Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema inaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya maofi sa wa Kampuni ya Leo Beneath London (LBL) wanaodaiwa kujihusisha na ulaghai ukiwamo wa kupokea amana, kutoa riba na kufanya uhaulishaji wa fedha bila kuwa na leseni.

Taarifa ya Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba imeeleza kuwa benki hiyo haijafanya mazungumzo wala kutoa maelekezo yoyote ya kupewa leseni au kuruhusiwa kwa kampuni hiyo tofauti na taarifa zinazosomeka mitandaoni.

Tutuba alihadharisha wananchi kujihusisha na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye anatoa huduma za kifedha bila kuwa na leseni ya Benki Kuu au wasimamizi wengine wa huduma za fedha.

“Benki Kuu inawaonya watu na taasisi ambazo zinatumia jina la Benki Kuu kuuhadaa umma katika vitendo vyao vya kihalifu, kuacha kufanya hivyo vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” ameeleza Tutuba.

Aidha, amewahimiza wananchi wanaotaka kupata huduma za kifedha watumie taasisi zenye leseni ambazo orodha yake inapatikana kwenye tovuti ya BoT au wasimamizi wengine wa sekta ya fedha nchini.