*Zimeletwa na Wizara ya Maliasili
*TRA wakomaa wakidai kodi yao
*JWTZ waliliwa wadhibiti majangili
*Tembo kutoweka baada ya miaka 7
Wakati majangili wakielekea kumaliza wanyamapori nchini, Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imezuia shehena ya bunduki bandarini zilizoagizwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kuimarisha Kikosi Dhidi ya Ujangili.
Hayo yalibainishwa jana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa 2012/2013 pamoja na maoni ya Kamati hiyo kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2013/2014. Taarifa hiyo ilisomwa na Mwenyekiti wa Kamati, James Lembeli.
“Ni jambo la kushangaza kwani pamoja na wanyamapori ambao ni mali ya Serikali kuingizia Taifa pato kubwa, bado taasisi kama TRA haioni wala kutambua jitihada za mkono mwingine wa Serikali za kuokoa rasilimali hii ya Taifa inayoendelea kupotea siku hadi siku.
“Kwa lugha nyingine, TRA kuendelea kushikilia silaha hizo kwa kigezo cha fedha ni kushawishi majangili yaendelee kuteketeza tembo wa Taifa hili. Kamati inaishauri na kuitaka Serikali kuruhusu mara moja silaha hizo kuondolewa bandarini japo kwa masharti,” imesema Kamati hiyo.
Kamati ilisema idadi ya askari wanyamapori waliopo sasa ni ndogo mno kukidhi mahitaji na changamoto zilizopo. Alitoa mfano wa Pori la Akiba la Rukwa/Lukwati/Lwafi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 9,568.26 kuwa lina watumishi 45 pekee.
“Hali ni mbaya katika mapori karibu yote ya akiba ikiwa ni pamoja na Pori la Akiba la Selous ambalo lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 likiwa na watumishi wasiozidi 250,” imesema Kamati.
Kamati imesema ili kurejesha hali ya kawaida katika mapori, Serikali inatakiwa kuajiri askari wa wanyamapori wasiopungua 1,000. Pamoja na kuongeza askari na vitendea kazi, Kamati ya Bunge imeshauri Serikali kufanya operesheni maalumu kama ile ya Operesheni Uhai ambayo ilimaliza kabisa ujangili kwa miaka 10.
Ujangili wa tembo
Kamati ya Kudumu ya Bunge imesema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni janga la kitaifa. “Ni ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa kimataifa zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka (TAWIRI 2011).
“Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutokana TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.
“Endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara moja, ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka saba ijayo,” imeonya Kamati.
Kamati hiyo imeongeza kusema, “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo. Kinachosikitisha ni kwamba Wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete iliyoitaka Wizara kuomba msaada kwake kama tatizo la ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni hujuma inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara ambao wamepuuza kauli ya Mheshimiwa Rais.”
Kamati imeshauri Serikali kuendesha Operesheni Uhai kwa nchi nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia imependekeza Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu kali kwa watu wote watakaothibitika kuhusika na ujangili, hasa wa tembo.
Wapinzani wataka JWTZ wingie kazini
Hali ya ujangili inayolitikisa Bunge imeifanya Kambi ya Upinzani iitake Serikali kulishirikisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika ulinzi wa wanyamapori.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Peter Msigwa, alisema mapendekezo ya kutumiwa kwa JWTZ yanatokana na ukweli kwamba polisi na mamlaka ya hifadhi kulemewa na majangili.
Kambi hiyo, kama ilivyo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge, imependekeza Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho ili adhabu kali itolewe kwa watu wanaotiwa hatiani kwa ujangili.