NaTatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa wito kwa wakulima kutembelea banda lao lililopo katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ili kuweza kusajili nembo na alama za biashara.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Usajili kutoka BRELA Dodoma, Gabriel Girangay, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo kwenye maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Amefafanua kuwa wakulima ni wadau muhimu kwani wanapozalisha mazao wanayaongezea thamani hivyo kuhitaji kusajiliwa nembo au alama za biashara.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili watambue kwamba BRELA ni muhimu kwao katika kusimamia au kulinda bidhaa zao. Tutalinda vumbuzi zao katika masuala mbalimbali yanayohusiana na kilimo na teknolojia,” amesema Girangay.

Amesema wakala huo unafanya kazi ya kusajili kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, kutoa leseni za biashara kundi A, leseni za viwanda, kusajili viwanda vidogo na kulinda vumbuzi za wataalam mbalimbali.

“Tuko kwenye maonesho ya Nanenane kwa ajili ya kutoa elimu na huduma mbalimbali, ukifika katika banda letu utapata huduma za kusajiliwa jina la biashara na kila Mtanzania mwenye nia ya kuanzisha biashara afike kuna wataalam wa masuala ya Tehama, biashara, alama za biashara na huduma na shughuli zetu nyingi zinafanyika kidijitali.

“Tunatoa leseni za biashara kundi A ambazo ni zile zenye sura ya kitaifa na kimataifa, utaelimishwa kwanza na kama unataka kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi au kutoa bidhaa kutoka nje na kuleta nchini utapata leseni BRELA,” amesema.

Amefafanua kuwa BRELA inatoa leseni za viwanda vikubwa na vya kati vyenye mtaji wa kuanzia Sh milioni 100 kwenda juu lakini Sh milioni 100 kwenda chini ni viwanda vidogo ambavyo pia wanavisajili.

Aidha amesema kama mtu anahitaji kupata taarifa yoyote kuhusu kampuni, majina ya biashara, leseni au wanaotaka kukopa na kuingia ubia wa kibiashara afike katika banda hilo au ofisi za wakala huo na atapatiwa.

Please follow and like us:
Pin Share