Nchi hii kila kukicha inaacha maswali mengi. Mwanzo niliamua kunyamaza, lakini leo naona ni bora nihoji. Nahoji kutokana na taarifa zinazosambaa na kuzua mgogoro mkubwa ajabu katika mji wa Bukoba. Hapa inadaiwa kuna mapapa wawili – Mbunge Balozi Khamis Kagasheki na Meya Anatory Amani.
Taarifa zilizopo ni tuhuma kutoka kila upande. Kinachoendelea sasa ni vurugu. Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Kagera imeamua kuwatimua madiwani wanane. Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ikasitisha uamuzi huu.
Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, amesema CCM imesitisha uamuzi huo wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Kagera, na utapitiwa katika kikao cha Kamati Kuu kinachofanyika wiki hii. Kinachonipa shida sijui ni tuhuma zipi zenye uzito kati ya hizi nitakazotaja hapa chini.
Sitanii, nimesoma mara nyingi tuhuma kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Luteni Kanali Fabian Masawe, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Constansia Buhile, Katibu wa CCM Mkoa, Aveline Mushi, na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anathory Amani, lao moja.
Inadaiwa kuwa hawa wanashirikiana na kutumia kila nguvu, nafasi na fursa walizonazo kuonesha kuwa madiwani wanane wa CCM na mbunge wao wanaopinga maendeleo ni wavurugaji.
Pili, wananchi wa Wilaya ya Bukoba Mjini wameibiwa mchana kweupe. Tuhuma ni kwamba Meya Amani anafanya uamuzi binafsi bila kushirikisha vikao kwa kuwaumiza wananchi kwa kiwango kisichokubalika duniani na mbinguni.
Katika mradi wa upimaji viwanja, wananchi wa Kata za Nyanga na Buhembe, Meya Amani kwa kutumia kivuli cha halmashauri, bila kushauriana na madiwani aliwalipa wananchi fidia ya Sh 300 kila mita ya mraba ya ardhi iliyochukuliwa, lakini mwananchi huyo huyo aliyelipwa akimaliza kulipwa fidia ya Sh 300 kwa mita ya mraba, akitaka kuinunua mita ya mraba hiyo hiyo hata kabla hajaenda nyumbani, anaambiwa ailipie Sh 4,000.
Sitanii, Kampuni ya Mafuta ya Oryx ilipotaka kupewa maeneo ya kuweka vituo vya mafuta eneo la Kyakailabwa, Meya Amani inadaiwa akaiambia kampuni hiyo kuwa wananchi wamelipwa fidia ya Sh 1,600 kwa mita ya mraba.
Wananchi waliosikia uongo huu wakachukia, baadhi wakakataa kuchukua fidia na karibu wananchi 80 wamefungua kesi kupinga wizi huu. Mwananchi aliyelipwa Sh 700,000 akitaka kukinunua tena kiwanja kilichokuwa chake anaambiwa alipe Sh milioni saba!
Tatu, mradi wa stendi ya mabasi Kata ya Nyanga madiwani wanajulishwa tu kuwa Meya Amani ametumia Sh milioni 136. Uwanja wa stendi ya mabasi umesawazishwa, mradi haukuendelea na stendi imeendelea kubaki katikati ya mji wa Bukoba wakati uamuzi wa kuihamishia Kyakailabwa ulilenga kupanua wigo wa biashara na kuondoa msongamano mjini.
Sitanii, hivi ndivyo ilivyofanyika kwa Dar es Salaam stendi ilipoondolewa Kisutu na Mnazi Mmoja kwenda Ubungo. Na sasa wanafikiria kuihamishia Mbezi stendi hii. Uwanja uliosawazishwa Kyakailabwa kwa ajili ya stendi umeanza kuota nyasi.
Nne, suala la soko hakuna mtu anayekataa soko, bali wafanyabiashara hawajaandaliwa maeneo ya kwenda wakati soko linajengwa. Anatuhumiwa kuwa bila kuwashirikisha madiwani Meya Amani anasema Benki ya Uwekezaji (TIB) imekwishaikopesha Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kiasi cha Sh milioni 200 alizomlipa Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kuchora mchoro wa kujenga soko jipya eneo lililopo soko la sasa.
Pia inadaiwa kuna bonasi ya Sh milioni 90 imelipwa. Kwa nani? Haelezi. Soko hili anasema litajengwa kwa Sh bilioni 26, madiwani hakuna anayefahamu uhalisia.
Sitanii, tuhuma ya tano, kabla Amani hajawa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Baraza la Madiwani lilikwishapitisha uamuzi wa kujenga jengo la Kitegauchumi katika eneo ilipo stendi ya sasa. Mradi huu inadaiwa ameufuta. Tayari halmashauri ilikwishatumia Sh milioni 36 kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huu.
Sita, anadaiwa kuhamisha Mradi wa Maji wa Benki ya Dunia kutoka Kata ya Nyanga na kuupeleka Kata ya Kagondo anakotokea yeye kama diwani. Mradi huu ulipaswa kugharimu Sh milioni 700 hadi ujenzi wake unakamilika, lakini kwa sasa inadaiwa kuwa upembuzi yakinifu tu umechukua Sh milioni 800 na anawachangisha wananchi fedha za kujenga mradi huu.
Saba, halmashauri ilipendekeza kujenga barabara za kibiashara zinazozunguka mji wa Bukoba kuanzia Uwanja wa Ndege (Kashai) – Kahororo- Mugeza – Buhembe – Nyakato – Nyanga – hadi Kyakailabwa kwa ajili ya kuungana na barabara kuu ya lami ya Bukoba – Mtukura.
Pia Barabara ya Kashozi – imejengwa kwa kiwango cha lami kilomita tatu kutoka Machinjioni hadi Karuhunga (Nshambya), ili ipite Ihungo na kuungana na barabara iliyotajwa awali hapo juu eneo la Buhembe mji wote wa Bukoba uwe umeunganishwa kwa lami.
Hata hivyo, Amani ameamua kuweka kando mpango huu uliokuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete katika kampeni za mwaka 2010 ambapo watu wameishavunjiwa nyumba, anajenga barabara ya lami kwenye kata yake ya Kagondo.
Ameanza na ujenzi wa kilomita 2.5 kwa fedha za halmashauri kutoka Buzimba (Kagondo-Kaifo) kwenda Kagondo-Karuguru. Barabara hii haina faida yoyote kiuchumi zaidi ya yeye kufurahisha wapigakura wake kama diwani wao.
Tuhuma ya nane, mwaka 2000 Meya Amani akiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera inadaiwa kuwa alimpigia kampeni mgombea wa CUF, Wilfred Lwakatare, na kupeleka mbuzi usiku kwa Lwakatare kwa kutumia UKABILA kuwa aliyekuwa Mbunge wa Bukoba (M), Mujuni Kataraiya, alikuwa anatokea Tarafa ya Kiziba ni Mziba, na si Muyoza au mwenyeji wa Kyamtwara hivyo hakustahili kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini.
Wapo wanaosema Amani alifanikiwa Kataraiya akashindwa. Zamu hii anaendesha kampeni makanisani akisema mbunge wa sasa wa Bukoba (M) Balozi Khamis Kagasheki ni Mwislamu na Bukoba haistahili kutawaliwa na Waislamu.
Wanasema ameshiriki kikamilifu kuanzisha bucha ya nyama inayoitwa Edwin eneo la Rwamishenye kwa nia ya kumwangusha Majid Kichwabuta ambaye ni Mwislamu anayefanya biashara ya nyama na kwamba anaelekea kufanikiwa, kwani watu wengi wananunua nyama katika Bucha ya Edwin na wanazisusa za Kichwabuta.
Tisa, kati ya Kata 14 za Bukoba Mjini, CCM ina madiwani 10 wa kuchaguliwa kwenye kata. Saba kati ya madiwani hao wanampinga Meya Amani kupinga wanayoita madhambi haya anayofanya. Inaelezwa kuwa hata kufukuzwa kwa madiwani saba wa kuchaguliwa na mmoja wa viti maalum, kulikuwapo shinikizo.
Madiwani hawa wanatuhumiwa kuwa ni wasaliti wa maeneo. Hayo anayotuhumiwa Amani, inaelezwa kuwa ndizo tuhuma za madiwani hawa wanaodaiwa ni wasaliti. Madiwani wanaotajwa kuwa ni Deusdedith Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Daudi Karumuna (Ijuganyondo), Samuel Ntambala Luhangisa (Kitendaguro), Yusufu Ngaiza (Kashai), Richard Gasper (Miembeni) na Alexanda Ngalinda – Naibu Meya (Buhembe).
Inaelezwa madiwani wanaomuunga mkono Amani ni wawili; Chifu Karumuna (Kahororo) na Idebrandus Leo (Nshambya). Hawa inaelezwa kuwa sababu ziko wazi. Mwaka huu amewasafirisha kwenda barani Ulaya katika ziara ambayo halmashauri haikujulishwa ilikuwa ni ya nini na kwa manufaa gani.
Yeye Anatory Amani ni Diwani wa Kata ya Kagondo na ndiye anayehitimisha idadi ya madiwani 10 wa kuchaguliwa. Madiwani wanne; Dismas Rutagwelera (Rwamishenye), Israel Mlaki (Kibeta), Felician Bigambo (Bakoba) na Ibrahim Mabruki (Bilele) wanatokana na upinzani.
Tuhuma kubwa zinazomkabili Kagasheki ni kuwa anavuruga mipango ya Dk. Amani ili aharibu ndoto ya Dk. Amani kuwa Mbunge ifikapo mwaka 2015. Wanasema vurugu zote zinazoshuhudiwa ni kugombea ubunge mwaka 2015.
Sitanii, hali hii imeifikisha pabaya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. Ni vigumu kuendelea na utaratibu wa sasa. Rais Jakaya Kikwete amezitaka pande zinazokinzana kumaliza tofauti zao. Binafsi nasema migogoro haina tija kwa Taifa letu wala Manispaa ya Bukoba.
Ikiwa hali imefika mahala haieleweki, basi ni vyema Kamati Kuu ya CCM imalize mgogoro huu kwa kufanya uamuzi bila woga, wasiwasi au upendeleo kwa kiwango kitakachowafanya wananchi wenye kushuhudia haya yanayoendelea Bukoba kuwa haki imetendeka.