Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha Bilioni 215.25 ikiwa ni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2023/24..
Aidha Wizara hiyo ndio inayosimamia Mapinduzi ya Kidijitali nchini yanayoweka msingi wa kulipeleka Taifa kwenye Uchumi wa Kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti hiyo leo Mei 19,2023 Bungeni Dodoma,Waziri mwenye dhamana hiyo Nape Nnauye amesema kulingana na Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2021, Sekta ya Habari na Mawasiliano imekua kwa asilimia 9.1 mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 8.4 mwaka 2020 na kwamba ukuaji huu unathibitishwa na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano na kusambaa kwa huduma zitolewazo na Vyombo vya Habari.
Amesema fedha hiyo itasaidia utejekezwaji wa miradi ya ikiwemo Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano uliotengewa Shilingi bilioni 149.7, Mfumo wa Anwani za Makazi wenye jumla ya Shilingi bilioni 40, Mradi wa Tanzania ya Kidijitali uliotengewa Shilingi bilioni 39.3, Mradi wa Elimu kwa Umma uliotengewa jumla ya Shilingi milioni 940, Mradi wa Kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji wa Vifaa vya TEHAMA Shilingi bilioni 3.3, Mradi wa Upanuzi wa Usikivu kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Shilingi bilioni 13.1 na Mradi wa Kufunga Mtambo mpya wa Kisasa wa Uchapaji Shilingi bilioni 9.4.
Amesema Ununuzi wa mitambo kwa ajili ya vituo 112 vya kutolea Huduma (transmission and power equipment) umekamilika ambapo usimikaji umefanyika kwenye vituo 61 vya kutolea huduma. Usimikaji pamoja na uunganishaji wa mawasiliano katika vituo vingine 50 unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023.
Pamoja na hayo amesema Sekta ya Mawasiliano imeendelea kukua, takwimu zinaonyesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 55.7 mwezi Aprili, 2022 hadi kufikia laini milioni 62.3 mwezi Aprili, 2023 na Watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 29.9 mwezi Aprili, 2022 hadi kufikia milioni 33.1 mwezi Aprili, 2023.
“Watoa huduma wa Miundombinu ya Mawasiliano wamefikia 23 ukilinganisha na watoa huduma 22 mwezi Aprili, 2022 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4.5,watoa huduma za ziada (Application Services and Value Added Services) wamefikia 141 ukilinganisha na watoa huduma 102 mwezi Aprili, 2022 sawa na ongezeko la asilimia 38,”amesema.
Pia ameeleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa kuiongezea uwezo minara inayotumia teknolojia ya 2G pekee ili iweze kutoa pia huduma ya intaneti kwa kiwango cha 3G na 4G, na kuwawezesha wananchi kupata huduma za kidijitali ambapo kufikia mwezi Aprili, 2023 minara 227 imeongezwa uwezo huo.
Aidha, Serikali inaendelea na mradi wa kufunga mtandao wa intaneti katika maeneo ya wazi yanayotumiwa na wananchi katika shughuli zao.
Kuhusu kufanya mapitio ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, Waziri huyo ameeleza kuwa Muswada wa marekebisho ya Sheria hiyo umesomwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Februari, 2023, kukamilisha rasimu ya Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa umma, Kuratibu Vyombo vya Habari katika matukio ya Kitaifa na ziara za Viongozi nchini na kutoa msaada wa kitaalamu kwa Wizara na Taasisi za Serikali.
Amesema Wizara pia imefanikiwa kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi nchini ambapo hadi Mwezi Aprili, 2023 jumla ya Anwani za Makazi 12,669,718 zimetolewa nchini, vilevile, Wizara kufanikiwa kuratibu ushiriki wa Sekta katika shughuli za kikanda na kimataifa ikiwemo mikutano ya JPC, ATU, ITU, UPU, CTO, UPU, PAPU na kukuza mashirikiano na nchi za USA, China, Vietnam, DRC, Oman, Afrika Kusini na Malawi. Aidha, Tanzania imefanikiwa kupata kiti katika Baraza la Umoja wa Mawasiliano Afrika na Umoja wa Mawasiliano Duniani.
“Wizara inajivunia kuboresha Mfumo wa kidijitali wa NaPA kwa kuwezesha Mfumo kutambua zilipo huduma za Kijamii na Kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwezesha kufikiwa kirahisi kupitia moduli ya uelekeo ya Mfumo wa NaPA, Aidha, Wizara imeweza kuratibu majadiliano na wadau kwa ajili kufungamanisha Mfumo na mifumo mingine ya Serikali, kama vile TRA kwa ajili ya kurahisisha ukusanyaji wa mapato ,”amesema
Katika uchumi wa kidigitali, Waziri huyo ameeleza kuwa Sekta zote hufanya kazi kwa pamoja, kwa ushirikiano na mwingiliano zikiwezeshwa na mazingira bora ya kidijitali.
Mapinduzi haya yanawezeshwa na misingi muhimu ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mifumo ya Mawasiliano ya simu, usambazaji barua, vifurushi na vipeto kwa njia ya posta, uwepo wa vyombo vya upashanaji Habari pamoja na uimara wa uhuru husika.
Amesema Serikali imeendelea na jukumu la kukagua na kuhakiki ubora wa viwango wa vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki hapa nchini kwa lengo la kulinda usalama na afya za wananchi ambapo Kwa kipindi kinachoishia mwezi Aprili, 2023 TCRA ilipokea maombi ya ukaguzi wa vifaa vya kielektroniki 512 kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi.
Waziri Nnauye amesema maombi 423 sawa na asilimia 83 yalikidhi vigezo na kuidhinishwa kwa matumizi, maombi 76 sawa na asilimia 15 yapo kwenye hatua mbalimbali za ukaguzi na maombi 13 sawa na asilimia 2 yalikataliwa kwa sababu ya kutokidhi vigezo.
Aidha Serikali imeendelea kusimamia usalama mtandaoni kwa kufanya tathimini ya mifumo na miundombinu ya TEHAMA kwa lengo la kubaini madhaifu ya kiusalama na kushauri juu ya hatua za kurekebisha na kujilinda na matishio ya usalama mtandaoni ambapo kufikia mwezi Aprili, 2023, TCRA ilifanya uchambuzi wa anwani za kompyuta zenye viashiria vya kushambuliwa na kutoa mashauri ya usalama mtandaoni (Security Advisories) kwa Taasisi za Umma na binafsi ambapo mashauri 658 yalichambuliwa ukilinganishwa na mashauri 920 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2021/22 ili hatua stahiki ziweze kuchukulia kuimarisha usalama wa mifumo yao.
“Serikali imeendelea kukagua ubora wa huduma za mawasiliano zinazotolewa na watoa huduma. Katika kipindi kinachoishia mwezi Aprili, 2023, TCRA ilipima ubora wa huduma za mawasiliano ya simu inayotolewa na makampuni ya simu hapa nchini na ilibainika kuwa kuna mapungufu ya muunganisho usioridhisha, ubora hafifu wa huduma za sauti na data na kukatika kwa simu kabla haijaunganishwa,”amesema.