*Kura ya kutokuwa na Imani ni kikombe cha shubiri
*Wabunge wanajipanga kupata kura 176 kumwadhibu
*Spika wa Bunge ameahirisha tatizo, Zitto aibuka shujaa

WIKI iliyomalizika ilikuwa ni ya msukosuko wa hali ya juu baada ya Bunge kuamua kumkaanga Rais Jakaya Kikwete kupitia mgongo wa mawaziri wake.
Mijadala iliyotawala bungeni kwa wiki nzima, ilikuwa ikiwasuta mawaziri kwa kushindwa kufanya kazi na hasa kuwasimamia sawia wasaidizi wao ambao ni makatibu wakuu na wakurugenzi wa idara, vitengo na halmashauri mbalimbali nchini, lakini wachunguzi wa mambo wanasema hizo zilikuwa salaam kwa Rais Kikwete.

“Unaweza kudhani wanawakaanga mawaziri, si kweli. Ni vigumu kumwambia mfalme yuko uchi, isipokuwa ukiona hivyo unawafinya wasaidizi wake, wakishituka au wakalia mfalme atawahoji nini kimetokea. Wakati anawahoji, kama amekaa tenge ni lazima akiinuka kwenye kiti chake kuhoji kulikoni joho lake litashuka usawa wa magoti na kumstiri nyeti zake,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:

“Hapa wabunge wakisema Serikali imeshindwa kazi kwa kuruhusu matumizi mabaya, Rais Kikwete hawezi kusema yeye si sehemu ya maovu haya. Uliwahi kuona wapi treni inatembea bila kichwa? Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aliyoyabaini Rais Kikwete anawajibika nayo moja kwa moja.

“Hii ni Serikali ya Kikwete si ya Rais Paul Kagame wala Mwinyi… wakati umefika sasa afukuze watu wanaofuja mali za umma. Akiendelea na mchezo wa kukwepa lawama kwa kuunda Tume kuchunguza matatizo ili ionekane ni Tume imesema na si yeye, anaweza kuweka historia ya kuwa Rais wa Kwanza Tanzania kutomaliza miaka mitano kwa Bunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye,” alisema Mbunge wa CCM kwa sauti ya ukali.

Nguvu za wabunge walizoonyesha bila kujali tofauti zao za kiitikadi zimeliweka Baraza la Mawaziri katika wakati mgumu na sasa ni lazima baadhi ya mawaziri wajiuzulu.

Taarifa zilizopatikana zinasema Rais Kikwete anakusudia kulifanyia mabadiliko makubwa Baraza la Mawaziri apate fursa ya kulisuka upya. Katika mabadiliko hayo, kuna habari kwamba atatumia nafasi zake za kikatiba kuteua wabunge 10 nje ya wabunge wa sasa kuliboresha Baraza jipya atakalounda. Bado ana nafasi saba.

Msumari wa moto umepigiliwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao bila kumung’unya maneno, wamesema endapo mawaziri watuhumiwa hawatajiuzulu, wapo radhi kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Baadhi ya wabunge hao wameenda mbali zaidi na kusema wanaweza kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Jakaya Kikwete endapo atathubutu kuwakumbatia mawaziri hao.

Kwa jinsi hali ya mambo ilivyo, mawaziri walengwa nafasi yao ya kubaki kwenye baraza ni finyu kuliko ngamia kupita kwenye tundu la sindano, hivyo hawana namna nyingine isipokuwa kusalimu amri mbele ya msimamo wa wabunge.

Mawaziri wanaotajwa kuwa wamefeli kwenye utendaji kazi wamekwa wakijitahidi kujitetea, wakisema hawahusiki na udhaifu unaotajwa kuwapo kwenye wizara zao, lakini utetezi wao umeonekana si lolote, si chochote mbele ya wabunge waliokarishwa na ufujaji wa fedha za umma uliopindukia.

Mawaziri ambao wapo kwenye wakati mgumu ni Mustafa Mkulo (fedha), William Ngeleja (Nishati na Madini), George Mkuchika (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Lazaro Nyarandu (Naibu-Viwanda na Biashara), Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk. Omar Nundu (Mawasiliano) na Adam Malima (Naibu-Nishati na Madini).

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Kilimo na Chakula, Proifesa Jumanne Maghembe nao wanatajwatajwa kwenye orodha hiyo.

Wabunge wamewabana mawaziri kwa kutumia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa za Kamati tatu za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa.

Kwenye taarifa ya CAG kumeibuliwa kashfa nyingi za matumizi mabaya ya fedha za umma, misamaha ya kodi, matumizi ya fedha nje ya bajeti iliyoidhinishwa, wizi na ubadhirifu uliopindukia. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Kishapu pekee zimetafunwa Sh zaidi ya bilioni sita, huku watumishi waliohusika kwenye wizi huo wakiendelea na nyadhifa zao bila kuguswa.

Rais Kikwete aliwasili mjini Dodoma, juzi Jumapili katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuona atapambana vipi kurekebisha mambo.

Habari zilizopatikana zinasema baadhi ya mawaziri hao waliwasilisha barua za kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Pinda, Ijumaa usiku.

Vyanzo vya habari vimethibitisha kuwa baadhi ya mawaziri walikuwa wakibubujikwa machozi. Mawaziri Nundu na Dk. Chami wamekuwa wakijitetea kwa nguvu zote wakijaribu kuonyesha kuwa hawahusiki moja kwa moja na kashfa zinazoelekezwa kwao.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), ndiye aliyeibua suala la kuanza mchakato wa kukusanya asilimia 20 ya saini za wabunge ikiwa sehemu ya kuanzisha mchakato wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Tayari saini za wabunge zaidi ya 70 zimeshapatikana.

Chini ya kifungu cha 53A.-(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinasema; “Bila ya kujali masharti ya ibara ya 51 ya Katiba hii, Bunge linaweza kupitisha azimio la kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu endapo itatolewa hoja kupendekeza hivyo na ikapitishwa kwa mujibuwa wa masharti ya ibara hii.”

Kifungu hicho hicho cha 53 (A) (3) kinasema; “Hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitapitishwa na Bunge isipokuwa tu kama- (a) taarifa ya maandishi, iliyotiwa sahihi na kuungwa mkono na Wabunge wasiopungua asilimia ishirini ya Wabunge wote itatolewa kwa Spika, SIKU ANGALAU KUMI NA NNE KABLA YA SIKU INAPOKUSUDIWA KUWASILISHWA BUNGENI;

“(b) Spika atajiridhisha kuwa masharti ya Katiba kwa ajili

ya kuleta hoja yametimizwa. (4) Hoja iliyotimiza masharti ya ibara hii itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. (5) Hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu itapitishwa tu iwapo inaungwa mkono na Wabunge walio wengi.”

Hapa kilichoishitua serikali na kulazimika kuwabana mawaziri wanaotuhumiwa kushindwa kuendesha wizara wajiuzulu, ni kwamba kwanza katika mchakato wa kupata saini 70 wamo hata wabunge wa CCM waliokuwa wa kwanza kutia saini hizo.

Hii maana yake ni kwamba kama zimepatikana saini 73 ndani ya saa tano tu siku ya Ijumaa, hofu inatawala kuwa kwa kuwa kura ya kumwengua Waziri Mkuu ni ya siri, kura zikipigwa Serikali inaweza kupata mshangao wa kubwagwa kwa kupatikana kura 176.

“Ukumbuke wapo wabunge wenye kutamani kuwa mawaziri, hivyo hawa wanaweza kupiga kampeni usiku kucha zikapatikana kura 176 na Waziri Mkuu akaenguliwa,” mmoja wa mawaziri ambaye nafasi yake iko salama aliliambia Jamhuri.

Maana ya kura hizi alizopendekeza Zitto zikipatikana kura 176 katika kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bungeni, zitamlazimisha Rais kutumia kifungu cha 57 (1) (e) kinasema kiti cha Waziri au Naibu Waziri Kitakuwa wazi, iwapo Waziri Mkuu atajiuzulu au kiti chake kikiwa wazi kwa sababu nyingine yoyote. Moja ya sababu inayoweza kutajwa kama nyingine ni pamoja na kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Bunge.

Februari 7, 2008 tulishuhudia tukio kama hili. Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa alipojiuzulu, mara moja hata Baraza la Mawaziri lilivunjika kwa kutumia kifungu hiki. Isipokuwa katika hali ya upotoshaji, taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo zikasema Rais Kikwete amevunja Baraza la Mawaziri. Usahihi Baraza la Mawaziri lilivunjika kwa kitendo cha Lowassa kujiuzulu na hakuna mtu mwingine aliyelivunja.

Wapo wengi waliotupwa nje ya Baraza baada ya hatua hii ya Lowassa na hadi leo wanaugulia maumivu, lakini pia wapo waliopata fursa nyeti baada ya uamuzi huu wa Lowassa hivyo baadhi ya wabunge wanaovizia hali hii kama fisi wanasubiri na wanashadidia Baraza livunjike nao wauone ‘ufalme wa Mbingu’.

Tangazo la Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba Zitto hawezi kuwasilisha hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mkutano wa sasa ni sahihi kwa mujibu wa kifungu cha 53 (A) (3) (a).

Hata hivyo, Zitto kwa kuwa amekwishapata saini hizo 70 zinazohitajika muda wowote kabla ya mwezi Juni, anaweza kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika na kwa mujibu wa Katiba itakuwa imefuata utaratibu hivyo itabidi ijadiliwe Bungeni. Ni kutokana na hili Serikali ikifanya mchezo, vijana wa mjini wanasema ‘itakula kwao’.

Zitto, alisema upigaji kura dhidi ya Waziri Mkuu ungefanyika tu endapo kiongozi huyo asingemshauri Rais Kikwete kuwaondoa mawaziri wazembe.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, mawaziri wote wanawajibika kwa Rais isipokuwa Waziri Mkuu ndiye anawajibika kwa Rais na Bungeni. Bunge ndilo linalopiga kura ya kumthibitisha kazini Waziri Mkuu, hivyo lina mamlaka ya kupiga kura ya kutokuwa na imani naye likijiridhisha kuwa amepoteza uwezo wa kuwasimamia mawaziri walioko chini yake.

Hivyo ikiwa litapiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kifungu cha Katiba kinachovunja Baraza la Mawaziri kitafanya kazi na moja kwa moja mawaziri walengwa watakuwa wameenguliwa kwenye nyadhifa zao, kitu kinachotafutwa na wabunge.

Kwa nia ya kukufikishia taarifa hizi kwa wakati, jana imetulazimu kuchapa gazeti mchana, ila ulikuwapo uvumi kuwa Serikali inajiandaa kutoa taarifa au kufanya maamuzi magumu, hivyo hilo likitokea tutakujuvya katika toleo lijalo. Mhariri.