Leo Bunge linatarajiwa kupokea tamko la serikali kuhusu bei ya nishati ya mafuta ya petroli ambayo kupanda kwake kumesababisha mfumko mkubwa wa bei kuwahi kulikumba taifa na hata dunia katika siku za karibuni.

Uamuzi uliochukuliwa na Bunge wiki iliyopita kujadili kwa dharura kupanda kwa bei ya petroli, japo umekuja kwa kuchelewa, unapaswa kupongezwa na wananchi, hasa wapenda maendeleo.

Hatua hiyo ya Bunge imepokewa kwa faraja kubwa na wananchi waliokuwa wakiwatazama wawakilishi wao kwa jicho la shaka, wakishangaa ni kwa nini hawachukui hatua yoyote kuzungumzia ugumu wa maisha unaowakumba.

Bei ya petroli imeathiri maisha ya kawaida ya Watanzania wengi, kwa kuwa mbali na kupanda kwa nauli za usafiri na usafirishaji, karibu kila bidhaa inayotumika katika maisha ya kawaida nazo zimepanda huku vyanzo vya mapato vikisalia kuwa vilevile.

Macho na masikio ya Watanzania leo yanaelekezwa bungeni jijini Dodoma ambako serikali inatarajiwa kutoa msimamo kuhusu hali hii, huku wananchi wakiamini kuwa hiki ndicho kipimo kizuri cha uimara wa Bunge.

Bunge imara ni lile lenye uwezo wa kuishauri serikali na wakati mwingine hata kuiwajibisha pale inapobidi. Bunge ndiyo sehemu pekee yenye uwakilishi wa uhakika wa wananchi kutoka kila pembe ya Tanzania, hivyo ni hapo ndipo panapopaswa kuzungumziwa matatizo ya Mtanzania mmoja mmoja na kutolewa suluhu.

Wabunge wanapaswa kufahamu kwamba leo uwakilishi wao kwa wananchi unapita katika tanuri la moto, unapimwa na ni matokeo ya taarifa itakayotolewa na serikali na utekelezaji wake ndio utakaolipa heshima Bunge la 12.

Wananchi wanataka na kuamini kuwa Bunge linaweza kubadili mwelekeo mbaya na ugumu wa maisha uliowakumba 

wengi kwa sasa, kwanza kwa kuanza kudhibiti upandaji holela wa bidhaa hasa zile muhimu, kisha kushusha bei ya petroli.

Kwa hali ilivyo hivi sasa, iwapo bei ya petroli haitadhibitiwa ni wazi wananchi watakumbana na hali ngumu zaidi pale muda wa kulipa ada utakapowadia, kwa kuwa kuna kila dalili kwa shule za binafsi kupandisha ada.

Tunaamini kama Bunge likiamua, serikali itakubali kupunguza tozo kadhaa zilizopo katika petroli, hivyo kupunguza kwa kiwango fulani bei ya nishati ya mafuta.