MOROGORO

Na Everest Mnyele

Japo haisemwi, kimsingi ukweli ni kwamba Bunge ndilo husimamia mihimili mingine yote; yaani Utawala na Mahakama.

Ukuu wa Bunge; Bunge lisilo na woga, hupatikana pale tu panapokuwapo Katiba thabiti ya wananchi.

Kwanza, ni lazima tutambue katiba thabiti ni ya namna gani kabla ya kuzungumzia umuhimu wake katika uwajibikaji na utawala bora.

Wengi wanaamini Katiba thabiti ni ile inayotokana na wananchi kwa namna wanavyoiona inafaa kuendesha shughuli zao za kujitawala kiuchumi, kisiasa na kijamii. 

Katiba hii itaweka bayana mgawanyo wa madaraka kati ya Utawala, Bunge na Mahakama na jinsi wanavyopaswa kuangaliana (checks and balances) kwa manufaa ya taifa.

Mihimili hii inapaswa kufanya kazi kwa uwazi, haki na kuwajibika kwa wananchi. Hivyo tunapaswa kuona utawala unaowajibika kwa wananchi kwa kuhakikisha nchi ni salama, wananchi wanapata huduma kwa haki, usawa na uwazi; pia kuwa na serikali inayopokea ushauri na kufanyia kazi mara moja mawazo na ushauri unaotolewa na Bunge. 

Pia ni matarajio kuwa serikali itakuwa na taasisi imara na mifumo bora itakayowezesha wananchi kupata huduma wanayoitarajia kadiri Katiba inavyowaelekeza.

Vilevile ni kazi ya serikali kuonyesha kwa vitendo utawala bora na wale walio kwenye mamlaka waonyeshe wanafuata misingi yake.

Mwisho, Katiba thabiti inaweka mipaka ya serikali, madaraka ya Rais na namna anavyopaswa kusaidiwa katika uteuzi wa wakuu wa taasisi ili kuziimarisha katika uwajibikaji kwa wananchi.

Upande mwingine, Bunge linapaswa kufanya kazi ya kutunga sheria kadiri ya mahitaji ya nchi kwa wakati husika, kuishauri, kuisimamia na kuikosoa serikali bila woga wowote na ikilazimika kuiwajibisha serikali kadiri Katiba inavyoelekeza.

Bunge lazima lionyeshe ukuu wake (supremacy of the parliament). Ni dhahiri kuwa Katiba inayosimamia uwajibikaji na utawala bora itahakikisha hakuna kitu kinafanyika bila idhini au uthibitisho wa Bunge.

Nitatoa mfano nieleweke vizuri. Ni kazi ya Bunge kujadili na kupitisha Bajeti ya nchi, kuthibitisha wateuliwa wa nafasi mbalimbali kama majaji na wakuu wa taasisi nyeti baada ya kushauriwa na taasisi na mifumo inayosimamia michakato ya uteuzi. 

Hii yote huwasaidia walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali kuona kuwa wanawajibika zaidi kwa wananchi na taifa wala na si kwa aliyewateua peke yake. 

Hivyo ni muhimu Bunge kuonyesha ukuu wake bila woga, kwani hiki ndicho chombo cha kuwasemea, kuwatetea na kuwaongoza wananchi.

Bunge husimamia mihimili mingine japo si moja kwa moja, kuhakisha uwajibikaji kwa viongozi ni wa hali ya juu kabisa.

Mahakama kazi yake ni kutafsiri sheria na kuhakikisha haki inatendeka. 

Muhimu hapa ni Mahakama kuwa huru (independency of Judiciary) katika kutenda kazi zake. 

Nisisitize, Mahakama si tu inapaswa kuwa huru, bali ionekane ipo huru.

Haki isipopatikana mahakamani, wananchi, taasisi na hata Serikali hukosa matumaini katika maisha kwani kutofautiana na kugombana ni hulka ya binadamu. Ni Mahakama ndiyo sehemu pekee ya kutoa haki na kuleta matumaini. 

Huu ni mhimili muhimu sana katika kuleta utangamano. Ni chombo pekee ambacho wateule wake wa juu wanapaswa kuonyesha ubobevu, ujuzi na busara kubwa japokuwa wanaongozwa na sheria.

Awali nimeeleza kwa ufupi nini Katiba inapaswa kuelekeza na ngu0vu yake katika kuwawajibisha waliopewa mamlaka ya kuwatumikia wananchi. 

Hivyo kwa kuwapo Katiba thabiti, huboresha uwajibikaji wa Serikali, Bunge, Mahakama na taasisi zote. 

Kwa serikali, hii isipowajibika kwa wananchi hutolewa madarakani kupitia sanduku la kura au namna nyingine inayofaa.

Kwa Bunge, wabunge wasipowajibika hawatarudi bungeni na au Bunge linaweza kuongozwa na chama kingine. 

Mifano hii miwili unaonyesha jinsi gani Katiba thabiti husabaisha watu na viongozi kutimiza majukumu yao.

Serikali, kwa kuogopa kutolewa madarakani, itawasimamia wateule na taasisi za huduma kwa jamii wafanye vizuri kadiri ya matarajio ya wananchi, nje ya hapo watawajibika. 

Kwa ujumla, kuwepo kwa Katiba thabiti huleta uwajibikaji na kuimarisha utawala bora, hivyo wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa ufanisi; hatimaye kupata ustawi na furaha ya kweli.

Tusidanganyane, bila kuwa na Katiba thabiti, uwajibikaji na utawala bora vinabaki hadithi ya mdomoni na wananchi wataendelea kulalamika. 

Kuwa na Katiba thabiti yenye kuruhusu uhuru wa mawazo, demokrasia ya kweli na utawala bora ni afya kwa taifa na ni mwanzo mzuri wa kuleta ubunifu, nje ya hapo ni udumavu, kufanya kazi kwa mazoea ya ‘bora liende’. 

Woga unatuchelewesha kupata Katiba, au kwamba tunaishi leo bila kufikiria changamoto zinazoweza kutukabili baadaye. 

Tusidanganyane, Katiba thabiti ni ngome pekee ya kutufanya tutoke tulipo na kutupeleka mbele, kwani hali ya uwajibikaji na utawala bora kwa sasa haviridhishi kabisa.

Ripoti ya CAG ni ushahidi ingawa inasema machache kati ya mengi. 

Ndugu zangu, nchi hii ni nzuri sana lakini mifumo yetu na utendaji wetu vinatufanya tuwe mahali ambapo si sahihi kama Tanzania. 

Niwahakikishie, tunahitaji Katiba thabiti au mpya kuweka mambo sawa ili kuwe na nidhamu, uwajibikaji pamoja na utawala bora. 

Tunaweza kujidanganya kuwa tunakwenda sawa, lakini tungekwenda zaidi ya mara 1,000 kwa kufanya mabadiliko ya kimkakati. 

Mungu ibariki Tanzania na watu wake wote!