pg 1Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa wahusika kwenye ufisadi huo ni Naibu Katibu wa Bunge, Raphael Nombo; na Mkurugenzi Msaidizi wa Bunge (Utawala), Ndofi Merkion.

Kiasi cha fedha wanachodaiwa vigogo hao ni Sh milioni 103 ambazo walilipwa kwa kigezo cha kusafiri nje ya nchi, lakini badala yake walipokea malipo na kubaki nchini.

Kwenye ufujaji huo, Nombo anadaiwa Sh 32,281,757; ilhali Mpanda akiwa anatakiwa arejeshe Sh 71,281,757.

Mei 27, mwaka juzi, Nombo alilipwa Sh milioni 22.317 kwa ajili ya safari ya Israel katika Chuo kilichotajwa kuwa ni cha Galilee; na akalipwa kiasi kingine cha Sh milioni 9.8 kama ada.

Pia imebainika kuwapo kwa malipo ya posho ambayo baadhi ya wakurugenzi, akiwamo Nombo, hujiandikia viwango vya kulipwa.

Baadhi ya malipo hayo, JAMHURI imeambiwa kuwa hufanywa kwa wahusika licha ya ukweli kwamba kazi wanazokuwa wakizifanya ni sehemu ya utendaji kazi wao wa kila siku.

“Kuliwekwa utaratibu kila anayesafiri awasilishe boarding pass kama retirement jambo ambalo liliwakwaza wahusika kwa sababu walizoea kuchukua fedha na posho za safari, lakini hawaendi au wanaenda siku moja ya pili wanageuza.

“Safari ya Hispania mwaka 2015 ilikuwa ni siku 10 badala yake ndani ya siku tatu walikuwa wamegeuza- waliosafiri ni Katibu wa Bunge na wenzake.

“Kulikuwa malipo ya safari ya Israel- Nombo na Mpanda- walilipwa fedha, lakini hawakwenda na walipotakiwa kurudisha fedha hawakurudisha,” kinasema chanzo chetu.

Aidha, taarifa za uhakika kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zinaonesha kuwa wakurugenzi na watumishi wengine wa Bunge walikuwa wakitumia viwango vya kubadilisha fedha za kigeni kwa kukadiria vile vya mitaani badala ya kufuata vilivyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Kwa mfano BoT viwango vya kubadilisha vinaweza kuwa Sh 2,000 kwa dola moja ya Marekani wao wakaandika ni Sh 2,300. Hii ilifanywa zaidi na kampuni ya wakala wa tiketi za ndege. Kuna wakati ziliokolewa Sh milioni 400 kwa hati moja tu ya malipo; sasa fikiria mchezo huu umefanywa mara ngapi na kwa miaka mingapi kama hati moja tu ziliokolewa milioni 400,” kimehoji chanzo chetu kutoka Takukuru.

JAMHURI imethibitishiwa kuwa mwaka jana pekee, Bunge liliilipa kampuni ya uwakala wa tiketi za ndege ya Bon Voyage Sh bilioni 7 zikiwa ni malipo kwa tiketi za ndege za wabunge, wakurugenzi na maofisa kadhaa wa Bunge.

Chanzo chetu cha habari kutoka bungeni kinasema kuwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, licha ya kujua ukweli juu ya malipo hewa, yakiwamo yaliyofanywa kwa Nombo na Mpanda, haoneshi kuchukua hatua zozote za kinidhamu.

“Atachukuaje hatua wakati hawa ni sehemu ya mtandao wake? Ukijua walipataje nafasi hizo huwezi kushangaa kuona hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yao,” kimesema chanzo chetu.

 

Ofisi Binafsi

Ili kuweka mtandao usioweza kuhoji kinachoendelea ndani ya Bunge, taarifa zinasema Katibu wa Bunge Dk. Kashililah kwa ajili ya kulinda maslahi yake amejitengezea tabaka la wateule wachache ambalo lipo tayari kumlinda kwa gharama yoyote.

“Na kwa kuwa linahusisha fedha, hakuna hata mmoja anayefumbuka macho kuona kwamba hizo ni harakati za kuzibwa midomo hata watakapoona uozo wowote wasiwe na nguvu ya kuusemea. Ni kama vile wamelishwa yamini!

“Yametengenezwa matabaka ya watu wanaoishi kama malaika na wanaoishi kama mashetani,” kimesema chanzo chetu.

Ni kwa mbinu hiyo, inaelezwa kwamba Katibu wa Bunge ameridhia mfumo wa malipo kwa ajili ya viongozi wakuu wa Bunge wa kulipwa posho ya ziada mbali na posho nyingine zote wanazolipwa, kwa madai kuwa ni ofisi nyeti na zinafanya kazi nyeti.

Posho zinazolipwa kwa Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge, Naibu Makatibu wa Bunge (wawili) na Wakurugenzi wao wa Ofisi Binafsi ni Sh 250,000 kila siku wanapokuwa kazini, licha ya kuendelea kupokea mshahara.

Watumishi walio katika Ofisi hizo binafsi kama makatibu muhtasi, wahudumu na madereva hulipwa Sh 150,000 kila siku.

“Malipo hayo ni ya kila siku- haijalishi wamekuja kazini au la! Wapo likizo au wapo safarini- ni lazima walipwe! Malipo hayo ni mbali na mshahara na posho nyingine, hivyo kulingana na nafasi aliyonayo mfanyakazi hujilipa kati ya Sh 4,500,000 hadi Sh 7,500,000 kwa mwezi,” kimesema chanzo chetu.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya alipoulizwa na JAMHURI juu ya viwango hivi, amesema: “Katibu hatengenezi mfumo wa malipo kwa mtumishi yeyote, bali Tume hutoa vibali kwa matumizi ya posho au malipo ya aina yoyote kwa watumishi au hata viongozi ambayo huwekwa kwenye kanuni za uendeshaji Bunge; na haijawahi kutokea mtumishi akalipwa posho akiwa likizo.”

 

Ununuzi samani za ofisi

Katika hatua nyingine ya kutia shaka, kampuni moja imekuwa ikishinda zabuni za kusambaza samani katika ofisi za Bunge.

Chanzo cha habari kimesema kampuni hiyo, hivi karibuni ilipewa zabuni ya kusambaza mapazia katika baadhi ya ofisi za viongozi wa Bunge kwa gharama ya Sh milioni 30.

“Sofa na samani nyingine za ofisi bei zake huwa ni mara tano ya bei iliyopo sokoni. Lakini cha ajabu bado ofisi inamng’ang’ania,” kimesema chanzo chetu.

Kuna taarifa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ukaguzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Ununuzi (za Bunge), wamekalia kuti kavu baada ya kuhoji ununuzi huo.

“Awali walihoji samani zilizokuwa zinunuliwe kwa ajili ya nyumbani kwa Spika; walihoji kuhusu gharama za samani hizo kuwa hazilingani na thamani halisi. Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni alimkatalia Katibu wa Bunge kuidhinishia samani za Sh milioni 387 ambako gharama halisi ilikuwa Sh milioni 175.

“Lakini lengo ilikuwa fedha zinazobaki zitumike kuweka samani nyumbani kwa Katibu wa Bunge. Baada ya Wenyeviti hao kuonesha ufuatiliaji na kuhoji ununuzi huo, samani hizo hazikununuliwa, lakini Katibu wa Bunge aliapa kuwahamisha ofisi watendaji hao wa Ofisi ya Bunge kwa kumwekea vikwazo,” kimesema chanzo chetu.

Mwandumbya, alipohojiwa kuhusiana na hili amesema: “Kampuni ya (anaitaja) imekuwa ikitoa huduma mbalimbali katika Ofisi ya Bunge, mchakato wa tenda na utaratibu wake huratibiwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi na mikataba huhusishwa wahusika tu.”

 

Mipango ya kulihama Bunge

Duru za uchunguzi zibenaini kuwapo kwa juhudi kubwa zinafanywa na baadhi ya wakurugenzi wa Bunge waweze kuhamishiwa sehemu nyingine.

Vyanzo vya uhakika kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma vinasema kuna maombi ya baadhi yao wanaotaka wahamishiwe Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Wanafanya lobbing (uzengezi) wahamishwe Bunge maana wanajua wameharibu. Wanajua Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kuacha haya yapite hivi hivi, lakini wasichojua ni kwamba hata huko waendako hawawezi kuachwa tu watambe,” kimesema chanzo chetu.

Wiki iliyopita, JAMHURI liliripoti kuwapo matukio ya ufisadi ndani ya Bunge yanayohusu malipo ya Sh bilioni 6 kwa kampuni ya bima ya Jubilee.

Malipo hayo kwa bima ya wabunge na familia zao yalianza kulipwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Kiwango hicho kiliafikiwa kutoka kile cha awali ambacho kilikuwa ni Sh bilioni 9 kwa mwaka, lakini ‘kikapunguzwa’ hadi Sh bilioni 6 kwa mwaka.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwapo kwa maslahi binafsi wanayopata baadhi ya viongozi waandamizi wa Bunge pamoja na ‘washenga’ waliofanikisha zabuni hiyo.

Imebainika kuwa kabla ya kuanza utaratibu wa bima kwa wabunge na familia zao, Bunge lilikuwa likitumia kiasi kisichozidi Sh bilioni 3 pekee kwa mwaka kugharimia matibabu kwa walengwa hao.

“Tulishangaa kuona tunaachana na malipo yasiyozidi Sh bilioni 3 kwa mwaka kwa matibabu ya waheshimiwa wabunge na familia zao na kwenda hadi Sh bilioni 9. Hizi Sh bilioni 6 zinazolipwa sasa ni baada ya wakubwa kuona kiwango cha bilioni 9 ni kikubwa mno kwa hiyo wakaomba Jubilee wakipunguze na wao wakakishusha hadi Sh bilioni 6,” kilisema chanzo chetu.

Mpango mzima wa kuifanya Jubilee kushinda zabuni hiyo ya Bunge ulisukwa na kufanikishwa na raia wa Kenya (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye anasifika kwa kujihusisha na masuala makubwa ya kifedha. Mkenya huyo yuko kwenye orodha ya watu wanaotuhumiwa kuhusika kwenye utakatishaji fedha kupitia Benki ya Stanbic.

 Hata hivyo, Afisa mmoja wa Jubilee ameliambia JAMHURI, kuwa kampuni hiyo ilipata zabuni kwa nia ya kuokoa maisha ya wabunge na kuepusha ubaguzi na ucheleweshaji wa huduma ya matibabu kwa wabunge uliokuwa unafanywa na hospitali za Serikali kabla.

“Kulikuwapo urasimu mkubwa kuwapatia wabunge visa za matibabu. Unajiuliza, mbunge anaumwa, alafu anapitishwa katika urasimu mrefu hadi kufikia hatua ya kupata kibali cha kwenda India kwa kiwango kinachotishia kupoteza maisha ya waheshimiwa wabunge. Hapo ndipo busara ilitumika kuhamishia huduma hii ya matibabu katika bima, ambapo mbunge akipata tatizo anahudumiwa mara moja,” amesema Afisa huyo.

Ameutetea mpango huu kwa kusema haukuwa na harufu yoyote ya ufisadi na akasema kampuni yao iko tayari kufafanua zaidi utaratibu uliotumika kupata zabuni hii anayoamini imekuwa msaada mkubwa kwa wabunge.