Tunashukuru Ofisi ya Bunge imeendelea kuwathibitishia Watanzania kuwa ina matatizo ya kiutendaji.

Safari hii Mkurugenzi wa Ofisi ya Spika, Said Yakub, ambaye kimsingi si Msemaji wa Ofisi ya Bunge, amekiri kuwa kuna watoto wa vigogo, ingawa anadai taratibu zimefuatwa kuwaajiri. Sisi tunasema hazikufuatwa.

Ameshindwa kutoa majibu ya msingi ambayo msemaji wa ofisi hiyo, Owen Mwandumbya, pia alishindwa kuyatoa.

Pamoja na mambo mengine, kama taratibu zilifuatwa je, ni lini matangazo ya kazi yalitoka na kwa vyombo gani vya habari? Matangazo hayo yalitoka na kudumu kwa muda gani? Kanuni za uendeshaji wa shughuli za Sekretarieti ya Ajira katika utumishi wa umma zinahitaji matangazo yafanyike kwenye vyombo mbalimbali kwa siku zisizopungua 14 (rejea sehemu ya nne Kifungu 9 kifungu kidogo cha 3 kwa njia ya posta). Je, waombaji walifanya hivyo? 

Waliofanya usaili ni wangapi na kwa siku zipi? Hii ni muhimu kwa sababu habari za uhakika ni kuwa kuna wengine hata usaili hawakufanya. Walitua kutoa Afrika Kusini na Uingereza na moja kwa moja kuingia kazini.

Je, scorecard za usaili zinaweza kupatikana kuthibitisha hayo yanayosemwa na Yakub ili kuonesha waliostahili ndiyo walioitwa kazini. Ukweli ni kwamba yeye mwenyewe Yakub ni mmoja wa wanufaika wa utaratibu huo ambako mdogo wake ni mmoja wa walioajiriwa katika mazingira tata ambaye kwa sasa ni Katibu Msaidizi wa Bunge Daraja la Pili.

Pia, katika unufaikaji huo hata Mkurugenzi wa Huduma za Bunge, Bwana Athuman Kwikima  ambaye yeye alimuingiza shemeji yake mdogo wa mke wake Zainab Mkamba, ambaye naye kwa sasa ni Katibu Msaidizi wa Bunge Daraja la Pili.

Mmoja wa watoto wa vigogo, Victor Mhagama alifanya usaili mara mbili Idara ya Hansard na kushindwa, lakini alipewa ajira Idara ya Kamati za Bunge bila kufanya usaili katika idara hiyo.

Kuhusu muundo wa Utumishi wa Bunge ambako Yakub anadai uliasisiwa na Spika Samuel Sitta; wa Bunge la Tisa, hoja haikuwa ni lini muundo uliasisiwa, bali ni ukiukwaji wa taratibu wa kutoshirikisha wafanyakazi kwa kupitia vyombo vyao halali ikiwamo Baraza la Wafanyakazi na Menejimenti. Pamoja na Yakub kukiri muundo huu ulikataliwa na Utumishi ni ukweli usiopingika taratibu hazikufuatwa na pengine ndo sababu kuu mpaka sasa Utumishi hawajaupitisha.

Yakub kukiri kuwapo kwa Bwana Mpanda ambaye ni Katibu wa Katibu wa Bunge ambaye pia alipewa nafasi ya Ukurugenzi katika mazingira tata, kumbe hata Yakub ni mmoja ya watumishi walioingia kwenye utumishi wa umma katika kipindi kifupi sana na kupanda vyeo kwa haraka haraka. Aliajiriwa 2009 kwa mara ya kwanza kwenye utumishi wa umma kama Katibu Msaidizi Daraja la Pili, lakini ndani ya miaka mitatu alipewa nafasi Mkurugenzi Msaidizi, na hatimaye miaka mitatu mbele akawa Mkurugenzi kamili ambako ni kinyume kabisa na watumishi wengine ambao hupitia madaraja mbalimbali kama Daraja la Kwanza, Senior na Principal ambapo kila daraja mtumishi hutumia kati ya miaka minne hadi saba kupanda.

Kuhusu ununuzi wa magari, PPRA wanazo taratibu za zinazotumika iwapo serikali imeagiza magari inapokuta yaliyotakiwa hayapo. Haya hayakufuatwa na Bunge.

Yakub amethibitisha ambavyo Ofisi ya Bunge ilivyofanya uamuzi mbaya kwa kuitia Serikali hasara ya Sh bilioni 3 kwa mkataba kati ya Jubilee Insurance na Ofisi ya Bunge (2014/2015) bila kutoa sababu kwa nini walijitoa baada ya mwaka mmoja kama kweli Jubilee walikuwa ni watoa huduma bora zaidi ya NHIF.

Mshenga Astra Insurance Broker naye alilipwa Sh zaidi ya milioni 200 kwa ajili kufanikisha mpango huo kama washauri. Kama sasa NHIF wanaweza kutoa huduma hiyo kwa bei nafuu kwa nini huduma hiyo ilipewa kampuni binafsi  kwa gharama ya juu sana wakati mpaka sasa sheria hiyo bado haijarekebishwa?

Yacob anathibitisha kuwapo kwa posho ya Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa siku. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora watueleze kama huo utaratibu upo sawa iwapo viongozi wanasafiri kwenda nchi zenye saa tofauti na sisi wasaidizi wanaobaki hulipwa hivyo.

 

Bunge kuchangia Sh bilioni 6

Aprili, mwaka huu Katibu wa Bunge akiwa pamoja na Naibu Spika walimkabidhi Rais John Magufuli mfano wa hundi ya Sh bilioni 6 kama savings kutoka Mfuko wa Ofisi ya Bunge.

Kwamba, Ofisi imebana matumizi na hivyo kuchangia juhudi za Rais wetu katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Ni jambo jema kabisa! Lakini kwa nini Katibu wa Bunge anamdanganya Rais na kutaka kujikosha aonekane kweli anamuunga mkono Rais katika juhudi zake za kumwinua Mtanzania masikini ilhali hafanyi hivyo kwa vitendo?

Ni savings gani ambazo Ofisi ya Bunge ilifanya baada ya kuvunjwa kwa Bunge la Kumi? Katibu wa Bunge awe mkweli, amweleze Rais hizo fedha zimetoka wapi! Wote ni mashahidi kuwa baada ya Bunge la Kumi kuvunjwa ndipo yaliibuka matengenezo, ukarabati, kubadilisha samani, safari za kukata na shoka za viongozi wa Bunge pamoja na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge iliyopita na wateule wachache kulipana posho za kufuru kwa kazi ambazo zingeweza kufanyika katika muda wa kazi wa kawaida.

Wakati kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiendelea, viongozi wa Bunge walikuwa hawafahamu hatima yao baada ya uchaguzi kama watakuwapo au  la! Kilichofanyika ni kukomba kila kitu! Hata uchaguzi unaisha ofisi haikuwa na fedha kabisa! Sasa hizo savings zilitoka wapi?

Aprili 28, mwaka huu Ofisi ya Bunge ilipopokea fedha kutoka Hazina (Exchequer ya Sh 13,537,890,000.

Fedha hizo zilitolewa kwa rejea Na. EB/AG/159/15/1290)  ambazo kimsingi ilikuwa ni kwa ajili ya Bunge la Bajeti lililoanza wiki moja baadaye. Ndipo Rais akapewa hundi kwa maelezo ya Bunge limefanya savings na kuziwasilisha fedha hizo.

Kwa hiyo fedha zilizowasilishwa yaani Sh bilioni 6 mnamo Mei 4, mwaka huu zilimetokana na kubana matumizi ya sasa yaani wakati huu na si mwaka jana, maana kabla ya Aprili 28, mwaka huu akaunti ya Bunge ilikuwa na Sh milioni 700 tu!

 

Madeni ya Bunge

 Mbaya zaidi, Ofisi ya Bunge ina madeni mengi yasiyopungua Sh bilioni 7.8. Baadhi ya wanaodai ni CRJE wanaodai Sh 912,399,033.60; wamelipwa Sh 257,200,000. Bado wanadai Sh 655,199,033.60.

Jaffrey Industries wanadai Sh 1,025,448,320. Wamelipwa Sh 402,335,307.50 bado wanadai Sh 623,113,012.50. Haya ni malipo kwa huduma za meza. Hao hao Jaffery Industries wanadai Euro 364,066.50 ambazo zilizolipwa ni Sh 512,724,160 na kubaki deni la Sh 379,238,838.50.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanadai Sh 446,340,478.50 ambako zilizokwishalipwa ni Sh 322,348,128.20. Bado wanadai Sh 123,992,350.30.

Kuna msururu mrefu sana wa madeni hadi Magereza Tanzania. Unajiuliza, hivi inawezekana vipi utoe Sh bilioni 6 ukisema ni baada ya saving, ilhali ukiwa na madeni makubwa kiasi hiki?

Juni, mwaka huu Bunge lilishindwa kulipa posho za wabunge ili kuokoa jahazi. Zikachukuliwa Sh bilioni 2 za Development Fund na kulipa kulipa posho hizo! Tangu wakati huo shughuli zote zimesimama zikiwamo za paa la Ukumbi wa Bunge.

Kwa leo niishie hapa, lakini ikitakikana, basi tutaendelea kutoa mengine makubwa kuliko haya.