Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa wito kwa wadau mbalimbali zikiweko Taasisi zinazosimamia Masuala ya Miliki Ubunifu kushiriki katika Maadhimisho ya siku ya Miliki Ubunifu Duniani ambayo yanatarajiwa kufanyika kesho jijini Dar es Salaam.
Maadhimisho hayo yenye Kauli Mbiu ya ‘Miliki Ubunifu na Malengo ya Maendeleo Endelevu: Kujenga mustakadhi wa pamoja kwa kutumia ubunifu’, lengo lake ni kukuza Vumbuzi na Bunifu mbalimbali kwa manufaa ya baadaye na kutambua mchango wa ubunifu katika kufikia maendeleo endelevu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 8, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka Brela, Loy Mhando amesema Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt .Ashatu Kijaji pamoja na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo.
“Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), lilianzishwa kwa lengo la kukuza na kulinda nyenzo za Miliki Ubunifu ikiwemo Vumbuzi kwa kutoa Hataza, alama zinazowekwa kwenye bidhaa na huduma, hakimiliki na hakishiriki,” amesema.
Amefafanua kuwa, Tanzania ni miongoni mwanachama wa WIPO ambapo imekuwa ikiunga mkono na kushiriki katika jitihada zinazofanywa na shirika hilo kwa kuhakikisha kuwa inakuza uelewa wa masuala ya Miliki Ubunifu pamoja na kuzilinda kisheria ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia na kukuza uchumi.
“Brela inawaalika wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Taasisi za umma pamoja na sekta binafsi ili kujadili kwa pamoja fursa, mafanikio na changamoto zilizopo katika nyanja ya Miliki Ubunifu.
“Vilevile baadhi ya wabunifu kutoka sekta mbalimbali watashiriki na kazi zao za Ubunifu zitaoneshwa. Pamoja na mambo mengine pia Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika eneo la Miliki Ubunifu baina ya Brela, Cosota na Taasisi nyingine zitasainiwa ikiwa ni njia ya kurasimisha ushirikiano uliopo baina ya Taasisi hizo katika kuhakikisha Miliki Ubunifu inaleta manufaa katika maendeleo ya kiuchumi na teknolojia nchini,” ameongeza.