*Zakutwa kwa msaidizi wake, ahukumiwa miaka miwili
*Mwenyewe atoa shutuma nzito bungeni dhidi ya polisi
Bunduki tatu za Mbunge wa Tunduru Kusini, Mtutura Mtutura, zimekamatwa kwa matukio ya ujangili katika Pori la Selous- Niassa, lililopo Tunduru -mpakani kwa Tanzania na Msumbiji.
Silaha hizo zilikamatwa zikiwa na msaidizi wa Mbunge huyo aliyetajwa kwa jina moja la Nakale ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Chiungo, Tarafa ya Namasakata wilayani Tunduru. Mahakama ya Wilaya ya Tunduru imemhukumu kifungo cha nje cha miaka miwili.
Ametakiwa awe anaripoti Kituo Kikuu cha Polisi Wilaya ya Tunduru kila mwisho wa mwezi. Polisi imethibitisha kuwa bunduki hizo zinaendelea kushikiliwa na Jeshi hilo.
Operesheni iliendeshwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro na Kamanda wa Kikosi dhidi ya Ujangili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Venance Tossi. Katika ushahidi wake mahakamani, Chiungo alikiri kuwa bunduki hizo ni mali ya Mtutura.
Bado kuna wingu limetanda juu ya hatua ya polisi kushindwa kumshitaki Mtutura ambaye bunduki zake zimethibitika mahakamani kutumika kwenye ujangili wa tembo.
Kumekuwapo madai kwamba silaha za mbunge huyo zimekuwa zikitumika katika matukio mengi ya ujangili, hasa wa tembo.
Mara kadhaa imeelezwa na wadau mbalimbali kwamba mtandao wa ujangili unawahusishwa watu wengi, wakiwamo wanasiasa.
Aprili 30, mwaka huu, Mtutura akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii na alishutumu Operesheni hiyo, akisema iliendeshwa kibabe, na kwamba kuna watu walioshitakiwa na kuhukumiwa kifungo cha nje bila kupewa fursa ya kujitetea. Hakusema kama bunduki zake ni miongoni mwa zilizokamatwa kwa kuhusishwa na ujangili wa tembo.
Ufuatao ni mchango wa mbunge huyo neno kwa neno kama alivyoutoa bungeno Aprili 30, mwaka huu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, lakini ili nisisahu mwishoni naomba nitamke tu mwanzoni kabisa kwamba nasikitika kuwa Mbunge wa kwanza ambaye siungi kabisa mkono hoja hii iliyopo mezani mpaka pale Serikali itakapotoa ufafanuzi juu ya yale masuala yote yaliyojiri katika Jimbo langu la Tunduru Kusini na Kaskazini kwa ujumla wke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Maliasili ilifanya Operseheni ya Malihai mwezi Novemba 2012, katika operesheni ile kwa kiwango kikubwa ilikuwa ni uvunjifu wa haki za haki za binadamu na kulikuwa na kutokuwa na utekelezaji wa utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu imetamka wazi rasmi kwamba mtu hawezi kuhukumiwa bila kufikishwa katika vyombo vya kutafsiri sheria ambayo ni Mahakama na vyombo vile vitoe fursa ya mtu yule kuweza kujitetea. Lakini operesheni hii haikuendeshwa katika misingi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika operesheni ile yalitolewa matangazo katika vijiji mbalimbali kwamba kila anayemiliki bunduki aiwasilishe bunduki ile ili iweze kukaguliwa. Wananchi kwa kuheshimu sheria na mamlaka zilizopo mbele yao walikubali na wakazifikisha bunduki zile ili ziweze kukaguliwa.
Lakini cha kushangaza kila aliyepeleka bunduki ile kwenda kukagulisha alisainishwa kwamba bunduki hii unaikabidhi Serikali na yeye mwenyewe kuwekwa mahabusu na matokeo yake anapelekwa mahakamani na alipofikishwa mahakamani hakupewa hata fursa ya kujitetea, anahukumiwa kwamba atumikie kifungo miaka miwili nje ya jela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya wananchi 200 sasa hivi wanatumikia kifungo cha nje ilihali hawakupata fursa hata dakika moja ya kujitetea. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atafute muda aje Tunduru, najua alifika Tunduru, lakini alidanganywa na Kamanda ambaye alikuwa anaongoza kikosi kile ambaye ni Kamanda Tossi.
Alimdanganya kwamba amekusanya bunduki zaidi ya 300 za majangili, ilihali bunduki zile wananchi wamezipeleka wenyewe kwa mikono yao ili zikakaguliwe. Matokeo yake bunduki zile zikawa confiscated, zimekamatwa na Serikali na athari kubwa sasa hivi inatokea kwa wananchi wa Tunduru. Wananchi wengi sasa hivi wameishauawa kwa tembo, mazao yao mengi sana yameishaliwa, vijiji vingi mwaka huu vitakumbwa na baa la njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii haiwezi kuvumiliwa. Nashukuru nilipozungumza na Mheshimiwa Waziri ameonesha utayari wake wa kuja Tunduru na kufanya kazi hiyo ya tathmini ili kuweza kujua nini kilichojiri katika eneo lile la Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, wamiliki hawa wameniandikia barua mbalimbali wakileta malalamiko. Kitu cha kushangaza zaidi imefikia hata wanaomiliki bunduki za kujilinda wenyewe bastola nao zimechukuliwa. Sasa sielewi kama bastola nayo inaweza ikaua tembo ambaye wao wanamkusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache tu nitasoma baadhi ya wananchi ambao wameniletea barua zao kuilalamikia Serikali juu ya vitendo vibaya vilivyofanywa na kikosi kile kinachoongozwa na Kamanda Tossi. Mmoja wao ni Hashim Ndeka, Rajab Ali Tumu, Hausi Hakimu Ndalamila, Gasi Mhamed Gasi, Shaibu Musa Chande, Omari Rajab Shamri na Ahmed Khalifa Mushangama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni baadhi tu ya Watanzania wachache ambao wamedhulumiwa nafsi zao, wamefungwa kifungo cha nje bila kupata fursa ya kujitetea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nilipouliza swali la nyongeza mwaka jana katika Wizara hii kwamba kuna baadhi ya wananchi wa Tunduru wanapigwa, wananyang’anywa mali zao na hata wengine ambao wamekwenda kuvua samaki kwa ajili ya kitoweo wanadhalilishwa, Naibu Waziri kwa masikitiko makubwa kutokana na majibu ambayo amepewa na wataalamu kutoka Tunduru alisema kwamba hakuna mwananchi yeyote ambaye amewahi kufanyiwa vitendo hivyo.
Nikamuuliza je, endapo kutatokea ushahidi utakuwa tayari kuwajibika? Alichosema ni kwamba, niko tayari kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Mbunge na ikibidi niende Tunduru nikajionee mwenyewe. Kwa masikitiko makubwa mpaka leo hajafika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache tu nimpe taarifa kama ifuatavyo; tumekusanya orodha ya watu wachache tu ambao wamepigwa, wamevunjwa mikono na wengine wameuawa na operesheni hizi mbalimbali ambazo zinafanywa katika eneo letu la Tunduru Kusini.
Katika Kijiji cha Michesela kuna wananchi zaidi ya 16, na waliopigwa mpaka kufa ni wawili Mohammed Hesabu kwa jina la a.k.a. Nangukule, Hausi Twalibu jina la utani anaitwa Mchicha. Halafu kijiji cha Meyamtwaru ni wananchi 16 na mmojawapo aliuawa kwa kupigwa anaitwa Jafari Amir Chikombola. Kijiji cha Kiumbo ni watu 10 ambao walipigwa na kunyang’anywa mali zao. Kijiji cha Amani ni watu 12 na mmojawapo alipigwa mpaka kufa ambaye anaitwa Hussein Salum Pasietu. Kijiji cha Nasia ni watu watano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakabidhi majina haya na baadhi ya barua ambazo nimekabidhiwa na wananchi hawa ili Waziri aweze kuzifanyia kazi.
Wananchi wamtuhumu
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Jamhuri, walisema historia ya Mtutura inatiliwa shaka na wana wasiwasi kuwa aligombea ubunge kupata kichaka cha kujifichia. Wanasema ndugu yake alipotoa taarifa kuwa bunduki ni zake, wakati anajitetea mahakamani yeye alifanya mbinu na kuhakikisha anafungwa kifungo cha nje.
Pia wanasema mchango alioutoa bungeni, unalenga kumtisha Waziri afanye uamuzi bila kwenda Tunduru, lakini akienda atashangaa kutokuta makaburi ya hao watu wanaotajwa kuwa wameuawa.
Kwa upande wake, Mtutura alifanya kila mbinu kulikwepa gazeti la JAMHURI kwenye viwanja vya Bunge Dodoma na hata alipopelekewa ujumbe wa maandishi kupitia kwa maafisa wa Bunge hakujibu. Pia alipopigiwa simu mwishoni mwa wiki, simu yake iliita kisha akawa haipokei.
Mwandishi wetu alimtumia ujumbe wa maandishi, ambao unaonyesha ulimfikia lakini hakujibu ujumbe huo pamoja na kuweka wazi tuhuma zinazomkabili.