Nimemsikiliza Naibu Spika Job Ndugai akilalamika kwamba nidhamu ya baadhi ya wabunge, hasa vijana si nzuri. Ndugai anarejea matukio kadhaa yaliyotokea wakati wa Mkutano wa Bunge ulioahirishwa wiki iliyopita. Alikwenda mbali zaidi kwa kukumbuka mambo yalivyo tangu kuanza kwa Bunge la Kumi. Analalamika kwamba asilimia zaidi ya 70 ya wabunge wa sasa ni wageni. Kuna vijana wengi ambao bado hawajazisoma na kuzitambua vema Kanuni za Kudumu za Bunge.
Mtazamo wa Ndugai kidogo unafanana na wachambuzi wengine wanaoamini kuwa matumizi ya runinga kurusha vikao vya Bunge, yamechangia wabunge wengi wafanye kazi za kisiasa kuliko za kibunge. Kwa mtazamo wao, wabunge wamejikita zaidi kutaka waonekane kwa wapigakura kuliko kujadili hoja zinazowasilishwa bungeni.
Nina mtazamo tofauti kidogo na ndugu zangu hawa. Kweli inawezekana kuwa ugeni na ujana vikawa vigezo vya kuwapo haya tunayoendelea kuyaona na kuyasikia katika vikao vya Bunge. Kweli, inawezekana wakawapo wabunge wanaotaka kuwafurahisha wapigakura ili ikiwezekana mwaka 2015 wawatazame kwa jicho la huruma.
Mwanzoni mwa Mkutano uliomalizika, Mbunge wa Isimani, William Lukuvi (CCM), alimpongeza kiongozi mmoja wa kijiji jimboni kwake aliyewazuia “wapinzani” kuendesha mkutano wa hadhara. Aliahidi kumzawadia kiongozi huyo. Hapo unaweza kuona matumizi ya runinga yalilenga kumhami Lukuvi dhidi ya wanaotamani “jimbo lake.”
Mtazamo wangu kwa hoja ya Ndugai na ndugu zangu wengine ni kwamba jeuri tunayoiona kutoka kwa wabunge – hasa vijana – tena wa vyama vya upinzani na CCM inatokana na ukimya wa Serikali katika mambo ya msingi.
Wafuatiliaji wa mijadala bungeni wanaona na kusikia hoja nzito na za kufikirisha zinazotolewa na wabunge wa kambi zote. Hoja zinazotolewa na wabunge hawa hazipati majibu ya kuridhisha.
Tofauti na wazee, vijana wa dunia ya leo wanataka kuona mambo yakienda kwa kasi zaidi. Hawataki mwendo wa kusuasua. Wanataka kuona watuhumiwa wa masuala mbalimbali wakishughulikiwa haraka. Tena wapo vijana ambao wengine huwa hawataki hata kusubiri sheria ichukue mkondo, bali wao wenyewe waichukue mkononi. Ndiyo maana tunashuhudia mauaji ya wanaojiita “wenye hasira kali” yakifanywa na vijana. Sijasikia magenge ya wazee wakifanya hayo.
Mkutano uliomalizika umeibua hoja nzito. Kwa mfano, tumeambiwa kuwa kuna kundi la Watanzania kadhaa wenye ukwasi wa Sh bilioni zaidi ya 300 ughaibuni. Hili ni jambo zito, hasa tunapoelezwa kuwa fedha hizo, ama zimeibwa nchini au ni matokeo ya rushwa.
Majibu ya Serikali kwa jambo kubwa kama hili ni, “mwenye ushahidi aulete”. Wabunge wengi walichotaraji ni kupata majibu ya Serikali ya “hakuna jambo kama hilo”, au “kweli lipo, na wahusika ni fulani”. Sidhani kwa kufanya hivyo Serikali ingekuwa ikiendelea kuandamwa na wabunge.
Suala la utoroshaji madini nje ya nchi. Juzi, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, ameonekana kwenye runinga akiwa Korea Kusini. Alishuhudia maduka yakiwa yamejaa tanzanite hadi pomoni! Kibaya zaidi, tanzanite hiyo ina maelezo ya kutoka nchi nyingine! Maelezo hayo yanatolewa ilhali dunia ikitambua kuwa tanzanite inapatikana Tanzania tu.
Wabunge wamelia miaka yote tanzanite ichimbwe na wazawa, iwekewe utaratibu wa kudhibitiwa kuanzia machimboni Mirerani, iongezwe thamani hapa hapa nchini na kadhalika. Haya yote hayafanywi na Serikali inayojinasibu kuwa ni sikivu! Kigugumizi hiki kinatokana na nini?
Kumekuwapo hoja ya utafiti na uchimbaji madini ya urani. Tajiri anakiuka sheria kwa kukaribisha kampuni za nje. Wengine wanaingia ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuchimba dhahabu! Wanashirikiana na polisi. Serikali imelala, haioni wala haisikii hadi iambiwe na wabunge au waandishi wa Serikali. Ndiyo maana wabunge wanahoji, “Huu usalama wa Taifa ni wa kuwalinda viongozi wakuu tu?”
Mgodi wa dhahabu Buhemba, baada ya waporaji raia wa Afrika Kusini kuondoka, waliacha mitambo yote yenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Serikali ikawaweka polisi walinde. Polisi ndiyo wakawa mawakala wa waporaji na wezi. Wakawaita wezi hadi kutoka Kenya kwenda kuchukua kila walichotaka kuanzia mabati, madirisha, vitasa, magari hadi mitambo ya mabilioni ya shilingi. Wabunge wakasema. Wakalalamika. Waandishi wakaandika, lakini “Serikali sikivu” ikaendelea kuwa kimya hadi mali zote zilipoibwa.
Juzi tu bungeni ikatolewa hoja kwamba Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mama Anna Abdallah, ameshirikiana na wajumbe na wasio wajumbe wa bodi kujimegea mamilioni ya shilingi za posho. Fikiria, anasimama mbunge anawataja wenzake walivyogawana fedha, mbunge mmoja amesaini mara mbili na kulipwa mara mbili, mke wa mjumbe wa bodi naye kalipwa kama mmewe ambaye ni mjumbe.
Kashfa hii kubwa inazungumzwa bungeni. Inaachwa ipite hivi hivi, pengine kwa sababu Mama Anna ni mke wa Spika mstaafu! Katika hali ya kawaida, mbunge gani mwenye kuitakia mema nchi yake anaweza kuwa na nidhamu kwa kiti cha Spika?
Alisimama Mbunge David Kafulila. Akawataja kwa majina wabunge wenzake wala rushwa. Rekodi za Bunge zipo. Tuhuma nzito kama hii ikaachwa ipite kama upepo tu. Mungu si Athumani, siku ya siku mmoja wa waliotajwa akakamatwa akipokea rushwa! Sasa anatuhumiwa, na kesi yake ipo mahakamani. Je, ingekuwaje kama Kafulila angesikilizwa?
Wakati wa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki rushwa ilisambazwa bila woga. Kuna wabunge waliounda magenge ya upokeaji na usambazaji rushwa. Wabunge kadhaa wa Mkoa wa Dar es Salaam wanajijua kwa kushiriki dhambi hiyo. Wabunge waungwana wakasema Bunge halikuwasikia. Waandishi wa habari wakaandika, hakuna aliyethubutu kuheshimu maandishi yao. Mwisho wa siku wenye fedha wakashinda. Wasio na fedha, lakini wakafanikiwa kushinda ni wachache.
Mhimili mkubwa kama Bunge unapotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, lakini ukakaa kimya, mbunge gani zuzu atakayekiheshimu kiti cha Spika? Kamati ya Nishati ni tone tu. Kamati zote zina walakini.
Watanzania wanalia umasikini. Wanajiuliza, mbona Tanzania ina madini ya aina zote? Mbona ina gesi (na mafuta yapo), ina Serengeti ambayo ni hifadhi kubwa duniani? Mbona ina Selous ambalo ni pori la akiba kubwa kuliko yote duniani? Mbona ina pwani ya bahari yenye urefu wa kilometa karibu 1,000? Mbona Tanzania ina mito mikubwa katika Afrika? Mbona Tanzania ina maziwa makubwa katika Afrika? Huo Mlima Kilimanjaro, lini umehitaji kipuri ili uendelee kuwapo? Bandari zetu – Tanga, Dar es Salaam, Mtwara – mbona zinatosha kuikomboa Tanzania?
Nchi ambayo ina misitu ya kila aina, nchi ambayo inastawi kila kitu, nchi ambayo kijiografia inategemewa na mataifa mengi, nchi ambayo kisiasa ni imara, nchi ambayo ina lugha moja ya kuwaunganisha watu wake, nchi yenye watu wenye akili, nchi yenye rasilimali watu ya kutosha; kwanini pamoja na sifa zote hizo, inaendelea kuwa masikini?
Wabunge na wananchi wanaoitakia mema wamekuwa wakijaribu kutoa maoni ya kuondokana na umasikini huu. Kwa mfano, wanaiambia Serikali kwamba kwenye madini tunaibiwa. Matumizi ya Serikali ni makubwa mno – kila siku Watanzania lazima waonekane ughaibuni – wizi wa mali ya umma umevuka mpaka, udhibiti wa rasilimali zetu haupo, maadili ya viongozi hakuna.
Pamoja na ushauri wote huu, Serikali imetia pamba masikioni. Wa kuyazibua ni nani? Wa kuyazibua ni Bunge. Wabunge wanazungumza, lakini kiti cha Spika ni kama kimeamua kula yamini ya kuitumikia Serikali badala ya kuisimamia! Nauliza, katika mazingira ya aina hii, mbunge gani anayeipenda Tanzania anaweza kuwa na lugha ya staha?
Kwa mfano, hivi kweli Tanzania ya leo, pamoja na misitu yote hii inayokatwa mkaa, inaweza kulia kwa watoto wake kukosa madawati? Kama tunashindwa kuwa na madawati, tutaweza kujenga nyumba za walimu na maabara? Hivi kweli tunakubali shule zetu zifungwe kwa sababu ya kukosa vyoo, tena vyoo vya shimo? Nani katuloga?
Tufanye nini? Bunge liisimamie Serikali. Bunge lisiwe sehemu ya kulinda Serikali inayoshindwa kutekeleza wajibu wake. Lakini kubwa zaidi, Serikali iwashirikishe wananchi katika kujiletea maendeleo. Kinachoonekana sasa ni kwamba akili zetu zote, tukiongozwa na Serikali zimeishia ukingoni mwa miaka mitano, yaani kila baada ya uchaguzi mmoja, tunasubiri mwingine!
Kiti cha Spika kinaogopa. Wabunge wakweli wanajipembua na sasa wanaitwa wakosefu wa nidhamu. Kama kweli mwenendo wenyewe wa Bunge ndiyo huu, kiti cha Spika kitaendelea kupuuzwa maana kinaacha mambo mazito ya nchi yajiendeshe yenyewe. Mhimili wa Bunge usiposemea mambo mazito ya nchi, kazi hiyo itafanywa na mbunge mmoja mmoja. Kwa kuifanya kazi hiyo, sasa wanaambiwa hawana nidhamu!