Wamo Salama Ali Hassan Mwinyi, Filbert Tluway Sumaye, Zaria Rashidi Kawawa, Blasia William Mkapa, Harriet Matern Lumbanga, Pamela Edward Lowassa, Rachel Muganda, Salma Omar Mahita, Justina Mungai, Kenneth Nchimbi, Violet Philemon Luhanjo, Liku Kate Kamba, Thomas Mongella na Jabir Abdallah Kigoda.

 

Malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali yanaendelea kutawala kwenye mitandao ya kijamii, kutokana na “upendeleo” wa ajira na vyeo kwa watoto wa vigogo serikalini, taasisi nyeti, mashirika ya umma na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).



 

Malalamiko hayo yaliibuliwa wakati fulani kuhusu ajira za watoto wa vigogo hao katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini yakazimwa na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, aliyesema wameajiriwa kulingana na sifa zao za elimu.



Mjadala umekuwa mkali baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kutoboa hadharani kwamba watoto wengi wa vigogo wameajiriwa kwenye Kitengo cha Mizani, kwa namna inayotia shaka.


Upendeleo kwa watoto wa wakubwa unajadiliwa pia kwanye taasisi za kifedha na kwingineko kwenye mianya ya ulaji; hali ambayo inawakwaza watoto wanaotoka katika famili zisizokuwa na majina makubwa.


Hadi sasa, majina yanayovuma ya watoto hao ndani ya BoT ni ya Pamela Edward Lowassa, Filbert Tluway Sumaye, Zaria Rashidi Kawawa, Harriet Matern Lumbanga, Salama Ali Hassan Mwinyi, Rachel Muganda, Salma Omar Mahita, Justina Mungai, Kenneth Nchimbi, Blasia William Mkapa, Violet Luhanjo, Liku Kate Kamba, Thomas Mongella na Jabir Kigoda.


Kati ya hao, Mungai aliondolewa baada ya kubainika kwamba hakuwa na sifa za kufanya kazi katika taasisi hiyo kubwa ya fedha hapa nchini. Kadhalika, Salma Mahita aliacha kazi baada ya kuolewa na Baraka Munisi na kwenda kuishi nchini Marekani.


Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa baada ya Salma kuondoka, sasa imekuwa zamu ya Munisi kuajiriwa BoT. Ameajiriwa kama Mortgage Finance Specialist.


Pamela Lowassa: Huyu ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. Mtoto huyo anafanya kazi katika Idara ya Kumbi za Mikutano.


Filbert Sumaye: Amezaliwa na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye. Yupo kwenye Idara ya Mfumo wa Malipo (National Payment System).


Zaria Rashidi Kawawa: Huyu ni mmoja kati ya watoto wa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanganyika, na baadaye Tanzania, Rashidi Mfaume Kawawa. Binti huyu anaongoza Idara ya Uhusiano BoT.


Harriet Matern Lumbanga: Amezaliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Matern Lumbaga. Anafanya kazi katika Idara ya Mabenki.


Salama Ali Hassan Mwinyi: Ni binti wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan Mwinyi. Yupo katika Idara ya Mfumo wa Malipo.


Rachel Muganda ni shemeji wa aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Ballali. Anaendelea na kazi katika Idara ya Masoko ya Ndani.


Salma Omar Mahita: Ni binti wa Omar Mahita ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu. Alipata kazi wakati huo baba yake akiwa hajastaafu. Amewahi kufanya kazi BoT kabla ya kuolewa na kwenda kuishi nchini Marekani. Hata hivyo, mumewe aitwaye Munisi “ameziba nafasi hiyo” kwa kuajiriwa katika Idara ya Mpango Mkakati.


Justina Mungai: Ni mtoto wa Joseph Mungai, ambaye amepata kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri kuanzia Awamu ya Kwanza hadi Awamu ya Tatu. Aliondolewa BoT baada ya kubainika kuwa hana sifa.


Kenneth Nchimbi: Kenneth amezaliwa tumbo moja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi. Kazi yake ni Mhasibu.  Blasia William Mkapa: Ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa. Huyu anafanya kazi katika Ofisi ya Gavana.


Violet Luhanjo:  Violet amezaliwa na Philemon Luhanjo, ambaye ni hivi karibu tu amestaafu wadhifa wa Katibu Mkuu Kiongozi. Binti huyu ambaye ni mwanasheria kitaaluma anafanya kazi katika Idara ya Sheria.


Liku Kate Kamba: Liku ni mtoto wa mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini, Mama Kate Kamba. Kamba amewahi kufanya kazi mbalimbali tangu Awamu ya Kwanza, na wadhifa wa karibuni kabisa aliokuwa nao ni wa ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki.


Thomas Mongella: Thomas ni mtoto wa Mama Gertrude Mongella, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri wakati wa Awamu ya Kwanza.

 

Ameshakuwa Katibu Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Wanawake Duniani uliofanyika jijini Beijing, China. Ameshakuwa Rais wa Bunge la Afrika; na pia Mbunge wa Ukerewe mkoani Mwanza. Thomas anafanya kazi katika Idara ya Usimamizi wa Mabenki.


Jabir Kigoda: Ni mtoto wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda. Ndani ya BoT anafanya kazi katika Idara ya Huduma za Ndani.


Katika mjadala mkali unaoendelea kwenye mitandao ya kijamii, mmoja wa wachangiaji amehoji, “Ninachojiuliza na sipati majibu mpaka sasa ni hiki, kama imetokea coincidence (bila kutarajia) BoT ikaajiri watoto 14 wa vigogo; je, coincidence hiyo hiyo inaweza kutokea kwenye Wizara ya Elimu watoto wenye majina kama hayo hayo wakapangwa kwenda kufundisha shule za kata vijijini, ambako hakuna maji wala umeme na wakaendelea kuifanya kazi hiyo kwa moyo wa kizalendo bila kujali kuwa mishahara imechelewa na hawajapandishwa vyeo; na wakati huo huo wakiidai serikali sikivu malikimbizo?


“Hivi kweli binadamu wote ni sawa kwa maana ya fursa za ajira bila kuangaliana usoni, hasa BoT?”


Mbali ya BoT, mjadala kama huo unaendelea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako baadhi ya wanachama na wafuasi wanalalamika kwamba chama kimeanza kubadilika na kuwa cha kisultani (cha kurithishana vyeo).


Mfano unaotolewa ni wa nafasi nono ndani ya Umoja wa Vijana (UVCCM) ambako majina ya watoto wa vigogo ndiyo yanayong’ara. Majina hayo ni ya Dickson Membe, Freddy Lowassa, Ridhiwani Kikwete, Ashura Hussein Mwinyi, Ben Samuel Sitta, Debora Mwandosya, Irene Mizengo Pinda, Felister Job Ndugai, Christopher Ndejembi, Sharifa Gharib Bilal, Hawa Abdallah Kigoda, Judith Wilson Mukama; Jalome Pius Msekwa na wengine wengi.


Aidha, kumeibuka mjadala mkali baada ya baadhi ya wananchi kuhoji uhalali wa ukoo wa Kikwete kuteka siasa za Wilaya ya Bagamoyo; huku mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani na mke wa Rais, Mama Salma, wakipita kwenye ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) bila kupingwa.


Kwa BoT, Gavana Ndulu anasema watoto wa vigogo wanaodaiwa kuajiriwa kinyemela wamebainika kuwa na sifa stahili. Kauli ya Ndulu inatokana na kukamilika kwa uchunguzi uliolenga kumaliza utata uliopo kuhusu ajira za watoto wa vigogo.


Profesa Ndulu alisema mchakato wa uchunguzi uliendeshwa kwa uwazi na umakini, na kwamba watoto wanane kati ya 18 wanaofanya kazi za kitaaluma wote wana sifa.


Alisema kabla ya mwaka 2005 kulikuwa na vigezo tofauti na baada ya mwaka huo, walioajiriwa baadaye mwaka 2006/2007 walipaswa kuwa na vigezo vipya tofauti na vile vya mwaka 2000 hadi 2005.


Profesa Ndulu alisema kabla ya mwaka 2005, kazi za kitaaluma kigezo kikuu kilikuwa ni shahada ya kwanza, lakini baada ya mwaka huo kigezo kikawa ni shahada ya uzamili.


“Kwa hiyo, watoto hao wanane mnaoita wa vigogo wote walikuwa na basic entries (sifa za kujiunga), waliajiriwa kwa vigezo stahili, ambavyo kipindi hicho ilikuwa ni shahada ya kwanza, lakini pia waliendelea kusoma na kuweza kufikia shahada ya uzamili ambayo ni kigezo cha baada ya mwaka 2005,” alisema Profesa Ndulu.

 

BoT katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 chini ya uongozi wa Gavana Ballali, ilikumbwa na tuhuma mbalimbali, zikiwamo za watoto wa vigogo kuajiriwa katika mazingira yaliyotiliwa shaka.