Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Wazazi na walezi hapa nchini wametakiwa kuona umuhimu wa kuwasimamia kwa karibu Watoto wao wanaosoma katika shule za msingi na sekondari ili waweze kuepukana na tabia mbaya za utoro, uvutaji bangi na amewahimiza kujenga ushirikiano wao katika malezi bora na ufuatiliaji wa karibu maendeleo ya watoto wao wawapo shuleni kwani jukumu la wazazi haliko kwa kulipa ada peke yake.

Haya yamesemwa mwishoni mwa wiki na Mshauri wa Jeshi la Akiba wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Charles Mzena kwa niaba ya Brigedia Kamanda Meja Jenelali Charles Feruzi wakati wa mahafali ya 20 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Ruhuwiko inayomilikiwa na Jeshi la wananchi Tanzania {JWTZ ) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa shule hiyo.

Luteni Kanali Benedicto Bahame Mkuu wa shule ya sekondari Ruhuwiko inayomilikiwa na Jeshi (JWTZ)akizungumza kwenye mahafari ya kidato cha sita ya shule hiyo.

Kanali Mzena alisema kuwa jukumu la wazazi na walezi wa watoto wanaosoma ni kujua mwenendo na tabia ya watoto wao katika mazingira ya shuleni na jamii hivyo amewaonya wazazi wanaoshindwa kuwasimamia watoto wao waondokane na tabia hiyo ambayo inaweza kuleta mmomonyoko wa maadili kwa jamii kiujumla.

Alisema kuwa baadhi ya wazazi na walezi hujihusisha zaidi na kutoa fedha kwa watoto wao pasipo kujua matatizo pamoja na mahitaji halisi na tabia na maendeleo ya taaluma wanayokumbana nayo na si vinginevyo.

Kanali Charles Mzena mshauri wa Jeshi la akiba Mkoa ambaye ni mgeni rasmi kwenye mahafari hayo akimwakilisha Kamanda Brigedia ya kusini Meja Jenerali Charles Feruzi.

Alieleza zaidi kuwa mtoto kwa mzazi hakui hivyo ni muhimu wazazi kuendelea kutoa muelekeo wa Maisha, maadili pamoja na nidhamu hata baada ya watoto kufika kidato cha sita na amekemea vikali tabia zisizofaa ambazo zimeshamiri mitaani kama matumizi ya dawa za kulevya, bangi, na mienendo mingine isiyofaa kwani vijana bado wanahitaji uhangalizi mkubwa pamoja na maelekezo yenye mchango chanya kwa Taifa.

Katika nasaha zake kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo katika shule ya sekondari ya Ruhuwiko pamoja shuke zingine aliwataka kuiga mfano mzuri kwa watangulizi wao na kusoma kwa bidi ili kufikia ndoto zao na alisisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuona umuhimu wa kushirikiana na walimu kwa ajili ya mafanikio ya pamoja ya wananfunzi kwenye shule wanazosoma.

Kwa upande wake mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ruhuwiko inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Kanali Benedicto Bahame, alieleza mafanikio ya shule yake tangu ilipoanzishwa ikiwa ni pamoja na kupata tuzo mbalimbali, barua za pongezi na kutajwa kuwa shule inayoongoza kwa ufaulu miongoni mwa shule kumi hapa nchini za JWTZ.

Wanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Ruhuwiko

Luteni kanali Bahame alieleza kuhusu mchango wa mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini (CDF) Jenerali Jacob Nkunda ambaye mnamo Novemba 2022 alifanikiwa kutembelea shule hiyo na alichangia kiasi cha fedha shilingi milioni 238 kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi mkubwa wa kisasa ambao kwa sasa tayari umeanza kutumika.

Muhitimu wa kidato cha sita Omary Ramadhani akisoma risala ya wahitimu wenzake alielezea mafanikio waliyoyapata katika kipindi chote cha masomo shuleni hapo ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu kutokana na mpango mzuri wa kuhamasisha wanafunzi wote wa kidato cha sita kwenye mabweni ili kuwawezesha kujisomea kwa utulivu pia waliweza kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo michezo, utalii na kuanzisha vilabu vya dini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambavyo vimeweza kuwajengea uwezo mkubwa wa ujuzi na kijamii.

Makamu mwenyekiti wa bodi ya shule Yusufu Mwikoki aliwatakia wanafunzi mtihani mwema huku akiwakumbusha kuendelea kudumisha maadili waliyofundishwa kwani elimu bila nidhamu si lolote .

Mwikoki alifafanua kuwa shule hiyo inajumla ya wananfunzi 1155 ambapo wahitimu wa kidato cha sita kati yao ni 274 wakiwemo wasichana 84 na wavulana ni 190.

Wazazi na walezi kwenye mahafari ya kidato cha sita Shule ya Sekondari Ruhuwiko