Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kupitia Bunge Marathon 2025 Bunge limepanga kukusanya Sh bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Wavulana ya Bunge Jijini Dodoma.
Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 12,2025 wakati akizungumza katika mbio za Bunge Marathoni 2025 katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Amesema mara baada ya kukamilisha kwa ujenzi wa shule ya Wanawake ya Bunge kwa sasa wamepanga kujenga shule ya Wanaume katika eneo la Kikombo Jijini hapa.
Amesema shule hiyo itakuwa na madarasa ya kutosha,mabweni ya wanaume,Maabara,nyumba za walimu pamoja na viwanja vya Michezo.
“Nataka nioneshe faraja yangu baada ya kuona washiriki wa mbio hizi wa rika mbalimbali kukimbia mbio hizi hawa ni wanamichezo huu ni ubunifu mzuri hasa katika kujenga afya,”amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kwa upande wake,Spika wa Bunge,Dk Tulia Ackson amesema hiyo ndio marathoni pekee ya wananchi kwa maana inawakusanya Wabunge kutoka majimbo 264.

Spika Tulia amewashukuru wadau kwa kuweza kuwaunga mkono kwenye ujenzi wa shule ya Wavulana kidato cha Tano na sita.
“Tunatamani kuwa mfano mzuri na shule yetu ipo vizuri na tutajenga hapa Dodoma ili ipate nafasi ya kufuatiliwa na Wabunge kuonesha tunawajali wote wakike na wa kiume,”amesema Spika Tulia.
Amesema sababu ya uwepo katika mbio hizo ni kuiweka miili yao vizuri pamoja na kufanya mazoezi kwa kujali afya zao.

Mwenyekiti wa Bunge Marathon 2025,Festo Sanga amesema sababu ya uwepo wa mbio hizo ni kutokana na maono ya Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kwamba kuwe na jambo hilo.
“Mbio hizi ni za hisani zimelenga kujenga shule ya Wavulana ya Bunge Boys mara baada ya kujenga shule ya Wanawake,”amesema Sanga ambaye ni Mbunge wa Makete.
Amesema zaidi ya wakimbiaji 5000 wamejitokeza kukimbia mbio hizo huku akilipongeza Bunge kwa kuweza kuratibu zoezi hilo vizuri.