*Anaswa na kilo 50 Nairobi, zinafanana na za wanamuziki

*‘Unga’ wagonganisha majaji, mahakamani watafutana

Wakati Mahakama Kuu ikituhumiwa kuharibu mwenendo wa kesi za dawa za kulevya nchini kwa kutoa hukumu zinazopingana na sheria zilizotungwa na Bunge, mtu anayetuhumiwa kuwa ndiye aliyewapatia mzigo wa kilo 180 za dawa za kulevya wanamuziki, Agnes Jerald (Masogange) na Melisa Edward waliokamatwa Afrika Kusini Julai 5, naye amekamatwa na ‘unga’.

Masogange na Edward walikamatwa katika Uwanja ndege wa Oliver Thambo, Afrika Kusini wakiwa na mabegi tisa yanayofanana ndani yake yakiwa yamebeba dawa za kulevya aina ya methamphetamine, kwa taarifa za kiuchunguzi lilizozipata JAMHURI, mtu aliyetambulika kwa jina la Rumishaeli Mamkuu Shoo anayedaiwa kuwa bosi wa akina Masogange amekamatwa Nairobi, Kenya.

 

“Amekamatwa jana (Alhamisi, Agosti 29) jijini Nairobi akiwa na dawa aina ya methamphetamine kilo 50,” chanzo cha uhakika kililijulisha JAMHURI. “Pamoja naye, amekamatwa akiwa na mtu mwingine anayeitwa January Gabriel Liundi wakiwa na gari aina ya Rav4 nyeusi Na T 410 CLF.” Chanzo kingine kilisema dawa walizokamatwa nazo ni ephedrine ambazo hutumika kutengeneza methamphetamine.

 

Uchunguzi unaonyesha kuwa kabla ya Shoo kukamatwa mama yake alikuwa anahaa makao makuu ya polisi na Mkoa wa Kipolisi Ilala akiomba Shoo asiangukie mikononi mwa Kamanda Godfrey Nzowa wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya. “Yule mama alikuwa analia anasema Nzowa akimkamata atamweka ndani,” kilisema chanzo chetu.

 

JAMHURI lilipowasiliana na Nzowa, alikiri kusikia taarifa hizo ila akasema atazizungumzia zaidi baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Jeshi la Polisi Nairobi. “Nimezisikia, na ni kweli tulimkamata Julai 7 baada ya kuwa wale mabinti (Masogange na Edward) wamentaja, hatukumkuta na mzigo ila tukamweka chini ya uangalizi, na sasa kabla hajaja kuripoti, nimepata taarifa kuwa amekamatwa na ndawa hizo Nairobi. Nitawajulisha nikipata taarifa kamili,” alisema Nzowa.

 

Wakati bosi wa Masogange akinaswa, JAMHURI limepata hukumu mbili zinazoonyesha Mahakama inavyopingana wazi nchini kuhusiana na kesi za dawa za kulevya.

 

iliyotolewa na Jaji Upendo Msuya, ndiyo inaumiza vichwa wanasheria na Serikali kwa Ujumla, kwani imekinzana wazi na Sheria ya nchi kwa kutumia sababu dhaifu za kisheria. Katika kesi iliyowahusisha Watanzania wawili na Wapakistani wawili; Fredy William Chonde, Kambi Zuberi Seif, Abdul Ghan Peer Bux na Chambaz Malik, Jaji Upendo Msuya alitoa dhamana kwa kosa lisilodhaminika.

 

Jaji Msuya katika kesi hii ya mwaka 2011, alisema alitumia Ibara ya 148 (5) (a) (iii) kuwaachia watuhumiwa hao waliokuwa na jumla ya kilo 179 za heroine iliyokadriwa kuwa na thamani ya Sh 6,265,000,000 kwa maelezo kuwa Kamishna wa Kamisheni ya Kuzuia Dawa za Kulevya nchini hakuambatanisha cheti cha thamani iliyothibitishwa ya mzigo uliokamatwa.

 

Hawa walikamatwa Februari 2011 katika Mtaa wa Jogoo, Mbezi Beach uliopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

 

Pia alisema katika hati ya mashitaka, walalamikaji hawakuweka umri wa walalamikiwa, hivyo akakubaliana na hoja za mawakili wa walalamikaji Michael Mwambeta na Yasin Memba akawapa dhamana na kuagiza warejeshewe hati zao za kusafiria. Siku hiyo hiyo, Wapakistani walikimbia nchi na Watanzania wawili inaelezwa kuwa nao kuna nyakati walikimbilia Afrika Kusini.

 

Sura ya 27 (1) (a) ya Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya, inatamka bayana kuwa mtu aliyekutwa na heroine au cocaine na dawa za kulevya nyingine zilizoorodheshwa hapaswi kupewa dhamana, lakini Jaji Msuya alisema kukosekana kwa hati ya Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya yenye kuonyesha thamani, inaweza ikawa ishara ya watu hawa kubambikiwa kesi hivyo akaamuru waachiwe huru.

 

Upande wa mashitaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Mangowi na Mfikwa, ulisema kuwa sheria inataka watuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 na hivyo uchunguzi ulikuwa bado unaendelea, na wakaomba kuwa hivyo vyote vinavyodaiwa kuwa vinapungua wangeviwasilisha wakati wa hatua ya awali ya kusikiliza kesi, lakini Jaji Msuya akasema hakubaliani nao kwani hilo likiruhusiwa linaweza kuruhusu raia wema kubambikiwa kesi.

 

Wakati Jaji Msuya akitoa humu ya aina hiyo, Jaji mwenazake Kipenka Mussa, alipingana wazi na Jaji Msuya katika kesi dhidi ya Ramadhani Athumani Mohamed, Ally Mohamed Abdallah, Issa Abdallahman Soud na Rashid Mohamed Flashman, iliyotolewa Septemba 9, 2011.

 

Watuhumiwa hawa ambao wako rumande hadi sasa, walikutwa na kilo tatu za Cocaine zenye thamani ya Sh milioni 202,500,000. Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, ilikuwa imewapatia dhamana kwa kutumia kigezo cha hukumu iliyotolewa na Jaji Msuya awali, kwa mazingira yale yale kuwa washitakiwa walipofikishwa mahakamani dawa walizokamatwa nazo hazikuwa na hati ya kuthibitisha thamani ya dawa hizo kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Dawa za Kulevya Nchini.

 

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alikata rufaa kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Tanga kupinga dhamana hiyo, kwa maelezo kuwa kosa la kukutwa na dawa za kulevya kwa mujibu wa sheria iliyotajwa hapo juu halina dhamana, lakini pia kwa maelezo kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa kesi ambazo haina uwezo wa kuzisikiliza na hazidhaminiki.

 

Akitoa hukumu yake, Jaji Mussa alisema kwa masikitiko analazimika kupingana na hukumu ya Jaji mwenzake Msuya, ambayo ilitafsiri sheria bila kuangalia nia ya wabunge wakati wanatunga sheria hiyo. Alisema pia kwa mazingira ya watuhumiwa kutakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 na ukubwa wa Tanzania kusema kuwa ndani ya muda huo Kamishna awe ametoa hati ya thamani ya dawa za kulevya nchi nzima ni kujidanganya.

Jaji Mussa alisema nia ya msingi ilikuwa ni kutoa adhabu kali itakayozuia watu kufanya biashara ya dawa za kulevya zenye madhara makubwa kwa taifa na kizazi chote kwa ujumla, hivyo akafunga dhamana ya watuhumiwa haya na kuagiza sheria hiyo ya irekebishwe kufuta kifungu cha kutaka hati ya thamani kutolewa kwani kinasaidia wahalifu kuendelea kufanya biashara hii.

 

Hadi sasa Mahakama haijatoa chapisho maalum kubainisha ni hukumu ipi iko sahihi kati ya ile ya Jaji Msuya na hii ya Jaji Mussa hali inayowafanya mahakimu na watumishi wa mahakama kuchagua hukumu ya kutumia wanayoona inawafaa kulingana na matakwa yao au ya kisheria.

 

Pamoja na mgongano huo mahakamani, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka.

Wakati vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana.

 

Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.

 

Wakati kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.

 

Katika hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo halizingatiwi. JAMHURI halikubahatika kufahamu bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.

 

Wakati polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji mahakamani.

 

Habari za kuaminika zilizolifikia Jamhuri, zinaeleza kuwa kesi nyingi sasa zimepangiwa majaji zianze kusikilizwa baada ya JAMHURI kulipua kadhia hii na Serikali inajiandaa kuunda Mahakama Maalum ya Kesi za Dawa za Kulevya. Hili atalitangaza Rais Jakaya Kikwete muda wowote akirejea nchini kutoka safarini Ulaya.

 

Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI limekuwa likichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza hadharani majina ya wauza unga 504 katika matoleo manne yaliyotangulia.