Afya au siha (hygiene au health) ni hali ya mwili (physically) na akili (mentally) ilivyo kwa kadiri ya kila mtu binafsi anavyojisikia au kuonekana kwa wakati tofauti.
Afya inahesabika kuwa ni njema au nzuri mtu anapokuwa timamu, thabiti, na bila ya kuwapo kwa kasoro yoyote mwilini. Inaheasabika kuwa mbaya kama mtu ana dosari fulani mwilini au akilini. “Bora afya kuliko mali” – Msemo katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu (TUKI), kumaanisha kuwa afya ina thamani zaidi ya utajiri maishani.
Kuwa na afya njema kunamfanya mtu asiwe mlegevu katika kuendesha mambo yake. Huwa anayejumuika na watu wengine na kufurahia maisha, huku akiwa na uwezo wa kutekeleza majukumu na makusudio anayoyatarajia.
Na ni kule kuwa na ufahamivu wa jinsi mwili wake ulivyo ndiyo mtu huweza akafikiria, kutambua na kukatia shauri juu ya kinachofaa na kisichofaa kwa maisha yake na ya watu wengine.
IIi mtu aifanye afya yake iwe njema, pamoja na mambo mengine, viungo vya mwili wake mzima vinapasa viwe vinafanya kazi vyema na kwa kushirikiana. Katika kudumisha afya, vya muhimu kuzingatia ni lishe, mazoezi ya mwili, usingizi na mapumziko ya kutosha, usafi wa mwili na mazingira, utimamu wa kuendesha mambo na kuepukana na shida na matatizo:
Lishe
Vyakula vyenye lishe (nutrients) muhimu zimepangwa katika mafungu matano: (1) Wanga na sukari (carbohydrates), (2) mafuta (fats), (3) chembe zinazopatikana katika nyama, ute wa yai, samaki na mafuta yake (proteins), (4) vitamini (vitamins) na (5) madini (minerals).
Maji ni ya muhimu, lakini mara nyingi huchukuliwa kama ni kitu tofauti na lishe. Mahitaji ya mwili huhitilafiana kati ya mtu na mtu, kufuatana na umri, jinsia, na shughuli zao. Mwili hukosa lishe sahihi kutokana na kula hovyo kusikokidhi mahitaji ya mwili, vinginevyo kutokana na chakula kiingiapo mwilini kisiponyonywa au mwili unaposhindwa kuzitumia lishe hizo zinavyohitajika.
Mazoezi ya Mwili
Mazoezi ya mwili (body exercises) ni ya muhimu kwa afya njema. Mazoezi ya nguvu au mikiki huimarisha musuli, moyo na nyendo za damu, na kupumua, mbali na kuuwezesha mwili na akili kuhimili misukosuko.
Inafaa kila mtu ajichagulie aina ya mazoezi anayoyaweza. Kupanda baiskeli, kutembea harakaharaka (jogging), kuogelea na kutembea vitambo virefu; haya yote ni mazoezi mazuri kwa afya. Kucheza gofu au tenisi ni mazoezi mepesi na hayausaidii sana mwili. Madaktari wanasema mazoezi ya mara kwa mara huwafanya watu wawe wenye furaha zaidi, kuwa macho zaidi, wasiositasita kufanya mambo na kuvichangamsha viungo vya mwili.
Usingizi
Kulala usingizi ni wakati ambapo mwili huwa katika mapumziko makubwa, hata kufikia mtu asiweze kujua yanayotendeka katika mazingira aliyomo. Ndiyo maana Waswahili wakasema “usingizi ni nusu ya kifo”. Usingizini mapigo ya moyo na kasi ya kupumua huenda polepole.
Usingizi wa kutosha husaidia kuurejeshea mwili nguvu zilizopotea. Kwa muda gani mtu anahitaji kulala, jambo hili linatofautiana kati ya mtu na mtu. Watu wazima wengi huhitaji kwa siku walale kwa saa 7 hadi 8, wengine wanahitaji muda mrefu zaidi ama mfupi wa huo. Watoto wanahitaji muda zaidi wa kulala usiku na kwa vitambo vifupi vifupi nyakati za mchana.
Hutokea mtu akapatwa na tatizo la kukosa usingizi (insomnia), kutokana na mambo mbalimbali. Mathalan, mtu akiwa katika sehemu yenye kelele na pilikapilika, kuugua, maumivu, joto, wasiwasi na hofu. Na hili kama linakuwa ni tatizo la kuendelea siku nyingi, inafaa kumwona daktari. Dawa za usingizi hazifai kutumiwa bila ushauri wa daktari.
Mapumziko
Mapumziko, tafrija, starehe na burudani ni vitu vya muhimu sana kama ulivyo usingizi. Baada ya kazi ngumu au mazoezi mazito, mtu huhitaji apate mapumziko kamili. Anahitaji kujistarehesha kwa namna tofauti, hata kama ni kwa kuzubaazubaa tu mitaani. Kazi, mazoezi ya mwili na masomo navyo pia huchosha.
Itokeapo mapumziko na njia nyingine zinashindwa kuondoa mwilini yanayoudhi au kusumbua unyong’onyevu kama uchovu, na wasiwasi wa mawazo (distress), ujue una matatizo ya kimwili (physical) au akilini (psychological).
Usafi
Mwili unaoogeshwa au kunawishwa angalau mara moja kwa siku, huepushwa na maambukizo ya vijidudu vya magonjwa, uchafu na harufu mbaya pamoja na kuzuia maradhi ya ngozi. Hata hivyo, kuoga zaidi ya mara mbili kwa siku siyo vizuri, hupunguza mafuta katika ngozi, ambayo yana umuhimu wake kwa afya njema.
Usafi wa mazingira uzingatiwe kwa kutochafua vyanzo vya maji. Tusitupe taka hovyo kutoka majumbani mwetu. Tusiende haja (tusijisaidie) hovyo. Tupambane na kuangamiza vidudu kama mbu, kunguni, mchwa, viroboto, papasi na mainzi.
Nywele na kucha zinahitaji kusafishwa. Kupiga mswaki ni jambo la muhimu, kwani husaidia kuzuia kuoza kwa meno na maambukizo ya kwenye fizi. Inafaa kila inapowezekana kuonana na daktari wa meno. Ni jambo la busara kujikinga na magonjwa kuliko kusubiri yakupate ndipo uende kutibiwa. Utokewapo na chochote kinachoashiria hitilafu mwilini, nenda hospitali. Kujitibu mwenyewe kwa siku zaidi ya mbili, si jambo la busara.
Akili
Kuwa na akili timamu kunamfanya mtu amudu kujiweka katika hali njema ya afya ya kimwili na kiroho, na kutambua ukweli wa mambo yanayomhusu. Mtu mwenye akili timamu humudu kupambana na taabu, shida na dhiki zinazomfika. Hababaishwi na mambo yasiyomhusu au ya kipuuzi.
Yanayomkuta mtu akiwa utotoni au ujanani, humsaidia kuwa na ujuzi wa kukabiliana na mambo yanayomfika ukubwani. Utotoni mtu hutegemea wakubwa. Kadiri anavyokua hujifunza na kutambua mwendo upi wa maisha ndiyo unaofaa kuufuata au auendesheje, ili aishi vyema. Kadiri anavyokua kila mtu huwa akifanya makosa na kupata njia ya kujayaepuka. Kukomaa kwa akili za binadamu hakuishii wakati wa kukua kimwili na kubalehe tu, bali ni kitu cha kuendelea hadi uzeeni.
Shida na Dhiki
Taabu, shida, wasiwasi na dhiki (stress) huufanya mwili kukabiliwa na mambo ya kutishia maisha ya kila mtu. Mara nyingi hutokana na ukosefu wa ajira, kubeuliwa, ama mtu anapoachwa na awapendao. Hata hivyo, stress inaweza ikamjia mtu akiwa katika hali ya kawaida. Kwa mfano, wakati mtu akiwa anaangalia mashindano fulani, kukiwa na upande anaoupendelea ulingoni au uwanjani hupatwa na hali hiyo. Kama inavyokuwa pia wakati mtu akiwa anasubiri habari za mgonjwa wake anayefanyiwa operesheni, ama habari za mjamzito wake anayetazamiwa kujifungua wakati wowote. Na kama hali hizi hazidhibitiwi ipasavyo, hatimaye mtu huyo anaweza akaugua mwilini ama akilini.
Dalili za stress ni pamoja na kuumwa na kichwa, kupata kikohozi kisicho na msingi na hata kuwa na harara ya kwenye ngozi na kutokwa na jasho, hasa katika nyayo na kwenye viganja vya mikono. Kama hali hii inafikia kiwango cha juu, mtu anaweza akapatwa na shinikizojuu la damu (hypertension), au ajiwe na vidonda vya tumbo (ulcers). Visababishi na dalili anazokuwa nazo mtu aliye na stress, vinakaribiana na anavyokuwa navyo mtu mwenye mapigo ya juu ya moyo (hypertension).
Kwa jumla, afya ya kila mtu ni jambo la kunufaisha au kuwa la maangamizi kwa nchi na taifa zima, kama si dunia nzima. Hasa tukichukulia jinsi maambukizo ya magonjwa yanavyosambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine, nchi na nchi au taifa moja hadi jingine.