Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Kibaha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imejenga shule za Msingi mpya mbili,Madarasa 13 na Matundu ya Vyoo 21 kwenye shule 8 za Halmashauri ya Mji Kibaha Mkaoni Pwani zilizogharimu shilingi 1.280,300,000 kupitia Mradi wa BOOST.
Shule mpya zilizojengwa ni Kongowe na Miembesaba zote zikiwa Kata ya Kongowe kwa shilingi 950,600,000 zikihusisha miundombinu yote ya muhimu wakati wa kuanzisha shule mpya na kiasi cha shilingi 332,400,000 zikitumika kujenga madarasa 13 na matundu ya Vyoo 21 kwenye shule 6 Kongwe.
Alice Gombanila ni Afisa Elimu takwimu na vielelezo Halmashauri ya Mji Kibaha amesema Serikali kwa Mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI ilifanya uamuzi sahihi kuleta mradi wa BOOST kwani kwa madarasa 13 yaliyojengwa zaidi ya Wanafunzi 585 wamepata mahali bora pa kusomea
Aidha,Afisa Elimu Msingi na Awali wa Halmashauri ya Mji Kibaha Bernadina Kahabuka amemshukuru Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza shule mpya mbili zinazolenga kupunguza Msongamano kwenye shule za Kata ya Kongowe na Kata jirani kwani Madarasa mapya 32 yanakwenda kuwanufaisha zaidi ya watoto 1440 wakati wa masomo hivyo kuboresha Mazingira na kujifunza na ujifunzaji
Protas Dibogo ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha ameeleza kuwa kazi ya ujenzi na usimamizi wa mradi wa BOOST ilifanywa Mchana na usiku kwa kuzingatia muda,ubora na thamani ya fedha ili kutimiza ndoto za Mhe.Rais Samia hivyo ametoa rai kwa wanafunzi na walimu kuitunza miundombinu hiyo ili itumike kwa kizazi kilichopo na kijacho kwa maslahi mapana ya Taifa na Dunia kwa ujumla
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Mussa Ndomba kwa niaba ya wananchi amemshukuru na kumtakia afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kuwaongoza vema Watanzania.