Kwa namna mwenendo unavyoonekana katika Bunge, nashauri waheshimiwa wabunge wauzibe ule ufa namba tatu, ulioelezwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, unaotikisa Taifa letu. Ufa huo ni ule wa “Kuendesha mambo bila kujali sheria (Nyufa: uk. 14 ibara ya pili)”
Ikiwa Bunge ni chombo cha kutunga sheria na kinatengeneza na kanuni za kuendesha mambo ili upatikane utawala bora huku lenyewe halijali hizo kanuni, basi huo ni mfano mbaya sana. Wabunge kutohudhuria vikao ni kutojali sheria, wabunge kutotii kiti katika mijadala ni kutokujali sheria; wabunge kuzungumza bila kupewa ruhusa ni kutokujali sheria na ndiyo maana Mwalimu aliutaja huu kuwa ufa namba tatu na akawasihi Watanzania kuendesha nchi kwa kujali sheria za nchi.
Kwa vile kila mbunge amekula kiapo, ninaamini kujali sheria ni pamoja na kushika ahadi za kiapo kile cha ubunge na hivyo kujenga utawala bora hapa nchini. Katika kuhitimisha maoni yangu kuhusu mwelekeo wa Bunge letu la sasa, niliona vema nikumbushe tu juu ya umuhimu (priority) wa kuujenga ule ufa namba moja, wa kwanza kabisa aliotueleza Baba wa Taifa unaolitikisa sana Taifa letu.
Alisema, na mnukuu “ufa wa kwanza ni Muungano”. Ulipotikisika ufa mmoja mkubwa tuliouona ni katika Muungano (Nyufa uk. 9) Bunge lina wajumbe kutoka kila upande wa Muungano. Mimi niliposikia hotuba ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani akisema, Zanzibar imevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kuwa imejitoa katika Muungano, niliduwaa.
Baadaye nikamsikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali akikanusha hayo na kusisitiza kuwa hakuna kipengele cha Katiba ya Jamhuri kilichovunjwa, na ya kwamba Zanzibar ilikuwa bado ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nikatulia. Wasemaji wote wawili ni wasomi wa sheria na kwa lugha zao za utani wa kisheria huwa wanatambuana kama “Learned Brothers” nikaona mimi niwatolee uvivu wangu hapo hapo wakiwa bado bungeni.
Wanasheria wana tabia ya kuchombeza maneno ya hadaa ilimradi kuchanganya wengine. Kwa Kiingereza kutumia misamiati ya hadaa wanasema kutumia ‘symantics’. Lakini bungeni si mahali pake. Pale panatakiwa maelezo ya kawaida kabisa, kufafanua mada na kupata ufumbuzi wa matatizo ya Muungano wetu. Si kurejea vifungu vya sheria tu.
Sote tunajua maana ya Muungano. Upo muungano kati ya watu wawili – mume na mke, ndiyo ndoa; upo muungano wa vitu viwili au zaidi (kisayansi tunaita ‘mixture’) mseto na upo huo muungano wa nchi mbili au zaidi. Miungano yote hiyo tunaisema ni “physical unions” na wahusika hawabadiliki kimaumbile bali inakuwapo hali ya ukubaliano wa kufanya mambo fulani fulani kwa pamoja.
Laiti nchi zingeyeyuka wakati wa kuungana au wanadamu wangeyeyuka wanapofunga ndoa hapo kingetokea kitu kipya kabisa kisayansi kinachoitwa “compound”. Maadam, watu au nchi haziyeyuki ndipo tunaona Utanganyika unabakia katika vikabila vyao na Uzanzibari katika vyao.
Ni mithili ya chumvi inapoyeyuka katika maji, ladha ya chumvi na hali ya maji vinaonekana, lakini mchanganyiko ule unaitwa ‘saline’ si chumvi tena na wala si maji tena, lakini sifa zao zingalipo (every component retains its characteristics).
Wenzetu kule Marekani waliunda muungano wa viji-nchi vingi tu, tuite majimbo; lakini wao wanaita ‘states’. Walipoamua kuungana wazee waasisi wao walitoka majimbo 12 tu na walikuwa wajumbe 55 pekee. Hawa walikaa wakabuni muungano katika kikao kilichoitwa “The Constitutional Convention”. (Encyclopedia Britanika vol. 22 uk. 755 –756).
Baada ya kukubaliana ulipatikana muungano tunaojua kama Marekani ya leo (United States of America-USA) yenye jumla ya muungano wa nchi 51 hivi sasa. Hakuna watawala vijana wala mabunge yao kuuchokonoa eti waletewe mkataba hadharani na watu waulizwe kama wanauafiki au hapana.
Si Rais Barak Obama wala watangulizi wake akina Clinton na Bush wamediriki kuhoji Rais wa kwanza George Washington (1789-1797) na Makamu Rais wake John Adams (1797-1801) walikubaliana vipi! Sasa ule mkataba wa Muungano (Instrument of Union) wakiletewa kwani tafsiri waliyokuwa nayo wazee – Nyerere na Karume – sisi tunajua? Kama hatujui tutasemaje tuirekebishe?
Kule Uingereza wana muungano wa nchi nne – England, Scotland, Wales na North Ireland. Nchi hizi ziliungana kwa hiari na ridhaa ya wazee mwaka 1801 kwa sheria inayoitwa Act of Union pale Ireland ilipojiunga rasmi katika Muungano wa zile nchi tatu zilizoungana kabla (England na Wales ziliungana 1301; Scotland iliunganishwa 1707), hivyo muungano wa nchi zile nne za Uingereza unaitwa The United Kingdom of Great Britain and Ireland kwa kifupi UK tunayoijua siku hizi. (Encyclopedia Britanica Vol. 10 uk. 734).
Mbona Bunge la Uingereza au Scotland hawaubezi muungano wao huo? Akina Cameron wala hawahoji uhalali wake eti sasa waletewe bungeni ujadiliwe upya na wananchi waonyeshwe yale makubaliano ya miaka hiyo?
Haya ndiyo mambo Baba wa Taifa aliyoyasema “Watanganyika wakiwakataa Wazanzibari, basi kwa tendo la dhambi ile ya ‘usisi’ Tanganyika na ‘wao’ Wazanzibari, wakaukuza ‘usisi’ Tanganyika hapatakuwa na Tanganyika! Wachagga si wazawa” (Nyufa: uk. 12).”
Je, Bunge letu hili la sasa mnataka kutupeleka huko kwenye ufa huu wa mfarakano au mnataka kuuziba usiendelee? Kuna methali isemayo “Usipoziba ufa utajenga ukuta” je, mnataka kutufikisha huko kwenye kujenga ukuta? Ni vema waheshimiwa wabunge mkakazana kuuziba ufa huu wa Muungano ili sote tuishi kwa amani na usalama katika Jamhuri hii ya Muungano wa Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania, dumisha Uhuru na Umoja, Amen.
Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).