango cha bilioni 9 ni kikubwa mno kwa hiyo wakaomba Jubilee wakipunguze na wao wakakishusha hadi Sh bilioni 6,” kimesema chanzo chetu.
Mpango mzima wa kuifanya Jubilee kushinda zabuni hiyo ya Bunge ulisukwa na kufanikishwa na raia wa Kenya (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye anasifika kwa kujihusisha na masuala makubwa ya kifedha. Mkenya huyo yuko kwenye orodha ya watu wanaotuhumiwa kuhusika kwenye utakatishaji fedha kupitia Benki ya Stanbic.
Vifaa vya Mghahawa
Chanzo cha habari kimesema kumeibuka sintofahamu kwenye hatima ya vifaa vya mghahawa wa Dodoma vilivyonunuliwa na Bunge, lakini siku chache baadaye vikakabidhiwa mwendeshaji mghahawa huyo ambaye ni kampuni binafsi.
Taarifa zinaonesha kuwa Bunge lilitumia takribani Sh milioni 700 kununua vifaa hivyo.
“Vifaa vilikuwa vipya kabisa, vimenunuliwa na siku chache akakabidhiwa mwekezaji, hii ni kuonesha kuwa zilitumika fedha za Bunge kumwezesha mtu binafsi kuja kufanya kazi hapa. Hakuna hakika kama alitoa fedha kufidia gharama za ununuzi,” kimesema chanzo chetu.
Watoto wa vigogo
Chanzo chetu cha habari kinasema: “Syndicate aliyoitengeneza Katibu wa Bunge na inayomfanikishia mambo yake ni kuwaweka sawa Wajumbe wa Tume ya Huduma za Bunge (hasa waliopita), Manaibu Katibu wa Bunge, DAP, Wasaidizi wake ambao ni Mkurugenzi katika ofisi yake, Mkurugenzi ambaye ni Msaidizi wa Spika, Watendaji wakuu kadhaa wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na baadhi ya vigogo serikalini na katika idara nyeti,” kimesema chanzo chetu.
Ujenzi, ukarabati majengo
Yapo madai ya matumizi mabaya ya fedha kupitia ujenzi na ukarabati wa majengo ya ofisi.
“Kuanzia ujenzi wa Ofisi Ndogo ya Bunge Dar es Salaam na kumbi zake, ofisi za watendaji na kila kinachohusisha ujenzi au ukarabati wa Bunge ni majipu matupu! Ukaguzi ufanywe ili kubaini ukweli huu,” amesema mmoja wa watumishi wa Bunge.
Unatolewa mfano wa kampuni moja iliyosajiliwa kwa masuala ya kielektroniki, lakini imekuwa ikipewa kazi nyingi za ujenzi za Bunge.
“Kwa miaka yote kampuni hii inayoshughulikia masuala ya kompyuta imefanya kazi za ujenzi bila kuwa na leseni ya ujenzi; ni hivi karibuni ndio imeaanza taratibu za kupata leseni ya ujenzi,” kimesema chanzo chetu.
Pia kampuni hiyo inatajwa kwenye zabuni ya mitambo ya ulinzi na usalama katika Ofisi ya Bunge.
“Kampuni iliyohusika pia ni hiyo hiyo. Mtambo huo ulikuwa na hatua tatu, ambazo hadi kukamilika kwake zimetumika zaidi ya Sh bilioni 7. Uchunguzi ufanyike kuangalia taratibu na hasa thamani ya pesa kama kweli inalingana na kazi iliyofanywa,” amesema.
Muundo wa ofisi wakosolewa
Muundo mpya wa Ofisi ya Bunge nao umeanza kukosolewa, ukitajwa kuwa umelenga kutoa nafasi kwa nia ya kujinufaisha.
“Muundo ulikuwa ni wa muhimu ili kuwezesha taasisi kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Muundo mpya ulihitajika baada ya taasisi ya Bunge kukua na majukumu kuongezeka; lakini mchakato wa kuupata muundo huo ulitawaliwa na usiri na kutoshirikisha watumishi; jambo ambalo lilitoa mwanya kwa wahusika kufanya walivyotaka.
“Kwa kawaida majukumu ndio hutengeneza muundo wa ofisi, lakini kwa Ofisi ya Bunge watu ndio walitengeneza muundo. Kwamba, muundo uliangalia zaidi ‘huyu ni nani na ni nani kwetu’.
“Muundo mpya umewabeba zaidi watu wao na kutengeneza nafasi nyingi hasa za wakurugenzi, wakurugenzi wasaidizi na wakuu wa vitengo huku baadhi yao wakiwa hawana sifa za kutosha kwa nafasi hizo.
“Uteuzi wa Manaibu Katibu wa Bunge ni kama vile watu wamejitengenezea nafasi. Aliyekuwa anaratibu shughuli za kutengeneza muundo alijipa cheo cha Naibu Katibu wa Bunge Utawala.
“Muundo huo mpya ulitengeneza nafasi nyingi za wakurugenzi na wakurugenzi wasaidizi bila kuzingatia mahitaji halisi ya ofisi kulingana na majukumu; mchakato wake haukuwashirikisha watumishi, chama cha wafanyakazi au Baraza la Wafanyakazi, menejimenti ya ofisi wala ngazi yoyote ya uongozi zaidi ya watu wachache kujifungia na kuuandaa na kuwatumia baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ajira ya Tume ya Utumishi wa Bunge kuupitisha na kuuhalalisha.
“Watumishi waliitwa na kusomewa uamuzi Septemba Mosi, mwaka jana katika ukumbi wa Karimjee. Muundo huo ilipofika Novemba 16, mwaka jana ulibadilishwa tena kimya kimya bila taarifa rasmi kwa watumishi.
“Kwanini hilo liliwezekana? Hilo liliwezekana kwa kuwa Wajumbe wa Kamati ya Ajira ya Tume ya Utumishi wa Bunge, ambao waliunda Kamati Ndogo ya Ajira iliyokuwa na wajumbe watatu ilikuwa inajua inafanya nini kwa maslahi ya kina nani.
“Walikuwa wakilipwa fedha nyingi, safari nyingi za nje na marupurupu mengine nje hata ya stahili zao. Wajumbe wa Kamati ya Ajira ya Tume ya Utumishi wa Bunge la Kumi (2010 – 2015) walitumika kuidhinisha matumizi ya fedha za ofisi pamoja na miongozo mingine kama kupitisha muundo mpya, kupandisha watumishi vyeo n.k.
“Wajumbe hao wa Tume waliendelea kusafiri nje ya nchi kwa kigezo cha kuhudhuria mafunzo na kujifunza ilhali wote walikuwa si wabunge tena baada ya kushindwa kwenye kura za maoni ndani ya vyama vyao. “Waliendelea kulipwa fedha nyingi zisizo na maelezo ya kutosha hadi Februari, mwaka huu wakati hawakustahili.
“Muundo mpya wa ofisi baada ya kukataliwa ulirejeshwa tena kufanyiwa marekebisho na muundo uliorekebishwa ulitoka tena Novemba, mwaka jana,” kimesema chanzo chetu.
Kanusho la Bunge
Baada ya kuandikwa kwa habari zinazohusu matumizi mabaya ya fedha na madaraka, Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa ndefu iliyolenga kuonesha kuwa yaliyoandikwa na JAMHURI hayakuwa sahihi.
Taarifa hiyo iliibua maswali kadhaa. Mosi, kama taratibu za ajira zilifuatwa je, ni lini matangazo ya kazi yalitolewa na kwa vyombo vipi vya habari? Hata kama yalitoka kwenye tovuti, je, yalidumu kwa muda gani? Kanuni za Uendeshaji wa Shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma zinahitaji matangazo yafanyike kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwa siku zisizopungua 14. (Rejea Sehemu ya Nne Kifungu 9 Kifungu Kidogo cha 3. Kwa njia ya Posta. Je, waombaji walifanya hivyo? Waombaji walikuwa wangapi? Waliokuwa short listed ni wangapi? Na vigezo vipi vilifuatwa?
Je, wangapi walifanya usaili? na kwa tarehe zipi? Je, uongozi wa Bunge uko tayari kuwaita tena waliosailiwa ili waweze kuthibitisha ushiriki wao? Je, alama za usaili zinaweza kupatikana kuthibisha hayo ili kuonesha waliostahili ndiyo walioitwa kazini?
Pili, kama ni kweli Muundo ulipitishwa, ni kwa nini hadi sasa watumishi waliopewa vyeo mbalimbali mishahara yao haijarekebishwa? Je, mbona Katibu wa Bunge payroll yake bado iko vilevile?
Je, Katibu wa Bunge anaweza kuonesha hiyo ripoti ya tathmini inayoonesha ufanisi uliongezeka kwa maana ya kupunguza gharama za uendeshaji kwa utitiri huu wa wafanyakazi waliopo sasa?
Tatu, gari lililolengwa ni lenye namba CKA lililokuwa linatumiwa binafsi na Katibu wa Bunge kwa miaka zaoido ya miwili kwa gharama za serikali; na si magari yote.
Kwanini Katibu wa Bunge anakwepa hoja ya msingi kwa kuunganisha na magari yanayokodiwa kwa ajili ya vikao vya Kamati ambayo ni mambo ya kawaida?
Nne, je, Katibu wa Bunge anashindwa nini kuonesha mkataba uliosainiwa na aina ya magari yaliyotakiwa kununuliwa? Je, si kweli kwamba baada ya kuleta magari hayo ambayo ni tofauti ndipo ofisi ilipoanza kuhangaika kubadilisha mihtasari ya kikao cha Bodi ili kuhalalisha kitu ambacho kimeshafanyika?
Tano, kuhusu tiketi za ndege, anaweza kuonesha boarding passes za maofisa wa Bunge waliosafiri nje na hata ndani ya nchi?
Sita, Rais John Magufuli, amekuwa akisisitiza dhana ya mtumishi muda wake unapowadia, aweze kustaafu isipokuwa pale mtumishi huyo na kada yake vinapokuwa adhimu na kwa sababu maalumu.
Je, kuongeza mikataba kwa watumishi ambao kada zao si adimu na kulazimisha kuongezwa mikataba ambayo inaenda kinyume na dira ya rai, ni uadilifu?
Mtumishi aliyetajwa kwenye habari iliyopita ana umri wa miaka 67 sasa wakati umri wa kustaafu kwa lazima kwa mtumishi wa kada yake ni miaka 60.
Kitaaluma mtumishi huyo ni karani wa kumbukumbu, lakini amekuwa anafanya kazi za Ofisa Usafiri wakati huo huo ofisi imeajiri maafisa usafiri wanaofanya kazi zisizo zao kitaaluma. Je, Bunge lilishindwa nini kuishauri Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili mtumishi huyu aweze kung’atuka?