Wiki hii Bunge linaanza mjadala wa rasimu ya Katiba. Mjadala huu unafanyika siku chache baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba, kuwasilisha rasimu hiyo bungeni, na baadaye Rais Jakaya Kikwete naye akalihutubia Bunge. Hotuba mbili za wakubwa hawa ndizo zilizonifanya niandike makala ya leo.
Sitanii, leo tunaumiza vichwa lakini chimbuko la matatizo yote haya liko wazi, ni Rais Jakaya Kikwete. Ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inasema hivi: “Bila ya kuathiri kutumika kwa Katiba ya Zanzibar kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Tanzania Zanzibar yasiyo mambo ya Muungano, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba itakuwa batili.”
Ibara ya kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatoa tangazo la nchi. Inasema Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano. Zanzibar mwaka 2010 walifanya mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, Ibara ya kwanza ya Katiba ya Zanzibar sasa inasema Zanzibar ni nchi.
Huu ulikuwa ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Tanzania.
Kiwango cha ukiukwaji huu ni sawa na uasi au uhaini.
Aliyekuwa Rais wa Zanzibar wakati huo, Amani Abeid Karume, kwa kushirikiana na Makamu wa Kwanza wa Rais sasa, Maalim Seif Shariff Hamad, walimega madaraka ya Jamhuri na Rais wa Jamhuri. Hawa kwa jaribio hili walilolifanya walipaswa kukamatwa na kuwekwa ndani kuepusha wasiambukize wengine tabia hii ya uroho wa madaraka.
Kwa bahati mbaya, Wazanzibari hawa ‘walitest zali’ na Rais Kikwete akawaacha. Aliapa kuilinda Katiba yetu, Katiba imevunjwa akiwa madarakani, na yeye hajafanya lolote kuhakikisha anazuia uvunjifu huu. Wasiwasi ninaoupata, ikitokea watu wengine huko Rukwa, Tabora au Kagera nao wakaamua kuwa na Katiba yao, basi Kikwete inaelekea atawaacha nao watangaze nchi.
Nafahamu gharama ya kuandika maneno haya mazito, najua wengi wanaogopa kwa kuwa Rais Kikwete yuko madarakani, ila mimi woga huo sina. Nilipata kumuuliza swali hili pale Ikulu, akasema mabadiliko yaliyofanyika Zanzibar yamerejesha amani, ila hakujibu sehemu ya pili ya swali langu. Matokeo ya ama udhaifu au kutojali huko, ndiyo sasa kunatufikisha hapa.
Sitanii, ingawa mimi ni muumini wa ujio wa Serikali ya Tanganyika, nakubaliana na Rais Kikwete kwa kiasi kikubwa juu ya hotuba aliyoitoa bungeni Ijumaa iliyopita. Tanzania hii aina ya Muungano tulionao unaweza ukawa na matatizo ya hapa na pale, lakini tukiuvunja kwa pupa tutakuwa na matatizo makubwa zaidi. Gharama ya kuvunja Muungano huu kijamii inaweza kuwa kubwa kuliko kuendelea nao.
Binafsi ninachopinga ni idadi ya mambo ya Muungano. Ukiyaangalia yaliyopendekezwa, bila ardhi kuwa suala la Muungano, tutakuwa tunajenga ufa mkubwa ajabu. Wapo wanaosema haliwezi kutokea, ila ikitokea ikaundwa Serikali ya Tanganyika, amini usiamini lazima Tanganyika nayo itaiga mfano wa Zanzibar. Itatunga sheria yenye kutaka mtu anayemiliki ardhi Tanganyika awe Mtanganyika.
Sheria ya aina hii ikiishatungwa, Wazanzibari tunaoishi nao waliojenga Dar es Salaam hadi Nkasi, itabidi kwanza wote warudi nyumbani kisha warejee hapa kama wawekezaji. Sheria ya Zanzibar inasema mtu akikaa Zanzibar kwa miaka 15 anakuwa Mzanzibari, lakini tujiulize hivi kama mtu anataka kufanya biashara akitokea Tanganyika ina maana akae miaka 15 Zanzibar kwanza ndipo aruhusiwe kumiliki ardhi?
Katika kuungana ni lazima kila upande ukubali kupoteza kitu fulani. Hoja kwamba Zanzibar hakuna ardhi, nimepata kuandika hili na leo narudia kuwa sikubaliani nayo. Leo Dar es Salaam katika eneo la Posta au Kariakoo, hakuna ardhi ila kuna haki ya kumiliki ardhi. Matokeo yake, baadhi ya watu wanajikuta wakinunua hatua 20 kwa 20 kwa hadi Sh milioni 700.
Ninachosema ni kuwa Zanzibar inapaswa kutoa haki ya kumiliki ardhi kwa Watanzania wote bila kujali iwapo amekaa Zanzibar kwa miaka 15 au zaidi. Kwa kufanya hivyo, ikiwa mtu ana uwezo kifedha akitaka kumiliki ardhi Zanzibar atanunua kwa bei ya soko. Kisichokubalika duniani na mbinguni, ni huu unafiki wa Wazanzibari kuruhusiwa kumiliki ardhi Tanganyika bila masharti, ila Watanganyika wakawekewa vikwazo Zanzibar.
Nimesema hapo juu kwa kurejea ibara ya 64 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa matatizo yote tunayopata sasa yamechangiwa na Rais Kikwete. Ni matumaini yangu kama alivyopata ujasiri wa kutamka kuwa chama chake, pengine na yeye wanataka Serikali mbili, basi awe na ujasiri wa kuwaambia Wazanzibari waisome Katiba ya Tanzania kisha wapime kama bado wapo kwenye Muungano au la.
Kauli zinazotolewa kuwa Wazanzibari hawakubali, binafsi sizikubali. Inawezekana tunawafanyia unafiki Wazanzibari, hivyo tunaona aibu kuwaeleza ukweli. Hoja zenye mashiko kama hii ya ardhi, sioni ni kwa jinsi gani Wazanzibari wakielezwa hawawezi kuielewa na kuikubali. Ikiwa watashikilia msimamo wao, basi tusonge mbele, ila naamini kila mtu anajua nani atapata hasara zaidi.
Suala la mapato ya Serikali ya Muungano katika mfumo wa Serikali tatu linapaswa kuchunguzwa kwa kina. Ushuru unaotajwa, inaweza kufika mahala ikawa ngumu. Kwamba bandari zimilikiwe na Zanzibar na Tanganyika kisha zikusanye ushuru na kuipa Serikali ya Muungano, hili ni suala gumu. Inawezekana zikatoa taarifa kuwa watu wanagoma kulipa, na huo ndiyo utakaokuwa mwisho wa Serikali ya Tanzania.
Sitanii, kichwa cha makala haya kinasema Bunge la Katiba livunjwe. Nimefikia pendekezo hili baada ya kubaini kuwa bunge hili lina walakini. Maelekezo mahususi yaliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete bungeni, ndiyo yaliyonishawishi kufikia wazo hili. Kumbe CCM tayari wameshaamua kuwa wanataka kuendelea na Serikali mbili.
Kinachonishangaza; ikiwa waliyajua haya kuwa wanataka Zanzibar wapate mafuta yao, wanataka gesi lisiwe suala la Muungano na kwamba wanataka ziwepo Serikali mbili, ilikuwapo sababu gani ya kupoteza fedha za umma kuunda Tume, kisha Bunge la Katiba, ambapo marekebisho haya yangeweza kufanywa kwa utaratibu wa kawaida tu?
Kama hivyo ndivyo, na Watanzania karibu sote sasa tunafahamu aina ya Katiba itakayotungwa, je, kuna sababu ya kuendelea na bunge la aina hii? Kwa kuwa Rais Kikwete amekwishaweka wazi, na kishindo cha kushangilia Serikali mbili kilivyoonekana bungeni, basi ni wazi kuwa tusitarajie jipya.
Hapa ninachoona, tumechezewa mchezo wa karata mbili. Rais Kikwete na wenzake waliona moto wa kudai Katiba mpya unazidi kuwa mkali na pengine unawapa umaarufu wapinzani, hivyo wakaamua ‘kuwapiga bao la kisingino’ kwa kutangaza kuwa CCM sasa watatunga Katiba mpya. Walijua fika kuwa hakuna kitu kama hicho, ila wakaamua kuuzuga umma.
Kama ni mkakati umewasaidia. Wameweza kulipumbaza Taifa kwa miaka miwili, harakati zilizokuwa zinafanywa na upinzani kama M4C na Sangara zikasitishwa. Kwa miaka miwili na zaidi nchi ikajikita katika mjadala hewa wa Katiba. Leo tupo mwaka 2014 kampeni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa utaanza punde, Katiba tutaiweka pembeni.
Tukimaliza uchaguzi wa Serikali za Mitaa itakuwa imetimu 2015, mbio ndefu za kugombea urais zinaanza, na hapo huo ndiyo utakaokuwa mwisho wa kuzungumzia Katiba mpya. Tutaanza kusikia ahadi hewa, majina mabaya na mazuri, kisha tukimaliza kumchagua huyo ajaye tunakwenda 2016. Wakubwa baada ya hapo watapanga mkakati mpya.
Sitanii, nchi yetu ni bingwa wa uchaguzi sasa. Tukimaliza mwakani uchaguzi, zinaanza kampeni za mwaka 2020, baada ya hapo 2025 mambo yanakwenda hivyo hadi mwaka 2050. Maisha yetu yatakuwa ni kampeni, viini macho kisha tunaendelea na maisha kama kawaida. Posho ya Sh 300,000 wanazolipwa wajumbe kila siku bora zikaelekezwa kwenye madawati.
Hakuna tija huko. Maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM yatatekelezwa bila kupindishwa hata chembe. Ikumbukwe CCM wanapigia chapuo kura ya wazi, sasa ndipo ninapozidi kuelewa maana yao. Wanataka kubaini katika umoja wao nani aliyepinga hoja za chama kisha wamshughulikie.
Mwelekeo ninaouona wala hatupaswi kupoteza muda. Bora Bunge hili livunjwe, tuendelee na mambo mengine maana hatutarajii jipya kutokana na bunge hili.