Pamoja na malalamiko mengi na ya mara kwa mara, lakini ndugu zangu Watanzania wenzangu hawa wamejaaliwa uwezo mkubwa sana kiuchumi (have a very strong economic base). Hilo kamwe hawalitangazi wanaliacha kwenye “low profile”- mambo yao kimya kimya tu.

 

Angalia sekta ya usafirishaji -daladala, teksi, mabasi na malori ya kubebea mizigo- karibu asilimia 90 ni mali ya Waislamu (ukiondoa Moshi, Bukoba na kule Makete kwa Wakinga). Je, wasio waislamu wanalalamikia kukosa fursa sawa kiuchumi? Hapana!

 

 

Twende kwenye nyumba za kupangisha. Karibu katika miji yote nyumba namna hii ni mali ya mamwinyi wa kiislamu. Asiye mwislamu hajalalamikia tofauti namna hiyo.

 

Ndiyo kusema ule utamaduni wa kiarabu wa biashara wenzetu wamekuwa nao tangu kale, ni mapokeo waliyopata toka kwa wagenii kutoka Arabuni. Mikoa ya kusini – tangu enzi za ukoloni magari yalinunuliwa na waislamu tu akina Manzi, Matumla, Sefu Mtekateka, akina Adam Yakiti, akina Nasoro Litunu, na kadhalika.

 

Laiti kama daladala, mabasi, malori na teksi yangemilikiwa zaidi na wakristo kungesikika lalamiko kuwa utoaji leseni za biashara unawakandamiza waislamu.

 

Tukubali tu kuwa tamaduni za kigeni tulizopokea kwa karne kadha zimetufikisha hapa penye ubaguzi wa wazi kulingana na mila na desturi kutoka Ulaya (ukristo) na mila na desturi kutoka bara Arabia (uislamu). Je, ndiyo tukubali hali hiyo iendelee kutugawa? Kwanini tusirudi kwenye mila na desturi zetu asilia za ubantu ambamo hakuna tofauti yoyote kati ya Watanzania?

 

Aidha, ndugu yangu Elias Msuya akagusia lile suala nyeti, lakini dai la muda mrefu la kutaka Mahakama yha Kadhi. Suala hili zaidi ni la mapokeo, wala siyo la kikatiba.

 

Nchi hii watu wake wamehusiana na wageni kutoka Arabuni na kutoka Ulaya. Wageni hawa wameleta dini na utamaduni wa makwao. Waarabu kutoka Uajemi wamefika huku Afrika Mashariki tangu karne ya 16 wakawa sehemu za Kilwa na Bagamoyo, na karibu Pwani yote ya Tanganyika.

 

Wameoleana na wananchi na kuzaa na vizazi kadhaa vipya! Karne ya 19 walipofika Waarabu kutoka Oman ndipo wakaleta na utawala ya kisultani visiwani Zanzibar na wakaenea hadi Pwani ya Tanganyika. Sultani wa Zanzibar aliyeitwa Seyyid Said mwaka 1832 akaeneza ufalme wake Pwani ya Tanganyika. Huyu ndiye aliyeleta Mahakama ya Kadhi hapa nchini na aliteua wawakilishi wake waarabu akawaita maliwali.

 

Maliwali wake ndiyo walitumika kuhukumu wakazi wote chini ya milki ya sultani. Maliwali walikuwepo hadi tunapata Uhuru – miji yote ya pwani -Tanga, Pangani, Bagamoyo, Dar es Salaam hadi Mikindani.

 

Mjerumani alinunua ule ukanda wote wa pwani maili 10 kutoka bahari kwa Sultan wa Zanzibar kwa bei ya fedha za kijerumani DMC (Dochi Maki) milioni 4 (sawa na pauni za waingereza 200,000 siku hizo) mwaka 1890 (J. Clagett Taylor:

 

The Political Development of Tanganyika uk. 16). Hivyo milki ile ya sultani sasa ikawa chini ya Mjerumani, lakini maliwali walibaki na mahakama zao za kadhi zikaendelea huku bara miji hii ya pwani.

 

Mjerumani hakuzifuta zile Mahakama za Kadhi, bali aliweka mahakama ya kiserikali kwa wazungu, wahindi na magoa. Mwingereza alipoingia mwaka 1918 hakuzifuta Mahakama za Kadhi, bali aliziongezea nguvu pale alipotunga sheria ya Mahakama iliyoitwa

 

The Native Authority Ordinance 1923. Sheria hii ilitambua utawala wa machifu kwa nchi nzima kwa kutumia Mahakama zilizoitwa “Native Courts” na kwa pwani iliendeleza matumizi ya Mahakama za Kadhi. Katika Mahakama hizo walitumia sheria za mila na jadi zilizoitwa “Customary Laws”. Kwa pwani sheria ilisema Mahakama za Kadhi zisiingiliwe na Serikali na zitatumika kumaliza kesi za mambo binafsi kama ya ndoa, talaka, malezi ya watoto, mirathi, wasia na wakfu.

 

Vitabu vya rejea katika Mahakama namna hiyo ni Qur’an, Sunna, Qiyas na Ijma. Kule Bara kwa machifu “customary laws” zilitumika kumaliza matatizo yote ya kikabila. Kumbe ni ukanda ule wa pwani tu ndiyo uliofuata mapokeo haya ya Kiarabu (Arabic culture) chini ya wakoloni wazungu.

 

Sehemu kubwa sana ya Tanganyika lilifuata mila na desturi za makabila yao na wakapokea desturi za wazungu waliotawala yaani ustarabu wa magharibi (western culture). Huu ustaarabu wa magharibi ndiyo uliokuja na dini ya kikristo.

 

Hivi nchi yetu ikajikuta ina desturi na mila za kienyeji (tribal traditions) mila na desturi za kiarabu (Arabic Culture) na mila na desturi za kizungu (western culture) ndipo na dini zetu ziko namna hiyo hiyo, zipo dini za asilia (paganism) upo uislamu (Islam) na upo ukristo (Christianity). Basi kwa mapokeo namna hiyo siyo sahihi, pokeo moja lidai utamaduni wake ndio uingizwe katika Katibza ya nchi.

 

Mimi ninafarijika sana ninapoona viongozi wetu wakuu wa Serikali na wa madhehebu mbalimbali wanakaa pamoja na kuzungumza uhusiano wetu wa kidini kwa lengo la kuimarisha UMOJA WA KITANZANIA.

 

Mathalani, ile Kamati ya Haki za Bunadamu yenye wajumbe wa madhehebu yote hivi karibuni imekosoa Serikali kwa utaratibu wake wa misamaha ya kodi na wakasema wazi wazi matrilioni ya fedha yamepotea kwa misamaha ya kodi.

 

Hapa uzalendo umewaunganisha wakristu na waislamu kuwa Watanzania. Juzi juzi hapa, Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi akizindua vitabu viwili katika ukumbi wa Diamond, alituasa tujenge tabia ya kutii sheria bila kushurutishwa.

 

Alipongeza madhehebu yote- waislamu na wakristo kwa kuandaa kampeni hiyo kwa pamoja akisisitiza kuwa kutii sheria bila shuruti kuna thawabu.

 

Huko nyuma Bwana Abdul Mtemvu alitoa makala yake katika gazeti la Mtanzania la Jumatano Aprili 29, 1998 uk. 7 iliyosema, “…Kujua Uislamu siyo jambo rahisi, ni jambo linalotaka uvumilivu na akili yenye ujasiri.” Ni kweli kabisa wale wote wanaojua uislamu hawapayuki ovyo ovyo. Ni wasikivu, hawana dharau kwa wasiokuwa waislamu, bali wanashirikiana kutunza amani.

 

Aidha, katika Qur’an Tukufu kuna miongozo mingi tu, kama vile Sura ile ya II BAQARAH aya ya 256 inasema wazi Uislamu Haulazimishi. Tukienda kwenye ile sura ya IV MAIDAH aya ya 82 inasema Uislamu hauchukii Ukristo; sasa vipi waislamu halisi wachome makanisa? Chuki namna hiyo siyo imani ya uislamu.

 

Nimesema mengi kujaribu kuonyesha kwa jadi zetu asilia Watanzania hatuna chuki za udini. Hayo tumeambukizwa na mila za kigeni kutoka Ulaya na Arabuni. Kwa vile wazungu waliwadharau sana waarabu katika ile karne ya 19, basi ukajengeka uhasama kati yao.

 

Walipofika huku kwetu Tanganyika kila kundi likawa linamsema mgeni mwenziwe. Pili, kila kundi limeleta dini yake -wazungu wameleta ukristo; waarabu wameleta uislamu.

 

Kejeli za wazungu kwa uislamu ziliwaumiza sana waarabu. Mathalani, kuanzia karne ya 19 wasomi mbalimbali wamesema maneno namna hii nanukuu, “certain scholar exponents of comparative religions say that unlike HINDUISM, CHRISTIANITY and ISLAM are PRORELYTIZING RELIGIONS” in many parts of the world these two have therefore been rivals…” yaani tofauti na dini ya Kihindi, Ukristo na Uislamu ni dini zinazotafuta uongofu wa watu, ndiyo sababu kila dini inavutia kwake kupata wafuasi wengi zaidi.

Basi, zimekuwa dini zenye ushindani.

 

Pili wasomi wa kiarabu na wa kizungu wamediriki kusema hivi,  “Different sources of information reveal the ROOT CAUSES OF ISLAMIC POLITICAL MOVEMENTS AND MUSLIM RADICALISM in the world today are the charges against Islam which HURT MUSLIM INTELLECTUALIS most deeply…. It is the impact of WESTERNERS’ political disparagement of the 19th Century made against MUSLIMS that has influenced much in the thinking of people of people in MUSLIM/CHRISTIAN populated countries….”

 

Maneno haya ndiyo yanayoonyesha hali halisi katika nchi kama hii yetu na nyingine kama hii zenye wakristo na waislamu karibu sawa kiidadi. Mitafaruku kadha huwa inatokea kati ya wafuasi wa dini hizi mbili.

 

Tanzania sote ni wazawa na wa asili ya ubantu tofauti kabisa na nchi kama Ireland ambako wakristo wao kwa wao hawaelewani eti wana madhehebu tofauti -hawa wakatoliki, hawa waanglikana.

 

Tukienda Iran waislamu wao kwao wanalumbana, hawaivi eti hawa wa Sunni na wengine wa Shia. Nenda Lebanon pale ndiyo kuna malumbano kati ya wakristo na waislamu. Sisi je, tunataka utamaduni huo wa kigeni? Hapana, katu hatuupokei tuepuke basi vishawishi vya kutugawa kwa misingi ya ufa ule na. 5 wa udini na ukabila.

 

Nchi yetu haina dini ya taifa, bali ina wananchi wenye imani mbalimbali kadri ya mapokeo waliopata kutoka kwa wageni waliotuingilia kimabavu wazungu (ukristo) na waraabu (uislam).

 

Tubaki Watanzania wenye utamaduni wetu. Kwa hiyo tutaendelea kuwa na Watanzania wenye dini za kiasilia (wapagani), watakuwapo wakristo na watakuwapo waislamu – nchi moja, taifa moja, lakini imani za kiroho ni tofauti kutokana na mapokeo tuliyonayo.

 

Mwalimu Nyerere aliwahi kuzungumza na mashekhe kule Zanzibar na aliwahi kuzungumza na maaskofu kule Tabora na kukazia kuwa nchi yetu haina dini, watu wetu wana dini na wengine hawana dini (Nyufa: uk. 27 ibara ya pili).

 

Watanzania tuuzibe ufa huu namba 5 ili taifa letu lisimegeke kidini wala kikabila tusije tukasema wao ni… na sisi? SOTE TU WATANZANIA tumetokana na yale makabila yetu ya kibantu (ethnic bantu tribes).

 

Mwandishi wa makala hii, F. X. Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu: 0755 806 758; email: [email protected]