Leo Bunge la Jamhuri ya Muungano linaanza mikutano yake mjini Dodoma, huku wafanyakazi na Watanzania kwa jumla wakitarajia kusikia limeifanyia marekebisha ya Sheria mpya ya Mafao ya wanachama wa Mifuko ya Jamii.

Kwa miezi kadhaa sasa tumeendelea kusikia kilio cha wafanyakazi wakilalamikia kipengele cha sheria hiyo kinachofuta fao la kujitoa, ambacho kinataka mwanachama aliyeacha au kustaafu kazi asipewe mafao yake kabla ya kufikisha umri wa miaka 55 au 60.

 

Kipengele hicho kinalalamikiwa kuwa ni cha kikandamizi dhidi ya wafanyakazi, kwani kinawanyima uhuru wa kuchukua na kutumia wakati wowote fedha zao ambazo wamekuwa wakikatwa katika mishahara yao.

 

Sisi JAMHURI tunaungana na wafanyakazi katika kulihimiza Bunge na Serikali kwa jumla kutengua kipengele hicho ili kuwaondolea wanachama wa mifuko hiyo kero isiyo ya lazima, hivyo waweze kunufaika na mafao yao wakati wowote.

 

Tunasisitiza jambo hili tukiamini kuwa hatua ya kutaka mfanyakazi atimize umri wa miaka 55 ndipo adai mafao yake, haitakuwa na manufaa kwa wahusika kutokana na ukweli kwamba wengi wanaweza kutangulia mbele ya haki kabla ya kutimiza umri huo.

 

Lakini pia, kama wadau mbalimbali wanavyosema, imethibitika mara nyingi kuwa wastaafu wenye umri wa kuanzia miaka 55, wamekuwa wakipata adha mbalimbali wakati wa kudai mafao yao katika mifuko hiyo na serikalini.

 

Kwanza ifahamike kwamba watu wa umri huo huwa tayari ni wazee na wengi wao huwa wanaishi vijijini, ambako inawawia vigumu kusafiri kwenda kudai mafao yao katika ofisi husika mijini.

 

Ukiritimba wa viongozi wa mifuko ya jamii na serikali katika kushughulikia madai ya wastaafu nchini, umesababisha wengi kudidimia kiuchumi na familia zao, huku fedha zao walizokatwa kutoka kwenye mishahara yao zikiendelea kushikiliwa na ‘wajanja’ wachache.

 

Uzoefu unaonesha kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakipigwa danadana wanapoanza kudai mafao yao na wengine wameishia kufariki kabla ya kulipwa haki zao. Mwalimu James Irenge, aliyemfundisha Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere amefariki akiwa bado hajalipwa mafao yake.

 

Kwa hiyo, mkutano wa Bunge unaoanza leo mjini Dodoma, pamoja na majukumu mengine muhimu, lishughulikie suala hilo la kurejesha fao la kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii, ili  kuondoa manung’uniko yanayoendelea kufukuta miongoni mwa wafanyakazi nchini.

 

Msimamo wa JAMHURI ni kwamba wafanyakazi wanastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa hasa linapokuja suala la kupewa haki zao. Bunge na Serikali kwa jumla vitakuwa vimeonesha kuthamini mchango wa wafanyakazi katika ujenzi wa Taifa letu kwa kurekebisha sheria hiyo.