Kati ya mambo yaliyojadiliwa na wapenzi wa soka wiki iliyopita, ni pamoja na matokeo ya mechi ya watani wa jadi — Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club (Mnyama) ya jijini na Dar es Salaam Young Africans (Yanga) yenye makao yake mitaa ya Jangwani na Twiga, baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom uliopigwa katika Dimba la Taifa Dar es Salaam.

Katika kindumbwendumbwe hicho ambacho Yanga walikuwa wakiongoza kwa mabao 3-0 kabla ya Simba kusawazisha mabao yote kipindi cha pili, ilishuhudia baadhi ya mashabiki wakizimia uwanjani. Kuna habari pia za shabiki aliyeripotiwa kupoteza maisha.

Haya ni mambo ambayo mashabiki wanahitaji kuyavumilia kwa sababu kihistoria timu za Simba na Yanga zinapokutana mengi yanatokea, kwani kila upande hautaki kushindwa. Kwa ufupi mchezo wa soka una matokeo ya aina tatu — kushinda, kushindwa au kutoka sare.

Kwa kawaida baada ya mechi za watani hawa wa jadi huwa kuna mambo mengi timu inapoonekana kuwa imeshindwa kucheza vizuri au imefungwa, zikiwamo lawama.

Ni dhahiri kabisa kuwa katika mechi ya wiki iliyopita Yanga ndiyo wanaohitaji kujiuliza zaidi kilichotokea, baada ya Mnyama kusawazisha mabao yote kipindi cha pili na kuonesha kuwa kama muda ungeongezwa alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo.

Hivi karibuni kocha wa Yanga, Ernier Brandts (pichani), alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kwa sasa anataka kuwapumzisha wachezaji wakongwe na nyota katika timu hiyo na kuwapa nafasi wengine.

Wachezaji  ambao kocha huyo anawataja kuwasugulisha benchi ni Ally Mustapha ‘Barhtez’, Nadir Haroub ‘Canavaro’ na Athuman Idd ‘Chuji’.

Huu ni uamuzi ambao kocha huyo ameufanya akiwa na lengo la kuboresha kikosi chake katika Ligi hii, ambayo ina upinzani mkubwa kuliko miaka iliyopita. Lakini pia hapo kuna swali jingine la kujiuliza, je,  ameamua kuwapiga benchi wachezaji hawa  baada ya kucheza chini ya kiwango katika ya mechi ya Simba?

Brandts kama Kocha Mkuu wa Yanga alitakiwa kufafanua zaidi anachokiona kwa wachezaji hawa tangu kuanza kwa Ligi hadi hapa walipofikia, hali kadhalika alitakiwa kusema ni mechi ngapi wameonesha kiwango cha chini ili kuweka wazi chanzo cha uamuzi wake.

Kwa wale walioangalia mpambano huo, watakubali kuwa kilichowaponza Yanga ni kujiamini zaidi wakasahau kuwa mpira ni dakika 90. Tabia ya baadhi ya wachezaji kujiamini iliendelea kuonekana katika mechi yake dhidi ya Rhino (Nyati) Rangers ya tabora ambapo Yanga walishinda mabao 3-0 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumatano ya wiki iliyopita.

Kuna wachezaji kama Haruna Niyonzima, Mrisho Ngasa ambao walizidisha mbwembwe, hali ambayo iliwafanya mashabiki kuanza kuwazomea na kulalamika jukwaani, huku baadhi yao wakisema kuwa hayo ndiyo yaliyosababisha sare dhidi ya watani wao.

Pamoja na kuamua kuwa na mfumo mpya wa kuwaweka benchi nyota hao, kuna umuhimu wa Brandts kuangalia mambo kama haya yanayoonekana waziwazi na kuanza kufikia hatua ya kuwakera mashabiki.

 

0783 106 700