Bunge la Ujerumani linalomaliza muda wake linatarajiwa kupitisha mpango mkubwa wa kuzuia ukomo wa serikali kukopa ambao umewasilishwa na vyama vitatu vya CDU/CSU na SPD vinavyotarajiwa kuunda serikali mpya ya mseto.

Friedrich Merz anayetazamiwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani anaupigia upatu mpango huo akitaka upitishwe na bunge la sasa, akihofia kwamba huenda ukapingwa na bunge lijalo litakaloanza vikao vyake mnamo Machi 25.

Mapema leo, Merz alisema kuwa sasa inabidi wajenge upya uwezo wao wa ulinzi kuanzia mwanzo.

”Kwa mkakati wa ulinzi na ununuzi unaoendeshwa na teknolojia, ufuatiliaji huru wa satelaiti wa Ulaya, droni na silaha na mifumo mingi ya kisasa ya ulinzi, na zaidi ya yote, kuwepo kwa maagizo ya kuaminika na yanayotabirika ambayo yanapaswa kuelekezwa kwa wazalishaji wa Ulaya wakati wowote inapowezekana.”

Mpango huo unaotarajiwa kupitishwa na wabunge unalenga kulegeza sheria za katiba na kuondoa ukomo wa kukopa na hivyo kuufufua uchumi wa Ujerumani ambao ndio mkubwa zaidi barani Ulaya.