DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amepewa tuzo ya CEO Bora wa Mwaka 2022 kwa Benki za Afrika.

Mwanamke huyo raia wa Tanzania ametunukiwa tuzo hiyo wakati wa sherehe maalumu zilizofanyika jijini Nairobi, Kenya, wiki iliyopita kutokana na mchango wake binafsi katika kuiongoza Benki ya NMB pamoja na sekta ya benki kwa ujumla wake.

Tuzo hizo zinazofahamika kwa Kiingereza kama ‘Africa Bank 4.0 Awards’ huandaliwa na Kampuni ya Kimataifa ya Elimu, Tafiti na Ushauri ya BII World.

Ruth alipata heshima hiyo wakati wa mkutano wa nane wa African Bank 4.0 Summit.

Taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam inasema Mhasibu wa Benki ya NMB, Aziz Chacha, alipokea tuzo hiyo kwa niaba ya Ruth kutoka kwa CEO wa Kenya Institute of Bankers, Julius Alengo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Chacha, amesema tuzo iliyopatikana ni kwa heshima ya wadau wa Benki ya NMB.

“Kwa maneno ya Ruth mwenyewe, tuzo hii ni kwa ajili ya mtaji wetu mkubwa ambao ni watu wetu na wafanyakazi wa NMB. Hakika bila hawa huenda hili lisingewezekana,” amesema.

Katika kipindi cha uongozi wa Ruth, Benki ya NMB imejizatiti na kulinda nafasi yake ya kuwa benki inayotengeneza faida zaidi nchini, ambapo taarifa za kifedha za benki hiyo za hivi karibuni zinaonyesha kuwa faida waliyopata baada ya kuondoa kodi kwa mwaka 2021 ni Sh bilioni 290.

Mwaka jana NMB ilifanikiwa kufikisha wateja milioni tano, ikitumia teknolojia ya kisasa kufikisha huduma za kibenki kwa watu ambao awali hawakuwa wakifikiwa na huduma za benki.