pg-1Watu kadhaa, wakiwamo wenye nasaba na Mbunge wa Mbarali, mkoani Mbeya, Haroon Mulla (CCM), wamekamatwa katika operesheni maalumu wakituhumiwa kujihusisha na ujangili.

Katika operesheni hiyo, inayoongozwa na kikosi kazi kinachovishirikisha vikosi vya ulinzi na usalama, bunduki 13 za aina mbalimbali zimekamatwa kwa ndugu zake Mulla. Mtoto wa Mulla, anayetajwa kwa jina la Fahad, ni miongoni mwa waliokamatwa na idadi kubwa ya bunduki. Bunduki zilizokamatwa zimetajwa kuwa ni riffle na nyingine za kivita; pamoja na risasi zake.

Mtuhumiwa mwingine ambaye ni ndugu wa Mulla, ametajwa kwa jina moja la Pirmohamed. Jina hilo ni la ukoo.

Vyanzo vya habari vimeiambia JAMHURI kuwa silaha hizo zimekamatwa maeneo mbalimbali, miongoni mwao zikifukuliwa ardhini katika makazi ya wanaukoo hao.

Zinadaiwa kutumiwa katika matukio mbalimbali ya ujangili likiwamo la hivi karibuni ambalo mmoja wa wanaukoo hao alikamatwa akiwa na nyara za Serikali. Katika tukio hilo lililotokea takribani wiki mbili zilizopita, Mahakama mkoani Mbeya ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Sh milioni 137. Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo na hivyo kumwezesha kunusurika na kifungo cha miaka 20 jela. 

Silaha zilizokamatwa zinadaiwa kutumika kuua wanyamapori katika mapori kadhaa nchini, lakini matukio mengi yakiwa yanafanywa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyoko katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Ruaha ndiyo hifadhi kubwa nchini, ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 20,300. Inafuatiwa na Serengeti yenye ukubwa wa wastani wa kilometa za mraba 14,000.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi, ameithibitishia JAMHURI kuwa kazi ya kuwasaka na kuwakamata watuhumiwa wa ujangili inaendelea vizuri.

“Ingawa sijapata ripoti kamili ya watuhumiwa waliokamatwa hadi sasa, nakuhakikishia kuwa kazi inakwenda vizuri kabisa.

“Hii kazi siyo Mbarali tu, bali ni maeneo mbalimbali nchini. Tusubiri ripoti ya Polisi kwa sababu wao ndiyo wenye ‘mandate’ (mamlaka) ya kulizungumzia suala hili. Shughuli zinaendelea kama kawaida,” amesema Meja Jenerali Milanzi.

Ameulizwa juu ya kukamatwa kwa ‘Mpemba’ baada ya kuwapo taarifa kwamba aliyekamatwa si ‘Mpemba’ halisi; na kwamba mhusika mwenyewe kakimbilia nje ya nchi.

“Si kweli. Mpemba amekamatwa. Hapa hakuna pa kukimbilia, Rais ‘katangaza vita’ dhidi ya ujangili, kwa hiyo hakuna mahali anapoweza kukimbilia mtuhumiwa tukashindwa kufika kumkamata,” amesema.

Kasi ya mapambano dhidi ya ujangili imekolezwa na agizo la Rais John Magufuli alipozuru Wizara ya Maliasili na Utalii kumshuhudia ‘Mpemba’ aliyekamatwa akiwa na nyara za Serikali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari, amesita kuingia kwenye undani wa kukamatwa kwa kina Mulla, akijitetea kwa kusema yeye si msemaji wa kikosi kazi. Anasema kikosi hicho kimeundwa nje ya eneo lake la kazi.

“Hiyo ni kazi maalumu ya kitaifa, hivyo wapo watu maalumu wanaohusika kuitolea taarifa, mimi siwezi kabisa kuzungumzia kikosi hicho na kazi yao,” amesema SACP Kidavashari.

Mkuu wa Operesheni za Polisi Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, DCP Jackson Nyambabe, ameulizwa na JAMHURI na kusema kuwa taarifa hizo zinaweza kutolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Mkomangwa.

Kaimu DCI Mkomangwa ameulizwa na majibu yake yakawa kwamba, kutokana na ugeni wake katika ofisi hiyo, hana taarifa zozote za kukamatwa kwa bunduki hizo.

“Sina muda mrefu ofisi hii, mimi bado mgeni. Suala hilo linashughulikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, wanaweza kukwambia kinachoendelea huko. Lakini ingekuwa vyema ukawasiliana na RPC wa Mbeya maana ni eneo lake la kazi; anajua kinachoendelea,” amesema.

Mbunge wa Mbarali, Mulla, ameombwa na JAMHURI kutoa ufafanuzi wa tuhuma zinazomgusa yeye na familia yake, lakini amesema asingependa kuzungumzia suala hilo kutokana na kuwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Alipoulizwa inakuwaje familia yake inaelezwa kumiliki kiasi hicho cha bunduki na kujihusisha na ujangili, akasisitiza kuwa kuna utaratibu unaochukuliwa pamoja na baadhi ya vitu kufanyika, hivyo asingependa kuingilia utaratibu huo kwa kuzungumza jambo lolote.

“Naomba nisiingilie yanayoendelea kufanyika, na kwa sababu suala hili lipo mikononi mwa vyombo vya dola, ni vyema tukaliacha kama lilivyo maana kuna vitu vinafanyika sitaki kuingilia. We fahamu kuna utaratibu unachukuliwa – upo njiani,” amesema Mulla.

Rais Magufuli, akiwa Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii (Mpingo House), Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam, alioneshwa pembe 50 za ndovu zilizokamatwa pamoja na magari yaliyotumika kubeba nyara hizo.

Watuhumiwa wanane wanaodaiwa kuhusika kwenye mtandao wa biashara haramu ya pembe za ndovu, walitiwa mbaroni kwenye operesheni hiyo.

Rais Magufuli alifahamishwa kukamatwa kwa jangili maarufu nchini, anayefahamika kwa jina la ‘Mpemba’, ambaye amekuwa akisakwa na vyombo vya dola kwa muda mrefu.

Kumekuwa na taarifa kwamba ‘Mpemba’ halisi hajakamatwa.

“Wapemba katika biashara hii wapo wawili. Yupo ‘Mpemba’ kinara zaidi ambaye hata Rais alidhani ndiye aliyekamatwa. Huyu ‘Mpemba’ kinara ana majina mengi. Jina lake ni Abdulkadir a.k.a Mbarouk, Sheikh, Mpemba. Huyu ni mfanyabiashara Kariakoo, anamiliki maghorofa kadhaa na anaishi Kariakoo Mtaa wa Manyema,” amesema mtoa taarifa wetu.

Mkuu wa Ushirikiano wa Polisi Kimataifa (Interpol) hapa nchini, SACP Gustavus Babile, ameulizwa juu ya taarifa za kutoroka kwa ‘Mpemba’, lakini amesema habari hizo ni ngeni kwake.

Juni, mwaka huu vijana wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa ‘Mpemba’, walikamatwa wakiwa na kilogramu 600 za pembe za tembo. Walikamatwa eneo la Msakuzi, Dar es Salaam. 

‘Mpemba’ anatajwa kuwa na ushirikiano wa kiuhalifu na baadhi ya wanasiasa maarufu, miongoni mwao akiwa ni mbunge katika moja ya majimbo Dar es Salaam. Kwa sasa JAMHURI inalifadhi jina lake.

Serikali imeunda kikosi kazi cha kupambana na ujangili kilichogawanywa katika kanda mbalimbali nchini.

Rais Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa mtandao wote wa majangili utavurugwa na hakuna atakayesalimika. Amewaagiza viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na vyombo vyote vya dola nchini, kuwakamata watuhumiwa wote wa ujangili bila kujali vyeo, umaarufu, jinsi, rangi, kabila wala dini.

Rais akiwa wizarani hapo, alisema: “Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na ninawahakikishia kuwa ninawaunga mkono, chapeni kazi, wakamateni wote wanaojihusisha na biashara hii haramu, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa au nani, kamateni, wala msijali cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu wake – sheria ni msumeno, watafuteni wote mpaka watu wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe ili tuokoe wanyama wetu ambao wanaendelea kuteketezwa.

“Hapa mmekamata pembe 50 maana yake tembo 25 wameuawa, haiwezekani maliasili yetu ikawa inapotea hovyo hovyo kwa sababu ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka.” 

Kuhusu kukamatwa kwa ‘Mpemba’, Rais Magufuli alisema kuwa angeshangaa iwapo kikosi hicho kisingeweza kumkamata kutokana na umaarufu wake, na kuwa ni mtu anayefahamika kwa kujihusisha na biashara hiyo kwa kipindi kirefu.

“Mpemba hilo ni jina lake analolitumia katika harakati zake za biashara ya ujangili ili asitambulike. Yuko mwingine pia anajiita ‘Mangi wa Kabila fulani’ lakini siyo majina yao halisi,” alisema.

Rais Magufuli amemteua Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali (mstaafu) George Waitara, kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).