Kwa wiki kadhaa tumekuwa tukiandika habari zinazohusu ufisadi, upendeleo na matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Ofisi ya Bunge.
Habari hizo zilipoanza kuchapishwa katika JAMHURI, haraka haraka Bunge likajitokeza kukanusha, ingawa kimsingi hakuna kilichokanushwa zaidi ya kuthibitisha kile tulichokiandika.
Kuna upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watuhumiwa wakuu kwenye sakata hili. Nao ni ule wa kujaribu “kuwatafuta wachawi”, huku zikiingizwa hisia za kisiasa.
Tunapenda kuwahakikishia watumishi hao wa Bunge na wasomaji wetu kwamba haya tunayoyaandika kuhusu Bunge ni sahihi, na tena hayana chembe yoyote ya kisiasa wala husuda. Tunayaandika haya kwa kuamini kuwa Bunge ni taasisi nyeti inayostahili kuongozwa na watu waadilifu.
Tunayafanya haya kwa kuitikia mwito wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa vyombo vya habari wa kuisaidia Serikali kujua wapi kuna ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka, ili hatua zichukuliwe kwa manufaa na ustawi wa nchi yetu.
Toleo lililopita tuliandika matumizi ya Sh bilioni 6 zinazolipwa kwa kampuni ya bima ya afya kwa wabunge na familia zao. Shilingi bilioni 6 ambazo ni za umma ni fedha nyingi mno ambazo haziwezi kutolewa kirahisi namna hiyo halafu Watanzania wakanyamaza tu. Tuna mfano wa kampuni moja binafsi ambayo inatumia Sh milioni 72 kwa mwaka kuwalipia bima ya afya wafanyakazi wake zaidi ya 200 kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Uongozi wa Bunge unatambua kuwa NHIF kuna huduma hii kwa bei nzuri kabisa, umekataa kujiunga huko. Umekataa kwa sababu unajua mlolongo wa kupata mrejesho (mgawo) wa fedha zilizokwishaingia kwenye Mfuko huo ambao ni mali ya Serikali; si mwepesi ikilinganishwa na kwenye bima za mashirika binafsi. Kama si hivyo, kuna sababu gani chombo kama Bunge kukataa kujiunga NHIF?
Badala ya “kutafuta wachawi”, ni vema Bunge na mamlaka zinazoitakia mema nchi yetu zikabaini chanzo cha matumizi haya ya fedha na kuamua njia sahihi ya kudhibiti mwanya huo na mingine mingi ndani ya chombo hicho.
Tunayasema haya kwa sababu fedha zinazotumiwa vibaya kwenye bima na kulipana masurufu manono kupindukia ndani ya Bunge ni za Watanzania. Kwa kuwa mihimili ya Serikali na Mahakama imeshachunguzwa mno kwa matumizi mabaya ya fedha za umma, tunaamini huu ndiyo wakati sahihi wa kulichunguza Bunge na wahusika hawana budi wachukuliwe hatua stahiki.