Menejimenti ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imefumuliwa.

Katika mpango mahususi unaotajwa kuwa unalenga kupambana na rushwa, vishoka, utendaji wa mazoea, na kuifanya BRELA ishiriki vilivyo kwenye ujenzi wa uchumi wa taifa, vigogo watano tayari wameondolewa kwenye nafasi zao.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa baada ya kufuta uongozi wa juu, kinachofuata sasa ni kuwaondoa wafanyakazi wote wanaokabiliwa na kashfa za uzembe, rushwa na urasimu.

Miongoni mwa vigogo walioondolewa tayari ni Mkuu wa Utawala, Bakari Mketo, ambaye amepelekwa Utumishi. Mwaka jana Mketo aliondolewa na kupelekwa mkoani Mbeya, lakini katika mazingira yanayotia shaka, alirejea kwa kile kilichoelezwa kuwa ni “maagizo kutoka juu”.

Aliyekuwa Mkuu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Geofrey Mwakijungu, amepelekwa Tume ya Umwagiliaji mkoani Dodoma.

Mkuu wa Fedha, Bosco Gadi, naye ameondolewa BRELA, na sasa amepelekwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko na Nafaka.

JAMHURI limethibitishiwa kwamba aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kampuni, Geofrey Kobelo, ameondolewa, kwa sasa anasubiri kupangiwa kazi nyingine.

Pia, aliyekuwa Mkuu wa Hakimiliki, Loy Muhando, na ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Afisa Mtendaji Mkuu, naye ameondolewa. Amepelekwa Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mabadiliko haya yamekuja wiki chache baada ya kuteuliwa kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfey Nyaisa. Uteuzi huo ulifanywa Januari 19, mwaka huu na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa. Kabla, Nyaisa alikuwa Mkurugenzi wa Utawala katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa mujibu wa Waziri Bashungwa, kuteuliwa kwa Nyaisa kumelenga kuisuka upya BRELA na kufuta taswira mbaya ya kiutendaji ambayo imekuwa ikilalamikiwa mno na wafanyabiashara.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa pamoja na kupanguliwa kwa safu ya uongozi, kuna mabadiliko makubwa yameshafanywa, na mengine yanaendelea kufanywa.

JAMHURI limemtafuta Nyaisa ili kupata undani wa mabadiliko hayo, lakini amegoma kutoa ufafanuzi. “Mimi ni Afisa Mtendaji Mkuu, si Msemaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Msemaji ni Katibu Mkuu, mtafute, atakupa maelezo unayotaka,” amesema Nyaisa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe, amesema: “Ninachojua tumefanya mabadiliko ya kuwa na Afisa Mtendaji Mkuu…ameanza vizuri, na kwa kweli kazi zinafanyika. Hayo mabadiliko mengine siyajui, lakini kama yapo, basi yanalenga kuboresha kazi za BRELA.”

Kwa miaka yote ya kuanzishwa kwake, taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi bila kuwa na kanuni zinazosimamia utendaji kazi wa utumishi.

“Huyu Afisa Mtendaji Mkuu amekuja kutusaidia, hatukuwa na staff by laws, hazikuwapo. Kila mtumishi alifanya anayojua yeye mwenyewe, sasa kunaundwa mfumo wa rasilimali watu, kunawekwa mfumo wa kuratibu kazi za kila mtumishi,” kimesema chanzo chetu.

Hatua nyingine ni kuandikwa kwa kanuni za usimamizi wa fedha, kwa kile kinachoelezwa kuwa kukosekana kwake kulitoa mwanya wa ufujaji.

‘Kibano’ kingine kilichowekwa ni cha kufutwa kwa malipo ya ziada, ambapo wakuu wa vitengo wameagizwa kuandaa mpango kazi wenye matokeo yatakayoendana na kazi kwa mujibu wa ajira ya kila mmoja.

Uongozi wa Nyaisa umefuta malipo ya muda wa ziara kazini baada ya kubaini kuwa kila mfanyakazi anapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa mkataba wake wa ajira. Kwa uamuzi huo, BRELA sasa imeokoa Sh milioni 3 kila siku ambazo zilitumika kwa malipo ya muda wa ziada kazini.

Katika mabadiliko hayo, BRELA inakusudia kufunga mtambo wa kisasa wa kuhudumia wateja; lengo likiwa kupunguza malalamiko ya wateja. BRELA imekuwa ikilalamikiwa mno kwa huduma mbovu, urasimu na vitendo vya rushwa.

Mfumo wa kusajili kampuni kwa njia ya mtandao nao umefumuliwa. Habari Mfumo uliopo sasa unaendeshwa kutokea nje ya nchi kwa muuzaji wa teknolojia hiyo aliyeko nchini Ukraine. Kwa mabadiliko yanayokuja, mfumo huo sasa unaandaliwa na Watanzania na kuendeshwa na Watanzania wenyewe. “Hii ni kwa masilahi na usalama wa nchi yetu,” kimesema chanzo chetu.

Mfumo huo wa Online Registration (ORS), ulinunuliwa kwa Sh bilioni 2.6; lakini BRELA imekuwa ikilipa Sh milioni 600 kila mwaka kwa ajili ya matengenezo.

“Huu ulikuwa wizi, kwa sababu Sh milioni 600 ni nyingi mno. Malalamiko ya wateja yamekuwa mengi kuwa mtandao haufanyi kazi au mtandao uko chini, lakini ukweli ni kwamba kulikuwa na mwenzetu humu kwenye kitengo hicho aliyekuwa akiutibua ili zitolewe fedha kwa ajili ya matengenezo.

“Tulipokuwa tukiwasiliana na aliyetuuzia mfumo huu kutoka Ukraine alituelekeza kwa wakala wake aliyeko Dar es Salaam, na kumbe wakala mwenyewe alikuwa ni watumishi fulani wa BRELA walio ndani na mwingine aliyeamua kuacha kazi ili anufaike kwa njia hiyo ya udanganyifu,” imeelezwa.

Katika kuthibitisha hiyo, mmoja wa wafanyakazi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara amesema yalitolewa maagizo kutoka uongozi wa juu kuhakikisha kuwa njama hizo zinabainika.

“Mfumo ulipokorofishwa wakaletwa vijana kutoka serikalini, wakaushughulikia na ni wao waliosaidia kubaini nani waliokuwa wakiuchezea. Hilo tumelishughulikia, lakini pamoja na hilo kuliweka sawa bado msimamo wetu ni kujenga mfumo wetu wenyewe kwa kuwatumia vijana wa Kitanzania – wasomi wazuri. Wanayajua haya mambo vizuri sana,” kimesema chanzo chetu.

Mabadiliko mengine kwa mujibu wa chanzo chetu ni kwenye ‘scheme of service’ ambayo imeonekana kupitwa na wakati.

“Tuliona imepitwa na wakati, tukashauri ipitiwe upya ili iendane na uhalisia. Mfano, wakubwa wetu waliweka kifungu kuwa ili uwe mtendaji mkuu au mkurugenzi wa utawala lazima uwe mwanasheria.

“Lengo la mpango huu ilikuwa ni wajanja wachache kutaka kugawana madaraka badala ya kuangalia na kuweka mbele masilahi ya nchi, tunashukuru hili nalo huyu bosi mpya ameliona.

“Ofisi ilikuwa kama kijiwe cha wapiga dili, sasa kila anayeingia lazima aandikishwe na kutoa kitambulisho cha shughuli anayofanya, kwa kweli sasa tuna matumaini ya kuiona BRELA mpya,” kimesema chanzo chetu.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwenye Bodi ya BRELA zinasema muda si mrefu makao makuu ya taasisi hiyo yatahama kutoka yalipo sasa, Mtaa wa Lumumba, na kwenda katika yalikokuwa Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Mtaa wa Sokoine na Shaaban Robert jijini Dar es Salaam.

“Lengo ni kuhakikisha wanakuwa katika ofisi nzuri na sehemu moja isiyokuwa na mwingiliano mkubwa na taasisi nyingine. Watakuwa wanajua nani anaingia, na anaingia kufanya nini. Huu ndiyo mwisho wa ‘vishoka’,” amesema mmoja wa wajumbe wa bodi.

Katika ofisi zao zilizoko katika Jengo la Ushirika, imeelezwa kuwa baadhi ya watumishi wa BRELA walifungua ofisi zao binafsi kwa ajili ya kupokea rushwa kutoka kwa wateja.

“Unakuta, kwa mfano usajili wa kampuni ni Sh 100,000. Mteja akifika anazungushwa na kuambiwa aende ofisi fulani ili asaidiwe haraka. Akifika kule anaambiwa atafanyiwa usajili wa kampuni yake ndani ya muda mfupi kwa malipo ya Sh 500,000. Kwa hiyo urasimu waliokuwa nao BRELA ulilenga kuwachosha wateja ili hatimaye watoe rushwa na ndipo wahudumiwe haraka.

“Sisi kwenye bodi tulishangaa kuona hata kwenye ofisi za kutunzia mafaili kamera za usalama zimenyofolewa. Zimenyofolewa ili kuwapa muda mzuri wa kuiba mafaili au kunyofoa nyaraka kutoka kwenye mafaili,” amesema.

Katika mkakati mpya, BRELA sasa watakuwa na mfumo mpya wa kuhifadhi mafaili kwa njia ya kawaida na ya kielektroniki; lengo likiwa ni kukomesha hujuma zilizokuwa zimeshaota mizizi.

Katika mabadiliko yanayoendelea, kampuni zaidi ya 10,000 ambazo zimesajiliwa, lakini hazifanyi kazi, zinahakikiwa sasa ili kufuta ambazo zipo kwa ajili ya ‘kutega biashara’.

Miongoni mwa kampuni hizo ni za wanasiasa ambazo chanzo chetu cha habari kinasema zimekuwapo mahususi kwa ajili ya kunasa ‘dili’ zinazotokana na wageni wanaokuja kuwekeza nchini.  

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa mno na wadau ni usajili wa kampuni nchini Tanzania kwa njia ya mtandao. Baadhi ya kero hizo ni kuambiwa kuwa “mfumo upo kwenye matengenezo”, “maombi yapo ‘final decision’” na uelewa mdogo wa masuala ya kampuni na kodi miongoni mwa watumishi wa BRELA.

Kwenye andiko moja kwenye mtandao wa kijamii, mdau mmoja wa utalii aliandika na kushauri haya kwa Nyaisa pindi alipoteuliwa: Alimshauri aondoe kasumba ya watu kuajiriwa kwa kujuana, aajiri watumishi wenye uwezo kama walioko BoT na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alishauri aanzishe mafunzo kwa vijana ambao anasema wengi hata sheria za kampuni hawazijui.

“Boresha mfumo wako ORS, bado una upungufu mwingi sana. Mfano, leo hii mtu akitaka kubadili MEMART ya kampuni yake bado hakuna standard nini kifanyike. Kampuni ikiwa na shareholder public haiwezi kwenda online, kampuni ikiwa na shareholder ambaye si individual au company – mfano NGO haiwi accommodated; kutana na wadau hasa mawakili na wahasibu wakusaidie kutatua changamoto. Rudisha Utumishi wafanyakazi wala rushwa na wasiojua kitu zaidi ya kuleta ukiritimba na dharau…BRELA inaweza kuwa kitovu kikubwa cha ukwepaji kodi hasa usipokuwa na wanasheria makini katika masuala ya company structure and restructure,” amesema mdau huyo.

BRELA ilianzishwa kwa Sheria Na. 30 ya mwaka 1997; na kuanza kazi rasmi Desemba 3, 1999. Watumishi wake ni 150; japo pia kuna wafanyakazi walioajiriwa kwa muda ambao ni 50.