Benki Kuu ya Tanzania (BoT),imebaini kuongezeka kwa udanganyifu wa fedha nchini
unaohusisha mwananchi kupokea taarifa(hati au barua pepe) inayodai kuwa ni uthibitisho wa malipo kupitia SWIFT na/au mifumo mingine ya uhamishaji
fedha.
Mpokeaji anafahamishwa kuwa fedha zimeingizwa kwenye benki au akaunti katika taasisi ya fedha nchini Tanzania; wakati mwingine, mpokeaji fedha anaelekezwa kulipa kiasi fulani cha fedha kuwezesha kupata fedha hizo nyingi.
Matukio mengi ya taarifa hizo yanahusisha kiasi kikubwa cha pesa kinachodaiwa kuletwa kwa ajili ya ufadhili wa mradi au matumizi binafsi.
Hivyo, Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutaarifu umma kwamba taarifa hizo ni za kughushi na za kubuni. Wananchi mnashauriwa kuwa waangalifu na kuacha kujihusisha na miamala hiyo ambayo kwa kawaida inalenga kuwatapeli fedha.Pia, wananchi mnakumbushwa kuzingatia kanuni bora za kufanya miamala ya fedha ili kuepuka upotevu wa fedha ambazo ni:
i.Kuhakikisha usalama wa taarifa za fedha wakati wa kutoa taarifa binafsi
mtandaoni (tovuti, mitandao ya kijamii), kupitia barua pepe au kwenye
simu;
ii.kutojihusisha kujibu barua pepe, barua au simu zinazoahidi kupokea
fedha kutoka kwa watu au kampuni wasizozifahamu vizuri;na
iii.kuwa waangalifu mnapofanya malipo ya mtandaoni kwa kufanya uhakiki
wa mshirika wa kibiashara (mtu au kampuni) kabla ya kutoa maelezo au
kufanya malipo.
Aidha, wananchi waliokumbwa na matatizo hayo wanashauriwa kutoa taarifa
kwenye vyombo vya usalamakwa hatua stahiki.