Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Kisutu imetengua hukumu waliyoitoa ya kuwataka viongozi wa Yanga wakiongozwa na Rais Injinia Hersi Said kung’oka madarakani.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya wanachama kadhaa wa Yanga wakiongozwa na Mzee Magoma kufungua kesi katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, ambapo baadae upande wa Yanga walituma maombi kadhaa mahakamani hapo likiwemo la kupitia kesi na hukumu upya, ombi ambalo lilikubaliwa na kutekelezwa leo.

Akizungumza na wanahabari mapema leo baada ya kutoka Mahakamani, Wakili wa Yanga, Simon Patrick, amefafanua hoja nne walizoziwasilisha mahakamani ambapo tatu ndizo zilizowapa ushindi, huku moja ikikataliwa.

Hoja ya kwanza ni ile ya kwamba Mahakama hiyo ya Kisutu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, kwa mujibu wa sheria namba 318 ya mwaka 2002, masuala yote yanayohusiana na uhalali wa baraza la wadhamini yanapaswa kusikilizwa Mahakama kuu.

Hoja ya pili iliyokubaliwa ni ile ya Wanachama Fatma karume na Mzee Jabir Katundu kunyimwa haki ya kusikilizwa kufuatia Mzee Abeid kuwawakilisha Mahakamani bila ya wao kumpa kibali cha kisheria, mahakama imeona hoja hiyo ina mashiko na wameamua kuifutilia mbali hukumu.

Hoja ya tatu iliyokubaliwa Mahakamani ni namna Mzee Magoma na wenzake walivyowasilisha ombi la kesi hiyo kwa njia tofauti na iliyopaswa kuwasilishwa.

Hoja iliyokataliwa na Mahakama ni ile ya kumkataa Mzee Magoma kuwa hakuwa mwanachama halali wa Yanga wakati anafungua kesi, ambapo Mahakama imesema hoja hiyo inahitaji ushahidi hivyo wameitupilia mbali.

Wakili Patrick amesema Mahakama imewaamuru Mzee Magoma na wenzake kulipa gharama za usumbufu zitakazowasilishwa na klabu ya Yanga walizotumia katika kufuatilia kesi hiyo.

“Bado hatujapiga hesabu kupata gharama kamili tulizotumia ambazo ndizo tutaziwasilisha mahakamani, lakini kwa haraka haraka hazipungui Milioni 70 mpaka Mia, kesi ni gharama kubwa sana kwa sababu mawakili lazima walipwe, na mimi sikuwa pekeyangu kwenye hii kesi nimesindikizwa na mawakili kama sita” amesema Wakili Simon Patrick

Aidha Wakili Patrick amesema endapo Mzee Magoma na wenzake watashindwa kulipa gharama hizo, klabu ya Yanga itaenda kukamata mali alizonazo na kama hana mali zenye kufidia gharama zao, basi wataomba awe mfungwa mpaka pale atakapoweza kulipa gharama zao.