Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, imepinga maombi ya wapangaji wa Shirika la Nyumba Taifa (NHC) ya kuuziwa nyumba wanamoishi.
Msimamo huo umetolewa kwenye taarifa ya Kamati hiyo ya utekelezaji majukumu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2011/2012 na kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013. Taarifa hiyo ilisomwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Abdulkarim Shah, bungeni, jana.
“Kamati inaendelea kusisitiza kuwa haikubaliani na utaratibu wa kuuza nyumba za Shirika zilizoko sasa kwa kuwa nyumba hizo ni mali ya Watanzania wote.
“Kamati inashauri Shirika la Nyumba kuendeleza juhudi zake katika ujenzi wa nyumba mpya 15,000 ambazo asilimia 70 zitauzwa kwa wananchi na asilimia 30 zitapangishwa. Hivyo, Kamati inawashauri wapangaji wa Shirika kujipanga kununua nyumba mpya zitakazojengwa na Shirika.
“Aidha, kwa kuwa sehemu kubwa ya nyumba za Shirika zipo katika maeneo mazuri ambayo thamani ya ardhi ni kubwa kuliko thamani ya nyumba, Kamati inashauri kuwa nyumba zote za Shirika zilizochakaa na ambazo uendeshaji wake ni mkubwa kuliko faida inayopatikana, zibomolewe na maeneo hayo yaendelezwe kwa kujenga majengo ya kisasa yatakayoendana na thamani ya ardhi ya eneo husika.
“Kamati inatoa angalizo kwa Shirika litakapokuwa likijenga nyumba zake kuhakikisha wanatenga maeneo ya wazi kwa ajili ya michezo ya watoto, maeneo ya kuegesha magari, na kadhalika,” imesema taarifa ya Kamati hiyo.
Katika hatua nyingine, Kamati imeshauri Wizara ya Fedha kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika nyumba za NHC zinazouzwa kwa wananchi.
Kamati imesema kuwapo kwa VAT kwenye nyumba hizo kunafanya ziuzwe kwa bei kubwa ambayo wananchi wa kawaida hawawezi kuimudu.
Naye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, akiwasilisha makadirio ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, na wafanyakazi wote wa shirika hilo kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanywa.