Kiwango cha elimu Tanzania kinatarajiwa kupanda, baada ya Serikali kuzindua mpango wa kufanikisha Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN).
Mpango huo umezinduliwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, na kuwashirikisha viongozi wengine wa elimu ngazi ya taifa, mkoa na wilaya.
Katika uzinduzi huo uliowashirikisha pia wadau mbalimbali wa elimu Dar es Salaam wiki iliyopita, Dk. Kawambwa alisema BRN ni tumaini jema litakalowezesha upatikanaji wa elimu bora hapa nchini.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kiwango cha taaluma katika shule nyingi kimekuwa hakiridhishi kutokana na matatizo mbalimbali yakiwamo ya idadi ndogo ya walimu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
“Ingawa kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi kimeongezeka, ubora wa elimu umeshuka kwa ufaulu katika shule za msingi na sekondari,” alisema Waziri huyo.
Viongozi watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) walitiliana saini wakiahidi kujituma na kuwajibika kutekeleza BRN kwa vitendo ili kufuta aibu ya kuporomoko kwa kiwango cha elimu hapa nchini.
“Kila mmoja akijituma na kuwajibika katika nafasi yake atasababisha kuwapo kwa mabadiliko na maendeleo makubwa katika sekta ya elimu,” alisema Waziri Kawambwa.
Mpango wa BRN una mikakati tisa ukiwamo wa upangaji wa matokeo kwa kuzingatia ufaulu na tuzo kwa shule, unaolenga uwajibikaji na ushiriki wa jamii katika usimamizi wa utoaji elimu bora.
Mikakati mingine ni motisha kwa walimu, kushughulikia madai ya msingi na kuboresha maslahi yao, utoaji ruzuku kwa ajili ya vifaa vya shule, ujenzi wa miundombinu, kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wa elimu wametoa wito kwa viongozi husika kusimamia na kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa vitendo ili kufikia malengo yanayokusudiwa.