Na Tatu Saad,JamhuriMedia
Uongozi wa klabu ya Singida Big Stars umekanusha taarifa zinazoenea kuwa wamefanya mazungumzo ya awali na mabingwa watetezi wa Kombe la Ligi Kuu ya Tanzania Bara ‘Yanga SC’ kuhusu usajili wa mchezaji Bruno Gomez Baroso.
Taarifa zilizokuwa zikienea mitaani ni kwamba Klabu ya Yanga imekamilisha sehemu ya usajili wa kiungo huyo raia wa Brazil na kuanzia msimu ujao ataanza kuwatumikia wana jangwani hao.
Akizungumza Afisa habari wa klabu ya Singida Big Stars Hussein Masanza amesema taarifa hizo sio za kweli, Bruno ni mchezaji wao halali ambaye ana amesaini mkataba wa muda mrefu na klabu ya Singida Big Stars ya mkoani Singida.
“Tumeziona hizo taarifa lakini nikuhakikishie hakuna ukweli wowote kuhusu kufanywa kwa Biashara ya usajili wa Bruno Gomez, huyu ni mchezaji wetu halali na amesaini mkataba wa muda mrefu wa Singida Big Stars” amesema Masanza
Vilevile Masanza amesema wao kama Singida Big Stars wana kikosi bora chenye wachezaji wazuri Ndio maana imekuwa kawaida wachezaji wao kuhusishwa kuwaniwa na klabu nyingine za hapa Tanzania.
“Imekuwa kawaida kwa wachezaji wetu kuhusishwa na taarifa za kuwaniwa na klabu nyingine za hapa Tanzania” amesema Masanza.
Kabla ya taarifa za Bruno kuhusishwa na Yanga kuanza kusambaa kwa kasi, mchezaji huyo alishawahi kusema kuwa amekuja Tanzania kwa ajili ya kuitumikia Singida Big Stars na ana malengo makubwa na klabu hiyo.
Bruno Gomez Baroso ni raia wa Brazil aliyesajiliwa na klabu ya Singida Big Stars mwanzoni mwa msimu huu, na ndie kinara wa magoli wa klabu hiyo.