Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Usajili wa Makampuni nchini (BRELA) imelenga kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya urasimishwaji.

Akizungumza katika maonyesho ya kimataifa ya viwanda yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba vilivyoko temeke, Dar es Salaam.

Afisa leseni wa asasi hiyo ya BRELA , Ndeyanka Mbowe amesema kuwa wao kama wasimamizi wa wafanyabiashara wamelenga kuboresha zaidi huduma ya utoaji elimu kwa wafanyabiashara ikiwa ni kufuatia mageuzi makubwa yaliyofanywa ambayo yataweza kurahisisha hatua za urasimishwaji ambapo watawawezesha wafanyabiashara kujisajili katika mfumo wa kidigitali.

“Tuko hapa katika Maonyesho ya Viwanda, BRELA kama wakala wa serikali ambayo tunashughulika na urasimishwaji wa biashara tumekuwa na majukumu msingi ambayo sisi tunayasimamia kama wakala.

Majukumu hayo yanatokatana sheria za msingi ambapo tunashughulika na kusajili makampuni, kusajili majina ya biashara, tunatoa hataza, tunasajili alama na huduma pamoja na kutoa leseni za viwanda katika daraja la kimataifa zinazosimamiwa na sera maalum.

“Tangu mwaka 2018 tulianza mageuzi ya kuanza kwenda katika mfumo wa kidigitali kwa maana tulianza kufanya urasimishwaji wa biashara kwa njia ya mtandaoni.

Tangu mwaka 2018 tumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwafikia wadau wetu ili kuwapa elimu ya usajili , urasimishwaji wa biashara na viwanda vyao pamoja ili waweze kuwa washindani katika soko la kitaifa na kimataifa “amesema.

Aidha pia afisa huyo ameongeza kwa kusema kuwa wamejipanga kuhakikisha wanatoa elimu kwa kushiriki katika maonyesho mbalimbali, kwa kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kukutana na walengwa wao na kuendelea kuwapa elimu juu ya urasimishwaji wa biashara zao .