Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema haiwezi kufanya chochote kumsaidia mfanyabiashara aliyeibiwa fedha kwenye akaunti yake katika Ecobank, Tawi la Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Mahakama Kuu ya Tanzania (Divisheni ya Biashara) imeitia hatiani Ecobank Tanzania Limited kwa kumwibia mteja wake, Kampuni ya Future Trading Limited, Sh milioni 66 kutoka kwenye akaunti yake.
Fedha hizo zimeibwa kwenye akaunti hiyo kupitia huduma ya Internet Banking na kuziingiza katika akaunti iliyoko nchini Afrika Kusini.
Hukumu hiyo ya kesi namba 68 ya mwaka 2014, imetolewa na Jaji Barke Sehel. Inahusu wizi huo uliofanywa kwenye benki hiyo Tawi la Uhuru katika akaunti Na. 0010135400019801 ya Kampuni ya Future Trading Limited.
Kampuni ya Future Trading Limited baada ya kuona hailipwi fedha zake, Desemba 3, mwaka jana iliiandikia BoT barua ikiomba iingilie kati ili iweze kulipwa.
Machi 18, mwaka huu, Kurugenzi ya Huduma za Kisheria ya benki hiyo iliijibu Future Trading Limited, ikisema:
“Baada ya kuyapitia malalamiko haya, kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Mwongozo wa Kutatua Malalamiko Dhidi ya Taasisi za Kibenki, 2015, ambao unaelekeza namna ya kutatua malalamiko dhidi ya taasisi za kibenki, imeonekana kwamba malalamiko haya hayana sifa ya kuwasilishwa Benki Kuu.
“Kwa mujibu wa masharti muhimu katika mwongozo, malalamiko husika, kabla ya kuwasilishwa kwenye dawati, yasiwe yamefikishwa mahakamani au kwenye chombo chochote cha uamuzi (tribunal).”
Barua hiyo iliyosainiwa na P. Luena na Geofrey Sikira, imehitimisha kwa kuiambia kampuni hiyo: “Kwa kuwa malalamiko haya yalishafikishwa na kutolewa hukumu mahakamani, Benki Kuu haiwezi kuingilia na kufanya chochote katika malalamiko haya. Tunakushauri kuwa unaweza kupata haki yako hapo kupitia mahakama kwa mujibu wa taratibu za kisheria.”
Mkurugenzi wa Future Trading Limited, Abubakar Suweid, amezungumza na JAMHURI na kueleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa BoT.
“Nilikwenda BoT nikiamini kuwa wao kama wasimamizi wakuu wa hizi benki wangeweza kuielekeza Ecobank inilipe.
“Hili lingekuwa jepesi kwa sababu kazi kubwa ya kuthibitisha kufanywa kwa wizi huu imeshafanywa na mahakama kwa kuwatia hatiani. Kilichotakiwa ni kuiagiza benki inilipe badala ya danadana na usumbufu ninaopata sasa.
“Miaka yote hii nimekuwa kwenye wakati mgumu. Nina mikopo kwenye benki nyingine, nimeshindwa kuilipa kwa sababu fedha zote zimeibwa Ecobank. Mahakama iliona namna wafanyakazi wa benki hiyo walivyoshiriki kuniibia. Sasa kama BoT hawawezi kushughulikia suala kama hili, basi wanyonge hatuna haki,” amesema.
Ecobank Tanzania Limited imetakiwa imlipe mlalamikaji Sh milioni 66.24 ambazo zilihamishwa kinyemela kutoka kwenye akaunti ya mteja huyo kwenda kwa mtu asiyeidhinishwa.
Pili, Ecobank Tanzania Limited imlipe mlalamikaji Sh milioni 25 ikiwa ni malipo ya fidia kwa madhara yaliyotokana na benki husika kufanya malipo bila idhini ya mteja.
Tatu, Ecobank imeamriwa imlipe mlalamikaji riba ya kiwango cha asilimia saba kuanzia siku ya hukumu hadi itakapokuwa imemaliza kulipa deni hilo.
Nne, mteja arejeshewe gharama za uendeshaji wa kesi.
Katika kesi hiyo, shahidi kwa upande wa mlalamikaji, Suweid, aliieleza mahakama kuwa alibaini wizi huo Machi 13, 2014.
Alisema alipigwa butwaa baada ya kubaini Sh milioni 66.24 zimehamishwa na alipoutaarifu uongozi wa benki alielezwa kuwa fedha hizo zimehamishwa na kupokewa nchini Afrika Kusini kwa njia ya ‘telegraph transfer’ kupitia maelekezo ya kielektroniki yaliyokuwa yakitolewa na barua pepe ya mlalamikaji iliyosajiliwa katika benki hiyo.
Suweid amesema kwamba hakuna popote ambako alisaini kuidhinisha uhamishaji huo wa fedha na wala hakutumia mfumo wa kielektroniki kufanya mawasiliano.
Amesema pamoja na malalamiko yake, benki hiyo iligoma kurejesha fedha hizo. Ecobank imepata zuio la muda la mahakama linaloinyima haki Kampuni ya Future Trading Company Limited kukamata na kunadi mali za benki hiyo.