Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu kwa Usimamizi mzuri wa kukabiliana na Maafa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama wakati wa wasilisho lililohusu namna Serikali ilivyojipanga katika kukabiliana na maafa pamoja na mfumo wa usimamizi wa Uratibu wa maafa katika kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na Utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi wa Vituo vya utoaji huduma za matibabu kwa waraibu wa Dawa za kulevya nchini lililowasilishwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama leo Bungeni Jijini Dodoma.
Mwenyekiti huyo amesema Serikali ilifanya kazi kubwa nayakupongezwa kutokana na jitihada zilizofanyika kuhakikisha waathirika wa mafuriko katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanag mkoani Manyara wanaokolewa na kurejesha hali.
“Tunapongeza sana Uongozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kazi mliyofanya ni kubwa ya kuokoa maisha ya wananchi na mal zao licha ya baadhi yao kupoteza maisha kama kamati tunawapongeza sana,” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Dkt. Mhagama amesema, inatia moyo sana kuona Wizara ama idara inazozisimamia zinafanya kazi ambazo watanzania wanazitarajia kwa hiyo kamati nayo inajiskia kama ni sehemu ya hayo mafanikio makubwa yaliyopatikana.
“Maafa ni majanga lakini tunapokabiliana nayo na kuyafanyia kazi vizuri inatupa nguvu sasa, tunapenda tukupongeze Waziri Jenista Mhagama, Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi na Watendaji wako wote kwa moyo wa uzalendo mliouonyesha katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilipitia,” ameeleza Dkt. Mhagama.
Vilevile Kamati pia ilipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kukabilana na madawa ya kulevya kwa kazi nzuri inayofanya ya kujenga vituo vya Uraibu na kushauri kujengwa vituo zaidi kwa Mikoa ya kusini pamoja na kuendeleza mapambano ya uzalishaji na biashara ya Dawa za kulevya kama vile Bangi,Mirungi na dawa nyingine.
Akitoa maoni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Edward Olekaita Kisau, amefafanua kwamba namna Serikali ilivyokabiliana wakati wote wa maafa na baada ya maafa ili kuhakikisha inarejesha hali na shughuli kuendelea kama ilivyokuwa awali na janga la Hanang’ ni mfano mzuri unaoweza kuchukuliwa katika uratibu mzima wa masuala ya kukabiliana na majanga nchini.
Naye Mjumbe wa kamati hiyo Dkt Alice Kaijage akitoa maoni kuhusu wasilisho la Utekelezaji wa Mpango wa Ujenzi wa Vituo vya Utoaji wa Huduma za Matibabu kwa Waraibu wa Dawa za Kulevya nchini alibainisha kuwa ni wakati mzuri sasa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) kuongozewa fedha za maendeleo kwani kazi inayofanywa na mamlaka hiyo ni kubwa na kuleta matokeo chanya kwa Taifa.
Awali akiwasilisha taarifa hizo mbele ya kamati hiyo Waziri Mhagama amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia majukwaa mbalimbali kwa lengo la kuijengea uelewa na uwezo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kupunguza madhara yanayotokana na maafa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imeendelea kujenga uwezo wa usimamizi wa maafa kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na vifaa, Serikali imefanya manunuzi na kuratibu upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya msaada wakati wa dharura na kuvihifadhi katika maghala ya kuhifadhia vifaa vya misaada ya kibinadamu ili kuongeza uwezo wa nchi katika kukabiliana na maafa,” ameeleza Jenista.
Aidha waziri huyo alitoa wito kwa wananchi kutokudharau utabiri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwani mamlaka ina vifaa vinavyoendana na teknolojia ya kisasa ambapo utabiri wa hali ya hewa kwa wakati huu, umekuwa na una usahihi wa asilimia 85 mpaka 95.