*Waziri wao ashangaa Watanzania kutochukua fursa waliyoiomba
*Ampongeza Rais Magufuli kubadili sheria za madini mwaka 2017
*Katibu Mkuu Madini asema Tanzania haina cha kujifunza Botswana

Na Mkinga Mkinga,
Aliyekuwa Gaborone, Botswana

Wakati Tanzania ikibadili sheria yake ya madini mwaka 2017, Botswana mambo ni tofauti, nchi hiyo inaongoza kwa kuwa na sheria nzuri ya madini pamoja na namna wanavyonufaika na vipengele vya kimkataba, ikilinganishwa na nchi nyingi za Kiafrika.
Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI katika nchi zote mbili umebaini kwamba ili kunufaika na madini lazima kuwepo na masuala kadhaa, hasa kuaminiana baina ya serikali na wawekezaji, uwazi wa mikataba na sera za nchi zinazotabirika.
Akizungumza katika mahojiano na Gazeti la JAMHURI jijini Gaborone, Botswana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya uchimbaji wa almasi ya Debswana, Balisi Bonyongo, amesema tatizo la nchi za Kiafrika ni kufikiri kuwa wawekezaji ni wezi.
“Dunia inasema kwamba tumefanikiwa katika kufanya biashara ya madini, lakini ukweli ni kwamba kufanikiwa kwetu kumekuja kutokana na serikali yenyewe kuwekeza katika rasilimali watu pamoja na kujenga imani kwa wawekezaji.
“Katika biashara kama hizi za uchimbaji, mtaji mkubwa baada ya rasilimali yenyewe (almasi) ni kuaminiana. Sisi tunahesabika kama tumefanikiwa kwa sababu tuko wazi na wawekezaji wanatambua masilahi ya nchi yetu. Masilahi ya nchi yetu hayayumbi…tumekuwa na mabadiliko ya uongozi bila kuathiri shughuli za uchimbaji.

“Hapa serikali ina mkono wake katika operesheni zote tunazozifanya… lakini huo ndio umekuwa utamaduni wetu. Hata bodi ya wakurugenzi hapa yenye wajumbe 13, wajumbe saba wanatoka kwa mwekezaji na wengine sita wanatoka serikalini,” amesema Bonyongo.
Kwa mujibu wa orodha ya wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ambayo mwandishi wa Gazeti la JAMHURI ameiona katika ofisi za Debswana, inaonyesha watumishi waandamizi na wenye kuaminika mbele ya jamii ndio huwakilisha masilahi ya umma katika biashara hiyo.

Akijibu swali kuhusu wajumbe wa bodi kutoka serikalini, mkurugenzi mtendaji huyo anasema: “Unajua hata mimi mwenyewe najua hapa nimebeba matumaini ya wananchi wenzangu, mapato yanayopatikana kutokana na uchimbaji ndiyo yanaendesha nchi, sisi hatuna bandari kama Tanzania.” Botswana inapakana na nchi za Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini na Namibia.
“Uchumi wetu kwa kiasi kikubwa sana unategemea madini pamoja na utalii, hivyo wajumbe wote wa bodi kutoka serikalini wanajua wajibu wao. Hata hao wawekezaji hawawezi kuingiza suala la rushwa… Serikali yetu inapinga vitendo vya rushwa,” amesema Bonyongo.

Ametaja jambo jingine kwamba ni kuhakikisha nchi inakuwa na uwazi katika mikataba ya madini. Mkurugenzi huyo anasema ni dhahiri kwamba madini ni mali ya wananchi wote, isipokuwa wachache wanakasimiwa mamlaka ya kusimamia.
“Unajua huwezi kuchukua wananchi wote wa Botswana milioni 2.8 hapa (Botswana) wakasimamia masuala ya mikataba ya madini, wala uzalishaji, isipokuwa sisi wawakilishi wachache ndio tunaingia huku na kusimamia masilahi yao,” amesema Bonyongo.

Bonyongo ambaye ni mtalaamu wa jiolojia, ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba amezisikia jitihada za Rais Dk. John Magufuli katika kuhakikisha wananchi wananufaika na madini, na zinamfurahisha.
“Nimesikia habari za Rais wenu (Magufuli), nadhani anahitaji kuungwa mkono. Kuvunja minyororo ya hao wawekezaji kunahitaji mshikamano wa kitaifa, halitakiwi kuwa jambo la mtu mmoja,” amesema.
Wakati Botswana ikionekana kunufaika na rasilimali zake na kujitegemea kiuchumi, Tanzania ni nchi yenye dhahabu, almasi na tanzanite, lakini bado uchumi wake unategemea misaada yenye masharti na mitego mingi kutoka kwa wahisani.
Waziri wa Nishati, Madini na Rasilimali Maji, Onkokame Mokaila, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, anasema nchi za Afrika zinatakiwa kujifunza kutoka kwenye uzoefu mzuri wa Botswana katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini ili kubadili mtazamo kwamba Waafrika hawawezi kupatana katika mikataba mikubwa ya rasilimali.
Waziri Mokaila ameliambia Gazeti la JAMHURI kwamba Serikali ya Botswana na mwekezaji, De Beers Group, waliingia mkataba wa miaka 10, mwaka 2011 na kwamba mkataba huo utadumu hadi mwaka 2021. Mkataba huo unahusu kuchambua, kuthamini na kuuza almasi inayochimbwa kupitia Kampuni ya Debswana.

Anasema sehemu ya makubaliano ya kimkataba yalihusisha Kampuni ya De Beers Group ambayo ni mbia, kuhamishia nchini Botswana shughuli zake za kuuza almasi ghafi, jambo ambalo linaifanya nchi hiyo kuwa moja ya nchi zinazonufaika kwa rasilimali. Mwaka jana Tanzania imepitisha sheria mbili za kuimarisha mapato ya nchi katika sekta ya madini.
Sheria hizo ni Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017, ambapo sheria hii inaweka utaratibu ambao wananchi kupitia chombo chao cha uwakilishi ambacho ni Bunge, kitapitia na kujadili makubaliano na mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi, ambayo imeingiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujiridhisha na masharti.
Sheria ya pili ni Sheria ya Mamlaka ya nchi Kuhusu Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017.  Sheria hii inaweka masharti yatakayohakikisha kwamba hatua yoyote inayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za taifa inatambua na kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama taifa huru lenye mamlaka ya kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa masilahi ya taifa.

Waziri wa Botswana, Mokaila, amesema mkataba huo ambao ulianza nchini humo Januari Mosi, 2011, ulikuwa mmoja wa mikataba mirefu zaidi iliyowahi kusainiwa baina ya Serikali ya Botswana na mbia.
“Kupitia mkataba huo wabia wetu Diamond Trading Company (DTC), itahamishia operesheni zake pamoja na wataalamu, ujuzi vifaa na teknolojia kutoka London hadi Gaborone.
“Botswana na De Beers tumefikia hatua kubwa katika uwekezaji baina ya serikali na sekta binafsi duniani. Mkataba huu na matokeo yake yanaisaidia Botswana kufikia malengo yake ya kuwa kituo bora katika uzalishaji na biashara ya almasi.
“Mkataba unatupatia uwezo wa moja kwa moja wa kulifikia soko, jambo ambalo ni muhimu sana kwa ustawi wa Botswana… tumeshuhudia ongezeko la ajira pamoja na fursa nyingine ambazo awali hatukuwa nazo. Haya yote yamefanyika kwa kuzingatia masilahi mapana ya nchi yetu (Botswana).
Katika mahojiano na Waziri Mokaila, amesema amewahi kusikia kwamba Tanzania inabadili sheria yake ya madini ili kunufaika zaidi. Kupitia dhamira hiyo, mamlaka hapa nchini ziliwasiliana na Serikali ya Botswana ili wataalamu kutoka Tanzania waende Botswana kujifunza, lakini ikaishia kuwa aibu.
“Unajua wakati naambiwa kuna mgeni kutoka Tanzania, nikasema nahitaji kuonana naye haraka, maana akilini mwangu nilikuwa nakumbuka barua kutoka Tanzania ikiomba kuja kujifunza hapa… hivi mmeshabadili sheria yenu ya madini?” amehoji Mokaila.

Katibu Mkuu: Hatuna la kujifunza Botwana

JAMHURI limemtafuta Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, kufahamu ilikuwaje Tanzania haikupeleka wataalamu Botswana wakajifunze, kama ilivyoomba mwaka 2016, naye akasema: “Sasa evolution (mabadiliko) za madini tumezifanya mwaka 2017, na hao hao Botswana wameomba kuja kujifunza kwetu… unajua kuwa na sheria ni kitu kingine na kuitekeleza ni kitu kingine.
“Sisi tumekuwa na sheria na tumeitekeleza effectively (kwa umakini), wao walikuwa na sheria lakini walikuwa hawajaitekeleza. Sasa walichokuwa wanakuja kujifunza kwetu ni how successful (kwa ufanisi) tumeitekeleza kwa muda mfupi… ni kweli wakati tunaanza kurekebisha sheria, tulijifunza nchi nyingi including (pamoja) na sheria yao.
“Kwa hiyo sasa hiyo ya 2016, leo mimi siwezi kuijibu wakati wizarani nimeenda mwaka jana. Na kama ingekuwa ni kesi, ningevuta mafaili nikaiangalia, lakini hii sioni kama ina umuhimu wowote. So far we are more successful than them (hadi sasa tumefanikiwa zaidi kuliko wao).”

Alipoulizwa iwapo tayari Tanzania imekwishaanza kuhifadhi madini yote Benki Kuu kama sheria inavyotaka na Botswana wanavyofanya, akasema: “So far (hadi sasa inafanya kazi. Individuals (watu mmoja mmoja) wanahifadhi madini yao Benki Kuu, lakini kama nchi hatujaanza kuitekeleza).
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, ameliambia JAMHURI kuwa yeye ni mgeni hapo wizarani, hivyo akaomba apewe muda kulifuatilia kufahamu nini kilitokea.

Madini ni uhai Botswana

Katika migodi yote ya almasi yameandikwa maneno ambayo yanawakumbusha watendaji wote umuhimu wa madini hayo kwa wananchi wa Botswana. Maneno hayo yanasomeka: “For our people, every diamond purchased represents food on the table; better living conditions; better healthcare; potable and safe drinking water; more roads to connect our remote communities; and much more.”
Maneno hayo yanamaanisha: “Kwa watu wetu, kila almasi inayouzwa inawakilisha chakula mezani, maisha bora, huduma bora za afya, maji safi na salama ya kunywa, barabara nyingi kuunganisha jamii yetu vijijini na mengine mengi,” maneno haya yalisemwa na aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus Mogae.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, mmoja wa Watanzania waishio Gaborone, Botswana, Julius Mutayoba, amesema Botswana haikufanikiwa kirahisi, kuna watu wamefanya kazi mpaka nchi imefikia hapo ilipo.
Amesema Botswana haikuwa katika mazingira rafiki sana baada ya kupata uhuru. Wakati wakoloni wa Kiingereza wakiondoka nchini humo, nchi hiyo ilikuwa na kilomita 12 tu za barabara ya lami na wahitimu 22 wa shahada ya chuo kikuu na 100 kutoka sekondari.

Mutayoba ameliambia JAMHURI kuwa mfumo wa sheria wa Botswana pamoja na masuala ya mikataba, nchi hiyo inafanya vizuri kwa kushirikiana na sekta binafsi.
“Ukiachilia mbali mapato mengi yanayotokana na almasi, hilo halijaweza kuathiri umoja na mshikamano wa kitaifa. Kwa kweli hawa jamaa wamejipanga sana na wananufaika. Nadhani hii ni nchi ambayo wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama mijini na vijijini kwa uwiano sawa,” amesema Mutayoba.

Mutayoba ambaye ameishi jijini Gaborone tangu mwaka 1998 akifanya kazi ya udaktari wa binadamu, anasema kuna wakati akikumbuka namna ambavyo Watanzania hawakuzingatia masilahi ya taifa na kusababisha hasara kwa vizazi kadhaa anaumia.
Tanzania bado inaweza kujifunza namna bora ya kunufaika na sekta ya madini kutoka nchi za Botswana, Namibia na Afrika Kusini, ili sekta hiyo iweze kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Sera ya madini ya Botswana inaeleza kwamba jamii inayozunguka migodi inapaswa kuwa mwanahisa wa mgodi husika na kwamba mwekezaji analazimika kujenga shule, hospitali na huduma nyingine za kijamii. Hapa kwetu kila halmashauri ya wilaya ulipo mgodi inapewa dola 300,000 (karibu Sh milioni 700) kwa mwaka.

Botswana imeweka utaratibu wa kuwafanya wawekezaji katika sekta hiyo kujenga viwanda vya kusafisha madini ndani ya nchi hiyo, jambo lililoisaidia kunufaika na rasilimali hiyo.
Kampuni ya Debswana, ambayo inashughulika na madini nchini Botswana, inamilikiwa kwa ubia baina ya serikali na mwekezaji De Beers kwa asilimia 50 kila mmoja. Ubia huo umekuwepo tangu kuanza kwa uchimbaji wa madini nchini humo.
Ubia huo unahusisha wabia wawili, Serikali ya Botswana pamoja na Kampuni ya Diamond Trading Company Botswana, inayomilikiwa na De Beers.
Wakati Serikali ya Botswana ikiendelea kula matunda ya rasilimali za nchi vizuri, Tanzania ndiyo kwanza imeshtuka na kubadili sheria ya madini ya mwaka 2010, iliyorekebishwa mwaka 2017, ili kulinda rasilimali hizo pamoja na kuhakikisha nchi inanufaika.

Sheria mpya ya madini imefuta na kubadilisha baadhi ya maneno au vifungu kutokana na mapendekezo ya kamati mbalimbali zilizohusishwa.
Katika sheria ambayo ilipitishwa na kusainiwa na Rais Dk. John Magufuli, inasema bayana kwamba makinikia hayatauzwa tena nje ya nchi, yatauzwa nchini na yatatozwa kodi. Sheria hiyo ilivunja Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) ulioanzishwa mwaka 2009 kusimamia mapato ya serikali kutoka sekta ya madini.
Katika sheria hiyo mpya, mamlaka ya Waziri wa Madini pamoja na Kamishna wa Madini yamepunguzwa ili kuongeza ufanisi na kuondoa urasimu uliokuwapo mwanzo. Sheria hiyo inaagiza kuanzishwa kwa kamisheni ya madini itakayokuwa na wajumbe tisa wakiwamo watatu wa kudumu, huku mwenyekiti wake akiteuliwa na mkuu wa nchi.
Baada ya kusainiwa kwa Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2017, baadhi ya kampuni zinazojihusisha na uchimbaji wa madini hapa nchini zilitoa taarifa za aidha kupunguza shughuli zao za uzalishaji au nguvu kazi, huku kampuni nyingine zikisitisha kabisa shughuli zake.

Kampuni ya uchimbaji wa almasi ya Petra Diamonds ilitangaza kusimamisha shughuli zake za uchimbaji katika mgodi wake uliopo Mwadui Shinyanga, Septemba mwaka jana.
Hatua ya kampuni hiyo kusimamisha shughuli zake za uchimbaji wa almasi, ilikuja baada ya kamati za Bunge kuwasilisha ripoti kwa Rais Dk. John Magufuli kufuatia uchunguzi walioufanya katika sekta ya uchimbaji wa madini ya almasi na tanzanite.
Hata baada ya kuwepo kwa tishio hilo, bado Rais Magufuli aliitangazia dunia kwamba haogopi kufunga shughuli zote za uchimbaji wa madini nchini ili kurekebisha mikataba iliyopo.
“Iwapo ni kuanza upya, basi tufanye hivyo. Na iwapo madini yetu mengi yameibwa, basi na tufunge migodi. Pengine watoto wetu na wajukuu wetu watakuwa na akili zaidi na watakuja kuifanya biashara hii badala ya kutazama tu madini haya yakiibwa,” alinukuliwa Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI jijini Gaborone hivi karibuni, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Dk. Stargomena Tax, anasema msingi wa nchi ya Botswana kunufaika na rasilimali zake ulianzishwa na mwasisi wa nchi hiyo, Sir Seretse Khama.
“Ukitaka kufahamu vizuri zaidi kuhusu namna Botswana ilivyojiandaa katika rasilimali zake hasa madini, nakusihi upate hotuba ya mwasisi wa taifa hili, Sir Seretse Khama. Misingi aliyoiacha imekuwa nguzo imara kwa taifa hili ambalo kwa hakika wananufaika na madini.

Debswana Diamond Company Ltd, ni kampuni ya ubia wa pekee baina ya Serikali ya Botswana na De Beers Group of Companies. Shirika hilo lilianzishwa Juni mwaka 1969, chini ya jina la asili la De Beers Botswana Mining Company ambaye ndiye alikuwa mmiliki.
Machi 1992, jina la kampuni lilibadilishwa na kuwa Debswana Diamond Company, huku kampuni hiyo ikiwa na majukumu ya uchimbaji wa almasi pamoja na kuchakata.
Kampuni hiyo inaendesha migodi minne ambayo ni Demtshaa (maarufu kwa jina la Maji ya Kobe), mgodi huo uligundua madini ya almasi kati ya mwaka 1969 hadi 1972 katika eneo lenye umbali wa kilomita 20 kutoka mashariki mwa mji wa Orapa Kimberlite.

Mgodi wa Demtshaa umepakana na ule wa Letlhakane uliopo eneo la Orapa. Uchunguzi wa awali ulionyesha mgodi huo utaweza kuzalisha carats milioni 5 kutoka kwenye tani milioni 39 za miamba ya madini ambayo ilitarajiwa kuchimbwa kwa miaka 31, mwaka 2014 carats nyingine 300,000 ziligunduliwa.
Mgodi huo ulizinduliwa rasmi Oktoba 2003 na aliyekuwa Makamu wa Rais wa wakati huo, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama. Wakati anazindua mgodi huo alinukuliwa akisema: “Mgodi wa Damtshaa ni nyongeza katika kuimarisha na kuunganisha nguvu zaidi katika taifa linaloongoza kwa kuzalisha almasi.”
Mgodi mwingine ni ule wa Letlhakane, ambao uko umbali wa kilomita 50 kutoka ofisi za Debswana na kilomita 190, magharibi mwa mji wa Francistown, mpakani na nchi ya Zimbabwe. Mgodi huo uligunduliwa wakati wa kuchukua sampuli na kufanya mchakato wa uthamini huko Orapa, na baadaye ukageuka kuwa mgodi wa pili kwa ukubwa na ukafunguliwa rasmi mwaka 1975. Itaendelea wiki ijayo.

Uchunguzi huu umefanywa kwa ushirikiano kati ya Gazeti la JAMHURI na Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).