Benki kuu ya Tanzania (BoT), imetoa mafunzo ya kutambua noti halali kwa watu wa makundi maalumu wakiwemo wasioona,wenye ulemavu wa macho na viungo.

Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Meneja Msaidizi Sarafu,Joyce Saidimu,alisema kuwa lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuyawezesha makundi hayo kupata uelewa wa kutosha wa kuzijua alama za usalama kwenye sarafu ili kuweza kugundua fedha halali kwani ni makundi ambayo yamekuwa yakisahaulika katika maswala mbalimbali.

Saidimu alisema kuwa,wameona umuhimu mkubwa wa kutoa mafunzo kwa makundi hayo ili waweze kuzitambua fedha halali na kuepukana na matumizi ya fedha bandia kutokana na changamoto walizonazo,na hatimaye kuweza kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ili na wengine ambao hawajafikiwa waweze kufikiwa kupitia wao.

Meneja Msaidizi Sarafu kutoka Benki Kuu ya Tanzania,Joyce Saidimu akizungumza katika mafunzo hayo jijini Arusha. 

“Sisi kama Benki ni utaratibu wetu kutoa mafunzo kama hayo mashuleni, sokoni na kwenye maeneo mbalimbali ya biashara, ila kwa awamu hii tumeamua kutoa elimu kwa watu wa makundi maalumu ili waweze kupata uelewa wa kutosha na kuzitambua noti halali.

“Mafunzo haya yatakuwa endelevu na tutakuwa tukiyatoa mara kwa mara ili waweze kupata uelewa wa kutosha juu ya maswala haya na kuepuka kushikishwa fedha bandia kwani tayari wana uelewa wa kutosha”, alisema Saidimu.

Aidha wameweza pia kutoa mafunzo ya namna sahihi ya kutunza fedha kwa ajili ya matumizi yao huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa kufundisha wenzao namna ya kutunza fedha.

Akizungumza baada ya mafunzo hayo ,Katibu Mtendaji wa shirika la maendeleo ya jamii na viziwi (DCPO),Jafari Shabani alisema kuwa ,waliomba kupatiwa mafunzo hayo kwa watu wenye ulemavu kutokana na changamoto mbalimbali walizokuwa wakikabiliana nazo katika kuzitambua noti bandia na halali,ambapo jumla ya watu wenye mahitaji maalumu 70
wameweza kupatiwa mafunzo hayo.

Jafari alisema kuwa, watu hao wenye mahitaji maalumu walikuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo na hata kupelekea wengi wao kupelekwa katika vyombo vya usalama pindi wanapokutwa na noti bandia kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya utambuzi wa alama za usalama kwenye sarafu.

Katibu Mtendaji wa Shirika la maendeleo ya jamii na viziwi (DCPO),Jafari Shabani akizungumza kuhusiana na mafunzo hayo.

Kwa upande wake ,Mshiriki wa semina hiyo Emmanuel Benjamini ameishukuru Benki Kuu kwa mafunzo hayo kwani hapo awali alikuwa akishikishwa sana noti bandia kutokana na biashara yake ya kuendesha Bajaji ila kutokana na elimu hiyo sasa wataweza kuchukua tahadhari mapema.

Aidha aliomba mafunzo hayo kuwa endelevu huku akiomba serikali kutoa mafunzo zaidi kwa watu wenye ulemavu kwani itasaidia sana kuona wanashirikishwa na kuondoa dhana ya kutatua