Na Cresensia kapinga, JamhuriMedia, Songea
Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanda ya kusini amewataka wahitimu wa kidato cha sita wa shule ya Sekondari ya Ruhuwiko Manispaa ya Songea inayomilikiwa na JWTZ kuzingatia elimu waliyopata na kufanya mitihani ya taifa vizuri inayotarajia kufanyika hivi karibuni.
Ushauri huo umetolewa jana na Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi kwenye mahafali ya 19 ya kidato cha 6 yaliyofanyika kwenye ukumbi mpya wa mikutano wa shule hiyo yaliyohudhuriwa pia na wazazi,walezi wa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya kidato cha sita.
Amesema kuwa ni wajibu wa kila mwanafunzi kuona namna ya kujitahidi kufanya vizuri zaidi katika mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni na hasa ikizingatiwa kuwa shule ya sekondari Ruhuwiko kwa muda mrefu imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na sita.
Ameongeza kuwa kitaaluma shule ya Sekondari Ruhuwiko iko vizuri hivyo anaamini kuwa baada ya kufanya mitihani hiyo matokeo yatakuwa mazuri na kuendelea kuleta sifa nzuri ya shule hiyo na ameupongeza uongozi wa shule ya sekondari hiyo pamoja na walimu kwa kuhakikisha kuwa taaluma kwa wanafunzi wao inaleta matumaini mazuri kwa Jamii.
Mkuu wa Shule hiyo ya Ruhuwiko LT COL Benedicto Bahame mapema akitoa taarifa ya utendaji wa shule hiyo kwa mgeni rasmi katika mahafali ya kidato cha sita Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi,alisema kuwa shule ya Sekondari ya Ruhuwiko ni miongoni mwa shule 10 zinazomilikiwa na Jeshi la ulinzi wa Tanzania hapa nchini ambazo alitaja shule hizo kuwa ni Airwing, Ali Khamis Camp, Jitegemee, Kawawa, Kigamboni, Kizuka, Makongo, Nyuki, Ruhuwiko na Unyenyembe na kwamba shule hiyo ni ya mchanganyiko kwa wavulana na wasichana ikiwa ni ya bweni na kutwa kuanzia shule ya awali,Msingi,kidato cha kwanza hadi cha sita.
Amesema kuwa shule ya sekondari ya Ruhuwiko ilianzishwa mwaka 1979 awali ikijulikana kwa jina la Huduma JWTZ Center na kimsingi ilianza ikiwa na kituo cha kufanyia mitihani na ilianzishwa kwa lengo la kuwaendeleza askari wa Jeshi la wananchi ambao hawakuwa wamefikia elimu ya kidato cha nne kwa wakati huo baada ya lengo la JWTZ la kusomesha askari wake angalao kufikia kidato cha 4 kufanikiwa kwa asilimia kubwa na kufutwa rasmi kwa mpango huo uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania JWTZ uliona ni busara kundelea kutoa huduma za shule kwa familia za Jeshi na raia.
LT COL Bahame amesema kuwa maendeleo ya taaluma katika shule yake yamekuwa yakiimarika mwaka hadi mwaka ambapo shule hiyo imekuwa na maendeleo ya kitaaluma na hasa kwa upande upande wa kidato cha tano na sita kwani shule hiyo imepata tuzo na zawadi kwa nyakati tofauti ambapo alitoa mfano kuwa mwaka 2020 shule hiyo ilitunukiwa tuzo na cheti na Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo kwa wakati huo kwa kuwa shule ya tisa kitaifa miongoni mwa shule zilizoboresha ufaulu kwa kiwango cha juu kwenye mitihani ya kidato cha 6 mwaka 2020.
Amesema kuwa mwaka 2021 hadi 2023 matokeo ya kidato cha 6 yameendelea kuwa mazuri zaidi na kufanya shule hiyo kuwa ya kwanza mfululizo kati ya shule 8 za kadato cha 5 na 6 zinazomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania ambapo matokeo hayo ya kidato cha 6 yameendelea kuwa mazuri zaidi kwa miaka mingi mfululizo na mwaka 2023 shule hiyo imefanikiwa kabisa kufuta daraja la 3 kwa kupata ufaulu wa daraja la 1 na la 2 na lengo la shule hiyo kwa sasa ni kuwa na ufaulu wa daraja la kwanza tu na si vinginevyo.