Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umefuta usajili wa kampuni 11 za LBL chini ya kifungu 400A cha sheria sura 212 mara baada ya kampuni hizo kufanya shughuli za kibiashara nje ya madhumuni yaliyoainishwa katika katiba na miongozo ya uendeshaji wa kampuni wakati wa usajili.
Kampuni hizo ni LBL Mtwara Company limited, LBL Morogoro Media Company Limited, LBL Geita Adversting Media Limited, LBL Mbeya Limited, LBL Future Vision Advertising Agency Company Limited, LBL Mbezi Advertising Media Company Limited, LBL Ubungo Media Limited, LBL mabibo Media Company Limited, LBL mbagala Media Company Limited, LBL Gongo la mboto Media Advertising Company Limited na LBL Dar es salaam Kigamboni Advertising Company Limited.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema mara baada ya kubaini dosari katika kampuni hizo msajili alizijulisha kampuni kuhusu kusudio la kuzifuta kati ya tarehe 2 na 26 Januari mwaka huu na kwamba kampuni hizo hazikuwasilisha maelezo yeyote.
Aidha ametoa wito kwa Watanzania pale wanapotaka kukopa fedha kujihakikishia kama taasisi husika inajulikana na Taasisi za kifedha kama Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ili kuepuka kupata hasara huku akiwahimiza kutoa taarifa mara moja kwa mamlaka husika zikiwemo taasisi za kiserikali na jeshi la polisi pale wanapoona biashara ya upatu ili hatua stahiki zichukuliwe.
Sambamba na hayo amesema BRELA kupitia msajili wake inaendelea na ufuatiliaji wa kampuni nyingine zinazofanya shughuli za kibiashara nje ya katiba zao na kinyume cha sheria na utaratibu.

