*CAG aanika madudu mengine mapya
*Omo, Blueband, mafuta ya ndege hatari
*Pikipiki feki, vinywaji hatari kwa walaji
*Aruhusu Kobil wachakachue mafuta

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametoa taarifa ya ukaguzi maalumu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na kuibua mambo ya hatari zikiwamo kampuni za mawaziri zinazoingiza mafuta ya magari yasiyofaa.

Ukaguzi huo umeanika pia orodha ya kampuni zilizoingiza bidhaa zisizofaa nchini kwa matumizi ya binadamu, lakini TBS wakaruhusu ziuzwe. CAG amesema athari za bidhaa hizo ni kubwa.

Baadhi ya bidhaa hatari zilizoingizwa nchini ni sabuni za Omo, siagi aina ya Blueband, vinywaji vya kuongeza nguvu, mbolea, pikipiki, oili za magari, mafuta ya magari, mafuta ya ndege, betri, chupa za chai, ngano, maharage, misumari na bidhaa nyingine nyingi.

Tairi za magari aina ya Yana ziliingizwa nchini zikiwa hazina ubora, na kwamba licha ya kuzuiwa, TBS imekuwa ikiendelea kuziingiza zikiwa na alama ya Shirika la Viwango la Kenya (KEBS).

CAG amebaini kuwa kampuni ya Uniliver ya Kenya imekuwa ikiingiza nchini shehena ya siagi aina ya Blueband isiyokidhi viwango, lakini TBS wameiruhusu iuzwe.

Pamoja na siagi hiyo, CAG anasema bidhaa nyingine hatari zinazoingizwa nchini na Uniliver zikiwa hazina viwango ni sabuni aina ya Omo.

Imebainika kuwa bidhaa hizo zimekuwa zikipimwa na kubainika kuwa hazina ubora, lakini wenye mali wamekuwa wakitaka upimaji urejewe, na kwa kufanya hivyo, hupimwa na kuruhusiwa kuingizwa sokoni.

CAG katika mapendekezo yake, ametaka upimaji ufanywe mara moja, na kama unakuwapo ulazima wa kurudia, basi kazi hiyo ifanywe na wataalamu tofauti na wale waliopima awali.

“Kumekuwa na shaka ya usahihi wa upimaji wa ubora wa bidhaa kwenye maabara za TBS, kutokana na bidhaa nyingi awali zilizoonekana kutokidhi kiwango na baada ya kurudia kuonekana zinakidhi viwango. Hivyo hivyo, huenda kuna bidhaa nyingi zilizopewa vyeti vya ubora kumbe hazina ubora na kuingia nchini na madhara yake ni makubwa kwa afya za watumiaji,” amesema.

Kampuni ya Crop Care imebainika kuingiza nchini mbolea zisizokidhi viwango na kuruhusiwa kuzipeleka kwenye maghala yake na kisha kuzisambaza.

Kampuni ya Insignia imekuwa ikiingiza ‘Calcium carbonate’ ambayo mara zote imebainika kuwa haina ubora, lakini imeachwa ili iuzwe kwa wananchi bila kujali madhara yake.

Kampuni ya mafuta ya Kobil yenye asili ya Kenya, imebainika kuwa imekuwa ikiingiza shehena ya mafuta feki ya ndege. Ingawa TBS wamekuwa wakibaini dosari hizo, mara zote wameiachia iuze mafuta hayo yasiyofaa.

Kampuni hiyo imefanya hivyo pia kwa mafuta ya magari, na pale ilipobanwa, imekuwa ikiomba na kuruhusiwa kuchakachua kwa kuchanganya na mafuta yenye ubora na kisha kuyauza.

“Kobil (T) Ltd wamekuwa wakiingiza mafuta yasiyokuwa na uzito unaotakiwa na wamekuwa ‘wakifeli’ zaidi ya mara tatu kwa kuingiza mafuta yasiyokuwa na uzito unaotakiwa.

“Waliingiza mzigo wa mafuta Agosti 3, 2011 ulipopimwa haukuwa na viwango vinavyotakiwa. Baada ya hapo aliomba ruhusa kuchanganya mafuta hayo yaliyofeli testi ya uzito na mafuta yaliyokuwa kwenye matanki yake hapa nchini ili kupata uzito unaohitajika, na TBS wakaruhusu,” amebaini CAG.

Kwa upande huo huo wa mafuta ya magari, kampuni ya Hass Petrolium imehusishwa na uingizaji mafuta yasiyokidhi viwango na kuruhusiwa kuyauza. Baadhi ya wakubwa katika kampuni hiyo ni wafanyabiashara maarufu, wanasiasa na mawaziri kadhaa.

Katika ukaguzi huo, CAG amebaini kuwa kampuni ya Bonite Bottlers Ltd yenye makazi yake Moshi, iliagiza kinywaji aina ya ‘Burn-Energy’ kilichokuwa hakikidhi kiwango. TBS waliwaandikia barua waonane na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, ili kinywaji hicho kirejeshwe kilikotolewa au kiteketezwe.

CAG anasema; “Kwa maelezo tuliyoyapata kutoka kwa maofisa waandamizi wa Bonite Bottlers, walikiri kutokupokea barua hiyo ya TBS na kwamba bidhaa hiyo iliingia sokoni.”

Kampuni ya Setways Investment imekuwa ikiingiza betri kutoka Malaysia na kupewa kibali cha kutumia nembo ya TBS, lakini zilipopimwa hazikukidhi viwango.

“TBS wamekuwa wakilazimika kuziruhusu ziingie sokoni kuuzwa licha ya kutokidhi viwango kwa sababu tu zina nembo yao ya ubora. TBS wamewaandikia barua za onyo zaidi ya mara tatu ili wafanyie marekebisho bidhaa hizo, lakini hakuna kilichorekebishwa. Hali hii inadhihirisha udhaifu mkubwa katika usimamizi wa sheria zinazohusu TBS,” imesema taarifa ya CAG.

CAG amesema kwamba pamoja na kuwapo bidhaa za maelfu ya tani zisizofaa kwa matumizi ya binadamu, hakuna mahali popote kunakoonyesha kuwa bidhaa hizo, ama ziliteketezwa katika madampo au katika Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

“Kupitia rekodi za Baraza la Mazingira, katika kipindi cha mwaka 2002-Juni 2011 hakuna bidhaa ambazo TBS iliomba kibali cha kuziharibu, ukiachilia mbali mzigo wa majokofu uliopelekwa NEMC Desemba 20, 2011 ambao hata hivyo bado haujateketezwa,” amesema CAG.

Imebainika kuwa TBS mwaka jana, kwa nyakati tofauti iliiandikia barua Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikiomba gharama za kuteketeza bidhaa zisizo na ubora, mali ya Unity in Diversity Foundation Ltd (UDF).

“Halmashauri waliwajibu TBS Mei 3, 2011 na kuainisha gharama na mahali pa kuharibia bidhaa hizo. Hata hivyo, kwa mujibu wa Halmashauri, baada ya kulipia gharama za uteketezaji hawakurudi tena Halmashauri kwa utekelezaji wa kuteketezwa kwa bidhaa hizo feki. Bidhaa hizo zilikuwa ni ngano na maharage…Udhaifu wa aina hii ni hatari sana kwa walaji au watu wanaotumia bidhaa hizi,” amesema CAG.

CAG amebaini kuwa mfanyabiashara Abdallah Matembele ameingiza nchini pikipiki zisizokidhi viwango, ikiwa ni pamoja na kuwa na kiwango kikubwa cha hewa ya sumu ya ‘carbon monoxide’ kilichopindukia.

Imeelezwa kuwa pikipiki hizi zilipopimwa awali zilibainika kuwa na upungufu huo, lakini upimaji uliporudiwa ilionekana kuwa hazina matatizo. Hatua hiyo imemfanya CAG atilie shaka suala hilo.

Suala kama hilo linafanana na la kampuni ya uagizaji mbolea –  Tanzania Crop Care ambako CAG anasema; “Aliingiza mbolea ambayo kwenye testi ya kwanza kipengele cha ‘total nitrogen’ alipata 0.6 wakati kiwango cha chini kabisa kilipaswa kupata 13.0. Waliporudia kufanya testi upya mbolea hiyo ikapata 13.5 na kwa hiyo ikafikisha kiwango kinachotakiwa cha 13.”

Kumekuwapo pia uingizaji wa bidhaa zisizoonyesha zilikotengenezwa na namba ya utengenezaji, jambo ambalo ni kinyume kabisa na sheria. Hata hivyo, CAG anasema bidhaa hizo, zikiwamo chupa za chai, zimekuwa zikiingizwa nchini. Miongoni mwa waagizaji ni Denis Chacha Bony.

Katika ukaguzi huo, CAG amebaini matumizi mabaya ya nembo za TBS zenye maneno, ‘Imethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania’ au ‘Approved by TBS’, kwani mara nyingi bidhaa zenye maandishi hayo zimefeli kwenye testi.

CAG amebaini kuwa watengenezaji na waagizaji bidhaa wengi wamekuwa wakichapisha wenyewe maneno hayo na kuyaweka kwenye bidhaa zao bila uhakiki wa TBS.

CAG anasema kwamba hata pale inapobainika kuwa bidhaa hizo ni feki, TBS wameshindwa kuamuru zisiuzwe kwa wananchi kwa vile tayari huwa na nembo za shirika hilo.

Itaendelea wiki ijayo.