Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imetoa wito kwa Serikali kutafutia ufumbuzi changamoto ya kelele ambayo imekuwa kero kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ndogo Kilumbe Ng’enda wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022 mbele ya ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo leo Januari 24, 2023 jijini Dodoma.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo,Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imesema inaendelea kusimamia na kutoa elimu kuhusu Mwongozo wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo.
Amesema mwongozo huu unalenga kuboresha usimamizi na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo kwa kuanisha namna ambavyo wadau mbalimbali wanatakiwa kushiriki katika kupunguza kero zitokanazo na kelele na mitetemo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko dhidi ya kelele na mitetemo ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau,Khamis amesema Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) inaendelea kusimamia utekelezaji wa mwongozo huo.
“Mtakumbuka mwaka 2021 tulikutana na wizara mbalimbali tukatoa tamko la la pamoja yote haya ni kuhakikisha tunasimamia ipasavyo mwongozo huu ili wananchi waepuke na adha ya kelele hiz,” amesema Naibu Waziri.